NORA DAMIAN -KAGERA
MGOMBEA urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia CCM, Dk. John Magufuli amesisitiza hana mpango wa kuongeza muda wa urais na ataondoka madarakani baada ya muda wake kuisha.
Akizungumza jana eneo la Kemondo akiwa njiani kwenda Bukoba mjini mkoani Kagera, Dk. Magufuli alisema kazi ya urais ni ngumu ndiyo maana anataka akimaliza muda wake apumzike.
“Urais ni mateso, kazi yoyote ukitaka kuifanya vizuri ni mateso, na ndiyo maana ninasema kwa dhati nikishamaliza hii miaka mitano iliyobaki sitaki niongezewe.
“Watapatikana wengine ndani ya CCM ili na mimi nipumzike niwaangalie wenzangu wakifanya kazi.
“Bahati nzuri ndani ya chama palikuwepo na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alifanya miaka yake akapumzika akatutoa kwenye ukoloni, vita vya Uganda vikaja akatutoa. Akaja mzee Mwinyi akaendelea na ruksa, akafanya kazi yake katika miaka kumi… angeweza kuendelea, lakini akasema imetosha.
“Akaja mzee Mkapa, na mimi nimefanya kazi na mzee Mkapa miaka kumi nikiwa waziri, amemaliza miaka yake kumi akapumzika. Amekuja mzee Kikwete amefanya miaka yake kumi amepumzika.
“Mimi nimekuja nimefanya miaka mitano, ndiyo maana ninaomba niongezewe ile mitano mingine iliyobaki nikafanye maajabu kwa ajili ya maendeleo ya nchi hii,” alisema Dk. Magufuli.
MUSTAKABALI WA TAIFA
Dk. Magufuli aliwataka Watanzania kujitambua na kuepuka kuwachagua watu wenye tamaa ya kura kwani wanaweza kuja kutawala kwa matakwa ya watu wengine.
Alisema Tanzania inakua kwa kasi, hivyo inahitaji msukumo wa kipekee wa watu watakaoweza kutoa uamuzi na kuwataka Watanzania kukichagua chama chake kiweze kuwaletea mabadiliko ya kweli.
“Msibabaishwe na maneno machafu, muangalie na kupima maneno wakati huu wa kampeni msije mkatolewa kwenye njia ya amani na usalama, tutapotea.
“Hamtapata Serikali kuwagawia pesa, hata maandiko hayasemi hivyo, mara mnaambiwa hakuna kulipa kodi, mtaendesha nchi bila kulipa kodi? Hata Ulaya wanalipa kodi.
“Unaweza kujaribu mengine, lakini usijaribu kuchagua utajuta miaka mitano, chagueni watu ambao wakiambiwa fanya hili wana uwezo wa kusema sifanyi, mustakabali wa taifa letu ndicho kitu kikubwa,” alisema Dk. Magufuli.
MIRADI YA MAENDELEO
Dk. Magufuli aliahidi kuibadilisha Bandari ya Kemondo ili iwe kitovu cha biashara katika Mkoa wa Kagera.
Aliagiza wavuvi kutozwa ushuru wa Sh 100, badala ya Sh 300 huku akiahidi pia kushughulikia kero za wakulima wa kahawa na wafanyabiashara wengine.
“Kemondo ndiyo mahali palipoleta utajiri kwa wananchi, ndiyo bandari iliyoanzishwa na Baba wa Taifa, baada ya ajali ya MV Bukoba ikapita karibu miaka 20 hatukuweza kuleta meli nyingine, tunatumia barabara.
“Tumeanza kununua na kukarabati meli tano kwa gharama ya Sh bilioni 152, MV Victoria tumenunua injini mpya kubwa, inaweza kubeba watu 1,200 na tani 400.
“Kemondo ninaifahamu, hapa tutapabadilisha, tunataka iwe bandari kubwa ya watu kufanya biashara, lazima ‘uji-commit ‘ ndani ya moyo wako kwa ajili ya kuwatumikia maskini.
“Vitu hivi vyote nilivyovianzisha tukiviacha hakuna wa kuvitengeneza, tukiondoka kabla hatujakamilisha haya, mtu anaweza akauza vyuma chakavu,” alisema Dk. Magufuli.
Pia aliahidi kuboresha miundombinu kwa kujenga barabara nyingi zaidi za lami, kujenga vituo vya afya, hospitali na kukarabati zingine zilizopo, upatikanaji wa maji na kumalizia kusambaza umeme katika vitongoji 116.
“Sisi tunaamini kupitia ilani ya uchaguzi mambo mengi yameelezwa, tuliyoyafanya miaka mitano iliyopita ya miaka hii (mitano ijayo) ni mengi zaidi, naomba mtuamini, tumejipanga kufanya makubwa zaidi.
“Ujenzi wa Hospitali ya Wilaya Malahala ambayo imekwama kwa zaidi ya miaka mitano, mgombea ubunge na diwani mtakapochaguliwa iwe ndiyo ‘issue’ ya kwanza kuniletea, hii ndiyo iwe kipaumbele, barabara ya Nshamba kilomita 36 mniachie nikichaguliwa nitaomba mje mnione, hili nilibebe kwa heshima ya watu wa Muleba.
“Matatizo hayawezi yakaisha siku moja, lakini tuko pamoja na ninyi, tumefanya ya kitaifa, kijijini mpaka vitongoji, tunaomba miaka mitano ili kero zilizobaki tuweze kuzimalizia,” alisema Dk. Magufuli.
Akizungumzia mafanikio ya Wilaya ya Muleba kwa kipindi cha miaka mitano, Dk. Magufuli alisema wametekeleza miradi yenye thamani ya Sh bilioni 65.32.
Alisema katika upande wa afya walitumia Sh bilioni 18.57 ambapo Sh bilioni 14.8 zilitumika kununua dawa na vifaa tiba, kujenga vituo vya afya na kufanya upanuzi wa vituo vingine kwa kujenga wodi ya mama na mtoto pamoja na chumba cha upasuaji.
Dk. Magufuli alisema pia wamejenga vituo vya afya vitano ambapo kila kituo kimegharimu kati ya Sh milioni 400 hadi 500.
Alisema Sh bilioni 9.946 zilitumika kugharamia elimu bila malipo, wakati Sh bilioni 8.4 zilitumika kujenga mabweni na shule ya msingi maalumu ya Kaigala, kukarabati Chuo cha Veta Kamachumu, chuo cha ualimu, madarasa na maabara.
Dk. Magufuli alisema pia wamefikisha umeme katika vijiji 124 kwa gharama ya Sh bilioni 4.4 na vimebaki vijiji 42 ambavyo aliahidi ndani ya miaka mitano ijayo watavimaliza.
KUMPA KAZI TIBAIJUKA
Awali akiwa Jimbo la Muleba, Dk. Magufuli alimpongeza mbunge aliyemaliza muda wake, Profesa Anna Tibaijuka na kuahidi kumtafutia kazi kwani bado anahitajika kuisaidia Serikali.
“Huyu (Profesa Tibaijuka) ni dada yangu, nilipokuwa naibu waziri wa ujenzi na mbunge wa Chato, marehemu mume wake alikuwa balozi wa Sweden, kwa hiyo huyu ni dada yangu.
“Mama Tibaijuka amesema amestaafu, lakini kwangu mimi hajastaafu, hii ndiyo faida ya kuwa na watu katika mahali fulani ambapo wanaweza kusaidia Serikali.
“Bashiru hakutegemea kuwa katibu mkuu wa chama, alikuwa anauza ndizi pale Kemondo baadaye alienda chuo kikuu akafundisha, lakini leo hii ndiye katibu mkuu Tanzania nzima.
“Serikali ina mavyeo mengi, mimi namwambia ProfesaTibaijuka hajastaafu licha ya yeye kusema amestaafu, hatuwezi kumuacha profesa anakaa wakati kuna maeneo mengi anaweza kwenda kufanya,” alisema Dk. Magufuli.
Aidha kwa nyakati tofauti, aliwaombea kura wagombea ubunge wa majimbo ya mkoa huo wakiwemo Dk. Oscar Kikoyo (Muleba) na Charles Mwijage (Muleba Kaskazini) na kuwataka wanachama wengine waliogombea kura za maoni kuwaunga mkono waliopitishwa na chama badala ya kuendekea kubishana kwani chaguzi zilishamalizika.
“Msifanye mzaha, haya mambo yenu ya kubishana bishana yatawatesa, kura za maoni tumemaliza walioshinda wameshinda. Sisi ndani ya CCM yameisha, ni lazima mjue kuna wakati ambao ni wako na kuna wakati utakuja wa mwingine.
“Nawaomba waliogombea na mheshimiwa Mwijage na Dk. Kikoyo ‘wawa-support’, sisi chama tunajua, twende mbele tupeleke maendeleo mbele.
“Tunatakiwa sisi wana Muleba tuwe kitu kimoja, tumefanya chaguzi ndani ya CCM, walijitokeza wengi sisi chama tulichambua, aliyeongoza, aliyekuwa wa pili tunafahamu, tukaona wote wazuri lakini yupo ambaye ni mzuri zaidi.
“Ya Chama Cha Mapinduzi mtuachie sisi tunajuana, hata mimi nilipogombea urais walikuwa watu 42, hawawezi wote wakawa marais. Dk. Kikoyo ni kijana wenu, inawezekana ana madhaifu yake msameheni, naomba shikamaneni wa vyama vyote, hata ukiwa huna chama kampigie kura Dk. Kikoyo,” alisema Dk. Magufuli.