24.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: Msishangae nikimteua mwanajeshi kuwa Mkuu wa Magereza

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli amesema Jeshi la Magereza lisishangae siku moja akamteua mwanajeshi kuwa Mkuu wa Magereza.  

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa nyumba za makazi ya Askari Magereza wa Gereza la Ukonga na kuagiza mradi huo ukabidhiwe kwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) baada ya kubaini kuwa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) imeshindwa kutekeleza mradi huo kwa wakati, licha ya Serikali kutoa Sh bilioni 10 za ujenzi.

“Nimemuona Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, anasema Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi wakutane, wameshakutana? Si ametoa maagizo hayo zaidi ya siku nne, wameshakutana hapa? Ni maneno tu, sasa sitaki maneno, nimeshachoka maneno.

“Kanali simamia hii kazi umalize, panga wewe, ulijenga Mererani, ulijenga nyumba 45 kule Dodoma za makao makuu, hautashindwa nyumba hizi, fanya kazi, jenga, siku tutawakabidhi magereza, wakafurahie katika nyumba zilizojengwa na jeshi, inawezekana siku moja wakaanza kujifunza kuona aibu, lakini siku moja wasije wakashangaa namteua mkuu wa magereza akawa mwanajeshi,” alisema.

Pia aliwataka wataalamu wa TBA waliokuwa wakisimamia mradi huo pamoja na askari magereza waondoke na kuwapisha JWTZ.

“Kwa hiyo hapa nisimuone mtu wa TBA, nisimuone mtu wa Magereza kuja kusimamia, muwaache Jeshi la Wananchi wafanye kazi zao, siku watakapokuja kunikabidhi na mimi nitawakabidhi Magereza, kwa hiyo watu wa TBA kuanzia leo (jana) nimewafukuza hapa,” alisema.

Katika hatua nyingine, ameelezea kutoridhishwa na utendaji kazi wa TBA katika mradi huo ulioanza zaidi ya miaka miwili iliyopita kwa kushirikisha Magereza na amewataka wabadilike katika utekelezaji wa majukumu yao.

“Nataka kila mlipo watu wa Magereza mfanye kazi, msimamie watu, kama ni ng’ombe muwafuge vizuri wazalishe vizuri hadi muuze mazao nje, kama ni kilimo mlime kweli kweli, muwe ni jeshi la kuzalisha.

“Hii ni aibu kuleta jeshi jingine la wananchi kuja kuwajengea nyumba nyinyi, wakati nyumba mnakaa nyinyi, mlitakiwa muwe mmeshapanga mkakati kwamba TBA wamesuasua, ngoja tufyatue matofali, tuanze kujenga,” alisema.

Kwa upande wake, Mkuu wa Utawala wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Kanali Charles Mbuge, alisema watakamilisha ujenzi huo ndani ya kipindi cha miezi miwili na nusu kuanzia leo na kazi zitafanywa usiku na mchana.

Pia ameitaka TBA kutoa maelezo ya namna Sh bilioni 10 zilivyotumika na ameonya endapo itabainika matumizi ya fedha hizo hayaendani na kazi zilizofanyika hatua kali zitachukuliwa.

Katika mradi huo, ujenzi wa majengo 12 ya makazi ya Askari Magereza yaliyopangwa kuwa na ghorofa nne kila moja ulioanza Desemba, 2016 umefikia asilimia 45 tu na unaendelea kwa kusuasua.

Pia alifanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa majengo ya makazi wa Magomeni Kota, Dar es Salaam na kuelezea kusikitishwa na hali ya kusuasua kwa ujenzi huo ulioanza Aprili, 2017.

Alishuhudia ujenzi wa majengo yenye ghorofa tatu ukiwa umefikia asilimia 36 na kazi za ujenzi zikiwa zimesimama kwa muda usiojulikana.

Mmoja wa wananchi wanaosubiri kukamilika kwa ujenzi wa nyumba hizo, Mzee Omary Mpimbila, alimueleza Magufuli kuwa wamekuwa wakifanya juhudi za kufuatilia hatma ya majengo hayo kutoka TBA na Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano lakini hadi sasa hawajapatiwa majibu ya sababu za kutelekezwa kwake.

Kutokana na hali hiyo, Magufuli, aliahidi kuchukua hatua za haraka kuhakikisha ujenzi huo unaendelea na wakazi wa Magomeni Kota wanapatiwa makazi kama walivyoahidiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles