29.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JPM, KAGAME WAJA NA RELI MPYA

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli na mwenzake wa Rwanda, Paul Kagame,  wamekubaliana  kujenga reli ya kisasa kutoka Isaka (Tanzania) hadi Kigali yenye urefu wa zaidi ya kilomita 400 kwa lengo la kukuza biashara.

Kutokana na hali hiyo Rais Magufuli amesema mawaziri wa miundombinu wa nchi hizo watakutana wiki ijayo  kupanga   utekelezaji wa ujenzi huo.

Rais Dk. Magufuli aliyasema hayo   Ikulu   Dar es Salaam jana baada ya kukutana na Rais Kagame aliyefanya ziara ya siku moja nchini.

Alisema  kwa sasa wamekwisha kukamilisha kazi ya upembuzi yakinifu na hatua inayoafuta ni kuanza kwa ujenzi wa reli hiyo ya kisasa.

“Upembuzi yakinifu umeshafanyika kinachosubiriwa ni kujenga tu  na tunataka kabla ya Desemba , mwaka huu tuwe tumeweka mawe ya msingi.

“Kazi kwenu mnaohusika mkalisimamie vizuri,”alisema Rais Magufuli.

Alisema reli hiyo  ikikamilika biashara itaongezeka na wafanyabiashara watasafirisha mizigo yao kwa gharama nafuu kwa sababu umbali utakuwa mfupi.

“Mizigo ya DRC pia itapita, tutaweza kuchimba madini ya nickel na kuyasafirisha popote duniani kwa sababu Rulenge kule Ngara tunayo, Rwanda na Burundi pia wanayo,”alisema Rais Magufuli.

Tanzania na Rwanda pia zimekubaliana kuimarisha ushirikiano wa  uchumi na  jamii katika maeneo ya ulinzi na usalama, miundombinu na ushirikiano ndani ya Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kiwango cha biashara kati ya mataifa hayo kimekuwa kikipanda na kushuka ndiyo maana wameweka mikakati ya ujenzi wa reli ya kisasa   kukuza biashara.

Alisema mwaka 2011  biashara baina ya mataifa hayo ilikuwa Sh bilioni 106.54, mwaka 2012 (Sh bilioni 27.34), mwaka 2013 (Sh bilioni 132.21), mwaka 2014 (Sh bilioni 64.45) na mwaka 2015 (Sh bilioni 83.95).

Rais Magufuli  alisema pia mwaka jana mizigo inayosafirishwa kwenda Rwanda kupitia Bandari ya Dar es Salaam iliongezeka na kufikia tani 950,000.

“Sasa unaweza kuona ‘trend’ kwamba imekuwa ikipanda na kushuka na tumekubaliana biashara kati ya nchi hizi mbili ni lazima ianze kupanda.

“Wananchi wa Tanzania na Rwanda nao wakubali  kufanya biashara na Serikali itatengeneza mazingira wezeshi,” alisema.

UENYEKITI WA AU

Kuhusu suala la Uenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Rais Dk. John Magufuli, alisema atamuunga mkono Rais wa Rwanda, Paul Kagame katika nafasi  hiyo kuhakikisha analeta mageuzi makubwa katika bara hilo.

Rais Kagame  anachukua nafasi hiyo kutoka kwa Rais wa Guinea, Alpha Conde, baada ya kuchaguliwa katika mkutano wa kilele wa AU uliofanyika Addis Ababa, Ethiopia mwaka jana.

“Tumeipokea taarifa hii kwa furaha  kwa sababu tunamfahamu Rais Kagame. Ni jirani yetu mwema na Tanzania na Rwanda ni pua na mdomo, nimemhakikishia kumpa ‘support’ kubwa katika nafasi hii,” alisema Rais Magufuli.

Alisema bara la Afrika  linakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwamo migogoro na ukoloni mamboleo lakini ana imani Rais Kagame ataweza kuyaangalia vizuri masuala hayo.

“Rais Kagame anaijua historia ya Rwanda ilikotoka, ameishi ugenini kama mkimbizi, yale mateso aliyoyaishi nina uhakika ataleta mageuzi makubwa Rwanda na Afrika nzima,”alisema.

KAULI YA RAIS KAGAME

Rais Kagame alimpongeza Rais Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya na kufafanua kuwa ataendelea kushirikiana naye   kudumisha uhusiano baina ya mataifa hayo.

“Tunafurahi kwa kazi tunazofanya pamoja, tumekuwa tukishirikiana na mawaziri wetu wamekuwa wakishirikiana kwa njia mbalimbali,”alisema Rais Kagame.

Alisema walikuwa na mazungumzo marefu   baada ya kuwasili nchini na kwa yale waliyokubaliana yataleta manufaa makubwa kwa nchi hizo mbili.

“Ingawa nimekuwa hapa kwa saa chache lakini tumejadili mambo mengi sana, natarajia kwamba tutaendelea kushirikiana   kwa ajili ya wananchi wetu.

“Rais Magufuli ameniahidi kuwa atanisaidia katika kazi za kuongoza AU, ni furaha yangu kufanya kazi pamoja na marais wengine na wengi wako tayari kunipa  ‘support’,” alisema.

Rais Kagame pia alizitaka nchi wanachama wa AU kuchukua hatua kukabiliana na tatizo la ajira   kuepuka vijana kuzikimbia nchi zao na kwenda kutafuta maisha kwingineko.

“Nchi zote za Afrika zifanye kazi kwa pamoja kwa kuhimiza biashara na uwekezaji   vijana wapate ajira. Tuwape elimu, ujuzi na kuwajengea mazingira bora,”alisema Rais Kagame.

Rais Kagame aliondoka jana jioni kurejea Rwanda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles