Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli anatarajiwa kuongo za mkutano wa 11 wa Baraza Taifa la Biashara (TNBC) Ikulu, Dar es Salaam leo.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Raymond Mbilinyi, ilisema maandalizi ya mkutano huo yamekalimilika.
“Huu ni mkutano muhimu, sekta za umma na binafsi, unatoa fursa kwa pande mbili kujadiliana namna bora ya kujenga mazingira ya biashara na kuvutia uwekezaji zaidi nchini,” ilisema taarifa hiyo.
Ilisema mkutano huo utakuwa wa pili kuuongozwa na Rais Dk. Magufuli kama mwenyekiti wa baraza tangu achaguliwe mwaka 2015.
“Mkutano huu unafanyika wakati kukiwa na mafanikio makubwa ya viwanda zaidi 3,500 vilivyoanzishwa katika kipindi kifupi cha uongozi wa Rais Maguful,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilisema Serikali imesimamia mabadiliko mbalimbali yaliyolenga kuboresha mazingira ya kufanya biashara na kuhamasisha ujenzi wa uchumi wa kati na viwanda.
“TNBC ni jukwaa pekee la majadiliano ambalo hutoa fursa kwa sekta binafsi Tanzania kujadiliana moja kwa moja na serikali kuhusu masuala ya kipaumbele kwa uchumi na ustawi wa maendeleo ya taifa,” alisisitiza.
Mabaraza ya Biashara ya Mikoa (RBCs) na ya wilaya (DBCs) chini ya wenyevikiti wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya, yameweza kuhamasisha na kuibua fursa mbalimbali za uchumi na maendeleo katika maeneo husika.