27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 23, 2024

Contact us: [email protected]

JPM: BOMOENI JENGO TANESCO  UBUNGO, WIZARA YA MAJI

 

Na MWANDISHI WETU  -DAR ES SALAAM

RAIS Dk. John Magufuli, ameagiza kuvunjwa kwa sehemu ya jengo la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na jengo la Wizara ya Maji yaliyopo eneo la hifadhi ya barabara ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja la Ubungo.

Rais Dk. Magufuli, alitoa agizo hilo Dar es Salaam jana baada ya kukagua ujenzi wa daraja la juu Tazara na ujenzi wa daraja la ghorofa tatu la Ubungo kwa nyakati tofauti.

Alimuagiza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi Ndyamukama Julius, kuvunja sehemu ya majengo hayo ili kupisha ujenzi wa miundombinu ya daraja hilo.

Alisema sheria ya hifadhi ya barabara katika eneo hilo ni mita 90 kila upande kutoka katikati ya barabara hivyo haina budi kuzingatiwa hata na Serikali yenyewe.

“Ninataka ikiwezekana leo au kesho jengo la TANESCO liwekwe X, wapeni notisi baadaye mje mkate mnapohitaji, kwa sababu sheria ni msumeno Serikali ikifanya kosa inasulubiwa, raia akijenga kwenye hifadhi ya barabara naye anachukuliwa hatua,” alisema Rais Dk. Magufuli.

Alisema Sheria ya Hifadhi ya Barabara ilikuwapo tangu mwaka 1932 na kwamba ilifanyiwa marekebisho mwaka 1964, 1966 na mwaka 1967.

“Lazima sheria iheshimiwe ili kuharakisha ujenzi wa daraja unafanyika bila vikwazo, sheria ni msumeno haina budi kuzingatiwa hata na Serikali yenyewe,” alisisitiza Rais DK.  Magufuli.

Pia aliiagiza TANROADS kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilomita 16 kutoka eneo linapoishia daraja hilo katika eneo la Ubungo kuelekea Chalinze ili itanuliwe kwa lengo la kurahisisha usafiri katika Jiji la Dar es salaam.

Rais Dk. Magufuli, aliwataka makandarasi wanaojenga madaraja ya Tazara na Ubungo kuharakisha ujenzi kwa kufanya kazi usiku na mchana ili yaweze kumalizika kwa wakati ama kabla ya muda huo kwa lengo la kurahisisha maendeleo ya kibiashara katika jiji.

”Dar es salaam ni jiji la kibiashara hivyo hakuna budi miundombinu yake ya usafiri iweze kurahisisha usafirishaji wa bidhaa mbalimbali kutoka ndani ya jiji na nje ya jiji,” alisema.

Naye Mhandisi wa Masuala ya Usalama wa Ujenzi, Richard Baruani, alisema ujenzi wa daraja la Tazara umefikia asilimia 64 na  linatarajiwa kukamilika Oktoba, mwakani.

Kuhusu daraja la ghorofa tatu la Ubungo, alisema ujenzi wake unatarajiwa kuanza rasmi mwezi ujao.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles