29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, Museveni waeleza reli, bandari zitakavyoboresha biashara

Na ANDREW MSECHU

RAIS Yoweri Museveni wa Uganda amewasili nchini kwa ziara binafsi ya siku moja na kupokewa na mwenyeji wake, Rais Dk. John Magufuli huko Chato mkoani Geita, huku wakieleza reli ya kati, SGR na bandari ya Mwanza zitakavyosaidia biashara.

Akizungumza baada ya kumpokea mgeni wake, Rais Magufuli alisema sasa biashara baina ya Tanzania na Uganda itakuwa rahisi zaidi, kwa kuwa wanaweza kusafirisha mizigo kutoka nchini humo kwa kutumia meli na kuunganisha kwa njia ya reli hadi Bandari ya Dar es Salaam.

“Tayari tuna meli kubwa ya mizigo kwenye Ziwa Victoria, kwa hiyo unaweza kusafirisha mizigo kutoka Uganda hadi Dar es Salaam kwa gharama nafuu sana. Lakini pia tayari tumeondoa baadhi ya kodi na vizuizi barabarani ili kurahisisha usafirishaji.

 “Tunaendelea kujitahidi kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuwezesha wananchi wafanye biashara na hapo ndipo utajiri utakapokuja,” alisema Rais Magufuli. 

Alisema Rais Museveni anastahili kupongezwa kwa uamuzi mgumu alioufanya wa kuhakikisha bomba la kusafirisha mafuta kutoka nchini kwake linapita Tanzania, likiwa na urefu wa kilometa 1,440 na kupita katika mikoa minane, kutoka Hoima nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga.

Rais Magufuli alisema uamuzi huo unaonesha kuwa Rais Museveni anakumbuka alikotoka na kuwa damu za Watanzania zilizomwagika katika vita ya kumwondoa Iddi Amin nchini Uganda hazikumwagika bure.

Alisema tayari Serikali imeanzisha mbuga tatu za wanyama katika ukanda huo ambazo ni Hifadi ya Taifa ya Burigi aliyoizindua wiki hii, ambayo inashika nafasi ya tatu kwa ukubwa, baada ya Serengeti na Ruaha.

“Serikali pia imeanzisha Hifadhi ya Taifa ya Rumanyika na ya Rubanda na kwamba iwapo zitatumika ipasavyo zitasaidia kuinua uchumi kupitia utalii, kwa kuzishirikisha nchi zote za Afrika Mashariki.

 “Kwa sasa ukiangalia watalii wote wanaokuja katika nchi za Afrika Mashariki, hawafikii hata nusu ya wanaokwenda Misri pekee.

“Misri kwa mwaka inapata watalii zaidi ya milioni 10. Morocco inapata zaidi ya watalii milioni tisa, sisi wa Afrika Mashariki, kwa pamoja watalii wanaokuja hawafiki hata milioni tatu, kwa hiyo juhudi zaidi za kuhamasisha utalii zinahitajika,” alisema Rais Magufuli.

Alisema Tanzania na Uganda zimekuwa na uhusiano mzuri wa kihistoria japokuwa uliyumba kidogo miaka ya 1970 baada ya kuingia madarakani kwa Iddi Amin, lakini sasa Rais Museveni ameendelea kuwa kiungo muhimu cha kuendeleza undugu.

RAIS MUSEVENI

Akizungumza baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Chato jana, Rais Museveni alisema anaamini reli ya SGR ikifika Mwanza itawarahisishia kusafirisha mizigo yao.

Alimpongeza Rais Magufuli kwa mradi huo huku akisema anapofika Tanzania ni kama anakwenda hijja, kutokana na mchango mkubwa alioupata kwenye mafanikio yake ya kisiasa.

Museveni alisema wakati Waislamu wakienda kuhiji Macca na Wakristo wakienda Roma, yeye sehemu ya hijja yake ya kisiasa ni Tanzania.

Alisema Tanzania inakuwa sehemu ya hijja kwa wanasiasa wengi kutokana na mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuhakikisha nchi zote za Bara la Afrika zinakuwa huru, mchago wake mkubwa ukionekana kwa nchi za Kusini mwa Afrika.

Rais Museveni alisema hata baada ya uhuru, nchi nyingi zinakabiliwa na changamoto ya maendeleo kutokana na kuongezeka kwa kasi idadi ya watu, hivyo ni vyema kuhakikisha amani inakuwepo ili kuwawezesha kubuni miradi na kuzalisha ajira.

“Ni wazi kuwa Serikali haiwezi kuwapa ajira watu wote, kwa kuwa miongoni mwa watu milioni 40, Uganda ina uwezo wa kutoa ajira 470,000 tu, hivyo ni lazima Serikali iangalie namna ya kuwezesha watu kuzalisha mali kupitia sekta binafsi,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles