Nora Damian, Bahi
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli, amesema ataendeleza jitihada za kuboresha elimu, vituo vya afya, kujenga shule, madarasa na huduma zote za kijamii kwa kukamilisha alipoishia.
Akizungumza leo Septemba Mosi wakati wa mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Sokoni wilayani Bahi Mkoa wa Dodoma, amesema yako mengi yaliyofanyika katika mji huo.
Ameyataja baadhi ya mambo yaliyotekelezwa katika mji huo kuwa ni ujenzi wa hospitali ya wilaya unaogharimu Sh bilioni 1.8 ambao amefikia asilimia 95, vituo vitatu vya afya (Bahi, Chifukuta na Mdemu) uliogharimu Sh bilioni 1.5.
Mafanikio mengine ni ujenzi wa shule tatu, madarasa 51, Sh bilioni 2.1 za elimu bila malipo, kupeleka umeme katika vijiji 43 na mradi wa maji katika vijiji vya Mdemu, Nguji, Bahi Mjini, Magaga, Mkakatika uliogharimu Sh bilioni 2.9.
“Miaka mitano iliyopita nilipita Bahi nikawaomba kura kwa lengo moja tu la kuleta maendeleo katika nchi yetu, mikoa na wilaya zetu.
“Ninajua yako mengi ambayo yamefanyika na ninyi ndiyo mashahidi, ninajua yaliyofanyika mji wa Bahi haikuwa hivi, sasa hivi mji umepanuka unapendeza.
“Miaka mitano ijayo tutaendeleza jitihada kwa kukamilisha pale tulipoishia, tutaendelea kuboresha elimu, vituo vya afya, kujenga shule na madarasa na huduma zote za kijamii.
“Ndiyo maana nimekuja tena kuwaomba kura nimalizie viporo, nimebaki na deni kubwa kwenu sitawaangusha, ninaomba siku ya tarehe 28 mwezi wa kumi mtakapokwenda kupiga kura msisahau jina la John Pombe Magufuli…nitaomba mnichagulie na madiwani na mbunge wa Bahi,” amesema Dk. Magufuli.