30.1 C
Dar es Salaam
Friday, December 2, 2022

Contact us: [email protected]

Salma Kikwete: Nitampigia hodi Magufuli kutatua kero za Mchinga

Mwandishi Wetu, Lindi

Mgombea Ubunge wa Mchinga kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Salma Kikwete, amesema atampigia hodi Rais Dk. John Magufuli kwa ajili ya kumuomba amsaidie kutatua kero za jimbo hilo.

Akizungumza juzi na jana ikiwa ni mwendelezo wa mikutano yake tofauti ya kampeni iliyofanyika katika kata za Rutamba na Mvuleni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu, Salma, aliwataka wapiga kura wa jimbo hilo lililopo mkoani Lindi kumchagua yeye kwa sababu ana uwezo wa kwenda kokote kupeleka matatizo yao yakasikilizwa na kutatuliwa.

“Mlikosa mtu wa kupeleka kero na matatizo yenu bungeni ndiyo maana mnashuhudia hiki kilichopo sasa kwa jimbo letu kukosa maendeleo, hii hali bado mnaitaka? Wenzenu wa maeneo mengine wanajengewa shule, vituo vya afya, zahanati na barabara, sasa nichagueni ili tuweze kupata maendeleo na kuwawakilisha bungeni kwa sababu mwanzo mlikosa kiunganishi,” alisema mama Salma.

“Mimi nina uwezo wa kwenda kokote nikasikilizwa kwa haraka, hata kwa Rais Magufuli nikigonga mlango atanifungulia kwa haraka kwa hiyo nipeni madaraka hayo tuweze kushughulikia kero zote za jimbo hili.”

Pia akiwa Mvuleni, alisema atashughulikia changamoto za eneo hilo ikiwamo ujenzi wa ofisi ya kata na vijiji ambao kwa sasa uko katika hatua za awali pamoja na uboreshaji wa huduma za maji safi na salama.

Salma alisema lazima watekeleze mpango wa matumizi bora ya ardhi kwa kutambua mipaka ya maeneo ya kata hiyo na kuhusu suala la afya alisema atahakikisha huduma katika eneo hilo zinaboreshwa ili kusitokee tena vifo vya wajawazito na watoto wachanga wakati wakijifungua.

“Kwa kushirikiana na diwani wa eneo hili nitazichukua kero zote za eneo hili ikiwamo ya afya na kuzisemea bungeni, matatizo yote haya mnayoyaona sasa hivi ni kwa sababu jimbo hili halikuwa chini ya CCM, masuala ya maji na barabara kutopitika mwaka mzima na mengine yote ya Mchinga nitayazungumza bungeni,” alisema na kuongeza:

“Mkinichagua mimi yatashughulikiwa, sikugombea jimbo hili ili kumpinga yeyote ndani ya CCM bali ni kutaka kutoa mchango wangu ndani ya Mchinga kwa sababu niliumia sana jimbo hili kuwa chini ya upinzani, sasa chagueni mafiga matatu kwa maana madiwani wa CCM, mbunge wa CCM awe kiunganishi chenu na mchagueni Magufuli ili tupate maendeleo ya jimbo letu.”

Akiwa Rutamba, Salma alisema ataboresha shule ya eneo hilo kwa kuhakikisha walimu wanaongezeka na wanafunzi waweze kusoma kidato cha kwanza hadi cha nne, cha tano hadi cha sita kisha waende kusoma vyuo vikuu.

Pia alisema atafuatilia mradi wa maji katika eneo hilo la Rutamba wenye thamani zaidi ya Sh milioni 300 unaocheleweshwa na mkandarasi ili ijulikane kama ameshindwa kazi kwa sababu zake binafsi au ameshindwa kwa jambo jingine.

“Mradi huu lazima ukamilike, hilo suala niachieni mimi, tutawasiliana na diwani na tutalifanyia kazi na tutafuatilia tujue kama sababu za mkandarasi kushindwa kazi ni zake binafsi tutajua na kama sababu ni zetu tutajua ili kuhakikisha unakamilika kama inavyotakiwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Salma, alisema atahakikisha wanawake, vijana na watu wenye ulemavu wanapata asilimia 10 ya fedha za mikopo zinazotengwa na halmashauri kupitia vikundi watakavyoviunda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
205,507FollowersFollow
558,000SubscribersSubscribe

Latest Articles