23.8 C
Dar es Salaam
Sunday, October 13, 2024

Contact us: [email protected]

MKAPA AKOSOA MFUMO WA ELIMU

*Ashangazwa kuwa ya mwisho kwa nchi za EAC

*Ataka mjadala wa kitaifa kujadili hali hiyo

Na RAMADHAN HASSAN,DODOMA

RAIS Mstaafu Benjamini Mkapa amekosoa mfumo wa elimu nchini huku akitaka kuwepo wa mjadala wa wazi wa kitaifa kujadili hali hiyo.

Pamoja na hali hiyo suala la kujadili kwa nini elimu ya Tanzania inazidi kushuka inaweza kupata njia ya kunusuru nchi na mfumo wake wa elimu.

Kauli hiyo aliitoa juzi mjini hapa katika sherehe za kumuaga aliyekuwa Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Profesa Idris Kikula na kumsimika Profesa Egid Mubofu kuwa Makamu Mkuu mpya wa Chuo hicho.

Mkapa ambaye ni Mkuu wa chuo hicho, alisema kwa sasa anaamini kuna tatizo la elimu nchini na amekuwa akiambiwa  kwamba ubora wa elimu upo chini ukilinganisha na nchi za Kenya na Uganda.

“Naamini kabisa, kabisa kuna Crisis (tatizo), ninasoma katika magazeti, nina letewa Presentation (maandiko)  kutoka kwa sekta binafsi ninapata Presentation kutoka vyuo binafsi, napata minong’ono kutoka hata vyuo vya umma kwamba kuna Crisis,” alisema Mkapa

Alisema amekuwa akijua kwamba kuna tatizo katika elimu nchini kupitia barua za wasomaji katika magazeti.

Rais huyo mstaafu alisema kuwa amekuwa Mhariri wa Magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na yale ya Serikali hivyo anajua barua ya msomaji na jinsi hisia za mhusika zinavyokuwa.

Mkuu huyo wa Chuo cha UDOM, alisema amekuwa akisoma katika magazeti hadi mke wake (Anna), amekuwa akimkataza kutosoma sana.

Alisema wakati wote akisoma magazeti na maandiko hayo amekuwa akikutana na malalamiko ya wasomaji kuhusiana na elimu ya Tanzania kuwa haina ubora.

“Mimi nilikuwa Mhariri wa magazeti ya chama na Serikali njia moja ya kujua mwenendo wa mambo na msisimko wa watu ni barua kutoka kwa wasomaji, ninaendelea kusoma magazeti sana, mpaka mke wangu (Anna)  ananilalamikia..

“…lakini nyingi zinalalamika kwamba elimu yetu inamushkeli, kuna wanaolalamika juu ya lugha, kuna wanaolalamika juu ya ratiba zake, kuna wanaolalamika juu ya ushirikiano lakini kuna wanaolalamika juu ya ushirikishwaji wa waliohitimu. Hapa lazima tufanye kazi na wazazi kuamua twende vipi mbele,” alisema Mkapa.

Hata hivyo alihoji orodha ya shule 10 bora za kitaifa ambapo alisema nyingi ni za watu binafsi na si za Serikali.

“Kwanini ukisoma orodha ile ya shule zetu za sekondari ufaulu wao katika 10 za kwanza unaweza kuwa na uhakika nane sio za serikali ni za binafsi ni kwanini… kuna kasoro gani kama serikali ndio mhimili wa elimu,” alisema na kuhoji Mkapa.

Kutokana na hali hiyo Rais huyo Mstaafu, alisema anaona kuna ulazima wa kuwa na mdahalo utakaowashirikisha watu wote wa kujadili ni kwanini elimu ya Tanzania inazidi kushuka.

“Ingekuwa vizuri mngeitisha mdahalo ‘Inclusive’ sio wa wenyewe kwa wenyewe wana taaluma uwe ni pamoja na wale wanaonufaika na elimu uwe wa uwazi wa kuzungumza, mpate kusikia, kusudi tuone kama kuna uwezekano wa kuboresha elimu katika nchi yetu.

“Watanzania wanaoniletea mimi taarifa wanasema katika Afrika Mashariki sisi elimu yetu ni ya chini kuliko Kenya na Uganda mimi sijui kama ni kweli lakini tunapaswa kujiuliza tatizo lipo wapi kuna tatizo gani na tunalitatuaje ili kuwe na elimu bora.

“Najua mtasema nimelalamika, nalalamika lakini nami ni raia bwana… sina gazeti sina NGO’s kama Twaweza, NGO iliyopewa jina langu inashughulika na mambo mengine, nilisikia mmoja anatoa korongo lake nami nikaona nitoe korongo langu mbele na nyinyi wote,” alisema huku akicheka.

Katika hatua nyingine Rais huyo Mstaafu ameiomba serikali kukisaidia chuo hicho fedha ili kizidi kuzalisha wataalamu wengi.

Akimzungumzia Makamu Mkuu wa Chuo aliyemaliza muda wake, Profesa Idris Kikula, Rais Mkapa alisema moja ya sifa kubwa aliyoipenda kutoka kwake ni ukweli na uwazi.

“Sifa zote za chuo hiki zimechangiwa na waliokuwa viongozi wa mwanzo,  wakati chuo kikianzishwa Profesa Shaban Mlacha, Profesa Ludovick Kinabo wakiongozwa na Makamu Mkuu wa Chuo huyu anaemaliza muda wake Profesa Idris Kikula,” alisema

Kutokana na hali huyo Mkapa aliiomba Serikali iwafikirie viongozi hao watatu kwa kuwapa tuzo ya kitaifa ya kutambua kazi njema walioifanya.

Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Chuo aliyemaliza muda wake, Profesa Kikula alisema changamoto aliyokutana nayo katika miaka yake 11 akiwa chuoni hapo ni kauli yake ya kuahidi kwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete, kwamba inyeshe mvua lije jua lazima chuo hicho kisimame.

“Bila hivyo sijui ningetokea mlango gani, ningeonekana ni  tapeli na mlaghai lakini nashukuru mambo yameenda vizuri,” alisema Profesa Kikula.

Hata hivyo alitoa rai kwa wanajumuiya wa UDOM kumpa ushirikiano Makamu Mkuu mpya wa chuo Profesa Mubofu.

Naye Makamu Mkuu mpya wa Chuo hicho, Profesa  Mubofu alisema ametoka kuongoza Shirika la Viwango Tanzania (TBS), hivyo atasimamia viwango ili chuo hicho kizidi kufanya vizuri hasa katika tafiti.

Alisema anatambua madhumuni ya uanzishwaji wa chuo hicho ni kufundisha, kufanya utafiti, pamoja na kutoa ushauri.

“Bado tunachangamoto katika suala la utafiti hivyo kwa pamoja tutahakikisha tunaweka mazingira mazuri kwenye kufanya tafiti mbalimbali  ambazo zitasaidia kukiongeza chuo hadhi,” alisema

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles