30.7 C
Dar es Salaam
Thursday, December 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM na kiu ya Tanzania mpya

 NORA DAMIAN

NAOMBA makaribisho haya yaendane na kura nitakazozipata tarehe 28, kishindo hiki kikawe cha kweli, nataka siku moja nikija hapa mtuulize uliahidi hiki kiko wapi, nataka kuwathibitishia tutayatimiza kwa ‘speed’ kubwa…nitakuwa mwaminifu kwenu sitajikweza,” anasema Dk. John Magufuli katika moja ya mikutano yake ya kampeni.

Dk. Magufuli ambaye anaomba ridhaa ya Watanzania aweze kuwaongoza tena katika ngwe ya pili, hadi sasa ameshafanya mikutano ya kampeni katika mikoa saba tangu Chama Cha Mapinduzi (CCM) kizindue kampeni zake Agosti 29.

Mikoa ambayo Dk. Magufuli amefanya mikutano hiyo ni pamoja na Dodoma, Singida, Tabora, Shinyanga, Simiyu, Mara na Mwanza.

Katika maeneo yote anakopita Dk. Magufuli amekuwa akipata mapokezi makubwa kutoka katika makundi mbalimbali ya watu sambamba na maelfu ya wale wanaojitokeza katika mikutano yake.

Wako wengine pia ambao wamekuwa wakijipanga pembezoni mwa barabara anakopita Dk. Magufuli na kumlazimu kusimama mara kwa mara kuzungumza nao.

Aidha, kwenye maeneo ambayo yanatengwa kwa ajili ya mikutano ya mgombea huyo wananchi wamekuwa wakifurika kuanzia saa 12 asubuhi na licha ya wakati mwingine kuwa na hali ya mvua bado mwitikio umeendelea kuwa mkubwa.

Mfano katika Jiji la Mwanza ambako Dk. Magufuli alifanya mkutano juzi, asubuhi kulikuwa na mvua lakini bado maelfu ya wakazi walijitokeza kwa wingi katika uwanja wa CCM Kirumba.

Dk. Magufuli anatumia fursa ya mikutano hiyo kueleza mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na yale atakayoyafanya kwa miaka mitano ijayo huku akisisitiza kuwa amejipanga vizuri katika maeneo yote kwa ajili ya kuleta mabadiliko ya kweli nchini.

Maeneo hayo ni pamoja na kuimarisha miundombinu ya usafiri wa barabara, reli, majini, anga, sekta za viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi pamoja na upatikanaji wa huduma muhimu kama vile umeme, maji na elimu.

Mara zote katika mikutano hiyo amekuwa akiwaeleza Watanzania kwamba bado ana deni kubwa la kuwatumikia na kwamba wameshapanga mikakati mingi ya kufanya ambayo ipo katika ilani ya uchaguzi na kuwaomba wamuamini.

Anasema miaka mitano iliyopita maeneo mengi nchini hayakuwa kama yanavyoonekana sasa kwani kuna mabadiliko makubwa hasa ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, madaraja, hospitali, shule na usambazaji wa maji na umeme hasa maeneo ya vijijini.

 Mgombea wa Urais kupitia Tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM, Rais Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akiwapungia mkono wananchi waliofurika katika uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kabla ya kuanza kuhutubia

 “Tumekuwa pamoja katika shida lakini tumekuwa pamoja katika raha, tuliyoyafanya ni mengi, tumekuja na ilani ya uchaguzi zaidi ya kurasa 303 mimi pamoja na wabunge na waheshimiwa madiwani watakuwa na jukumu la kuyatekeleza.

“Ninawaomba kura ili tuweze kutengeneza Tanzania mpya, katika kipindi cha miaka mitano Tanzania imevuka ‘level’ ya uchumi wa chini na kwenda uchumi wa kati, nina uhakika tutafanya maajabu…tuaminini tukafanye maajabu katika kipindi cha miaka mitano.

“Hatuombi kwa sababu ya madaraka, hatuombi kwa sababu tunataka sifa, tunaamini tutawafanyia kazi kwa sababu tuna upendo na jukumu la kuiletea maendeleo nchi yetu,” anasema Dk. Magufuli.

Anasisitiza kuwa anataka tochi ya maendeleo iendelee kuwaka kama alivyoanza na kipindi chake atawatumikia Watanzania kwa sababu hiyo ndiyo sadaka yake.

 Dk. Magufuli anasema ataendelea kuboresha huduma za afya, elimu, maji, umeme, ujenzi wa stendi, masoko, utatuzi kero za wakulima na wafanyabiashara, usafiri wa nchi kavu, majini na anga, masilahi ya wafanyakazi na kuongeza fursa za ajira.

“Nataka niitengeneze Tanzania iwe Ulaya ili wa Ulaya wawe wanakuja Tanzania, hakuna sababu ya kwenda kuchungulia treni za umeme Ulaya wakati una uwezo wa kutengeneza. Nataka kipindi changu cha miaka kumi niwatumikie Watanzania kwa sababu hiyo ndiyo sadaka yangu.

“Ninafahamu changamoto za nchi hii ni nyingi, kazi yangu na Serikali yangu ni sadaka kwa Watanzania wanyonge. Mimi matusi niyapate lakini ninyi mpate maendeleo ya kweli kwa faida ya wanyonge na Watanzania kwa ujumla.

“Ninawaomba kwa upendo mkubwa sana mturudishe tena kwa miaka mitano muyaone maajabu tutakayofanya,” anasema Dk. Magufuli.

MUSTAKABALI WA TAIFA

Dk. Magufuli anasema kuongoza nchi ni kazi kubwa na kuwataka Watanzania kutafakari mahali walipotoka, walipo na wanakoelekea kwa mustakabali wa taifa.

“Watu wanahitaji maisha yaliyo bora, kama ni huduma za afya wanazitaka, huduma za elimu wanazitaka, sisi tunataka maendeleo kwa Watanzania wote bila kubagua dini, vyama ndiyo maana tunawaomba mtupe kura za kutosha.

“Tunataka taifa hili liendelee kwenda mbele, ninawaomba tena kwa mara nyingine niwe rais wenu,” anasema Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli anasema ana mipango mikubwa ya kusaidia vijana ikiwemo kufufua viwanda vitakavyoongeza fursa za ajira.

“Tumejenga vituo vya afya, tumejenga hospitali tunataka haya tuyaendeleze. Suala la maji tuna miradi mikubwa imetekelezwa na mingine inaendelea, ninaomba muamini tuko tayari kutimiza ahadi zetu tulizopanga,” anasema Dk. Magufuli.

Kwa upande wa nishati ya umeme ambayo ni muhimu katika maisha ya kila siku, Dk. Magufuli anawaahidi Watanzania kuwa ndani ya miaka mitatu vijiji vyote vilivyosalia nchini 2,600 vitakuwa na umeme.

Takwimu zinaonyesha mwaka 2015 vijiji 2,018 ndivyo vilikuwa na umeme na hadi sasa vimeongezeka na kufikia 9,570 kati ya vijiji 12,228 vilivyopo nchini.

“Uongozi unapimwa na sisi ndugu zangu mmeshatupima vya kutosha, haya tumeyapanga na kuyaweka kwenye ilani ya uchaguzi kwa sababu tunataka tujenge nchi yenye uchumi wa kweli.

“Nafikiri tunaweza ndiyo maana nilifikiri ni wakati mwafaka kunipa tena kura nimalizie yaliyobaki.

“Kuongoza ni kutoa lengo ndicho tunachokifanya kwa maendeleo mapana ya nchi yetu, mimi bado naamini tuna mambo mengi ya kufanya katika nchi hii na hasa kuibadilisha,” anasema Dk. Magufuli.

Dk. Magufuli anasema katika nchi yoyote ukitaka kujenga uchumi ni lazima uanze na vitu vinavyochochea uchumi.

“Huwezi ukataka uchumi wakati vitu vinavyochochea uchumi hujaviendeleza. Niliona tutumie mbinu ya kujenga uchumi wa kisasa ndio maana tulianza na miundombinu, mafanikio haya halafu nikose kura ndugu zangu…hata wanaonitukana inawezekana wanasahau kwamba wananitukana wakiwa kwenye lami,” anasema Dk. Magufuli.

MATARAJIO WALIYONAYO 

WANANCHI

Mkazi wa Bariadi mkoani Simiyu, Magu Sita (73), ambaye alikuwa mmoja wa wananchi waliojitokeza katika mkutano wa kampeni uliofanyika viwanja vya Shule ya Msingi Somanga anasema; “Uongozi unaoendelea mimi naona rais wetu ameongoza nchi vizuri hasa ukichunguza vitu vilivyolala na vikafufuliwa, tunaendelea kumuombea katika uongozi wake. Vitu vingi amefanya, Simiyu tulikuwa tuna hali mbaya ya umeme yaani watu walikuwa wananyanyasika sasa hivi wanatulia.

Mkazi mwingine wa mkoa huo, Mandi Kulwa anasema; “Hapa Simiyu ametufanyia mambo mengi mazuri zahanati, shule, maji umeme yaani ametufanyia mambo mengi kweli hatuwezi tukamsahau.

Naye mkazi wa Mwanza, Benja Mwamungesha anasema Dk. Magufuli ameiongoza nchi vizuri hasa kwa kujali maisha ya wanyonge.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Heri James, anasema vijana wana kila sababu ya kumsaidia Dk. Magufuli kuibuka na ushindi kwani amefanya mambo mengi yaliyoongeza fursa kwao.

Anasema Dk. Magufuli ameongeza fursa kwa vijana kupitia maboresho makubwa aliyoyafanya kwenye sekta za afya, elimu, viwanda na miundombinu.

Anatoa mfano wa miradi mbalimbali kama ya uboreshwaji wa bandari na viwanja vya ndege nchini kwamba imetoa fursa ya ajira kwa vijana na kukuza sekta ya biashara.

MSINGI WA ILANI

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Rodrick Mpogolo, anasema ilani ya mwaka huu ni kubwa kuliko za miaka iliyopita na kwamba lengo ni kuendelea kustawisha maisha ya Mtanzania, kutokomeza umaskini na kuimarisha misingi ambayo imewezesha Tanzania kuingia katika uchumi wa kati.

“Chama Cha Mapinduzi kimeleta mgombea madhubuti, mgombea bora ambaye ana uwezo wa kuongoza zaidi ya miaka 20, CCM inaenda kushinda kwa sababu ni chama madhubuti, kina nguvu, kimetawala tangu nchi ipate uhuru,” anasema Mpogolo.

Vipaumbele sita vilivyomo katika Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 ni pamoja na kulinda na kuimarisha misingi ya utu, usawa haki na uongozi bora ili kudumisha amani, umoja na mshikamano wa taifa, kukuza uchumi wa kisasa, fungamishi, jumuishi na shindani uliojengwa katika msingi wa viwanda, huduma za kiuchumi na miundombinu wezeshi.

Pia vimo vya kuleta mageuzi ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuwa na uhakika wa chakula wakati wote na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya uchumi, kuimarisha upatikanaji wa huduma bora za afya, elimu, maji, umeme na makazi vijijini na mijini.

Vingine ni kuchochea matumizi ya utafiti, sayansi, teknolojia na ubunifu kama nyenzo ya maendeleo ya haraka ya kijamii na kiuchumi na kuongeza fursa za ajira milioni nane

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles