Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli amewataka raia wa Burundi waliopo nchini warudi kwao ili wakafanye kazi ya kujenga nchi yao.
Alitoa agizo hilo jana mbele ya Rais wa Burundi, Pierre Nkurunzinza, aliyekuja nchini kwa mara ya kwanza tangu kushindwa kwa jaribio la kutaka kumpindua akiwa hapa Mei, 2015.
Pia Rais Magufuli ameviagiza vyombo vinavyohusika, kusitisha kutoa uraia kwa wakimbizi kwa kile alichosema, siku hizi wapo wakimbizi wa aina mbalimbali wakiwamo wanaokimbia nchi zao ili wapewa uraia kwenye nchi nyingine.
“Katika dunia ya leo wako watu wanaokimbia maisha na wengine ambao wamezoea kukimbia tu,” alisema Rais Magufuli.
Akizungumza na wananchi wa Ngara mkoani Kagera jana, Rais Magufuli alisema awali Tanzania ilikuwa na makabila 121 lakini hivi sasa yameongezeka ya Wahutu na Watusi waliopewa uraia.
“Badala ya watu kukimbia wanapaswa kujifunza kujenga uchumi wa nchi zao, Waziri wa Mambo ya Ndani sitisha kuanzia leo kutoa uraia kwa wakimbizi wanaokuja ili wasitumie mwanya huo kukimbia nchi zao.
“Warundi mchukue hatua za kuanza kurudi nyumbani kwa hiyari mkajenge nchi yenu, siwafukuzi,” alisema Rais Magufuli.
Aonya mashirika ya wakimbizi
Rais Magufuli pia alionya mashirika yanayosema Burundi kuna matatizo na badala yake wahuburi amani na watu wafanye kazi kwenye nchi zao.
“Ninaomba mashirika ya wakimbizi yaache kuwarubuni kwamba Burundi kuna matatizo…wahubiri amani ya kweli kwamba wanaweza kwenda kushiriki katika maendeleo yao,” alisema.
Rais Magufuli alisema wako baadhi ya watu ambao wamekuwa wakifanya biashara kupitia mgongo wa wakimbizi na wengine kutoka Burundi waliwahi kuahidiwa kupewa Sh 10,000.
Aliwapongeza wakimbizi 150,000 wa Burundi ambao waliamua kurudi kwa hiyari yao.
“Mrudi nyumbani na hizo Sh 10,000 waje kuwapea huko,” alisema Rais Magufuli.
Aonya watendaji wanaotoza kodi wanyonge
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amewatahadharisha watendaji wote kuacha kukusanya kodi za wananchi wanyonge ambazo zimefutwa kisheria.
“Watendaji wanaopenda kukusanya kodi kwa wananchi wanyonge waache kuanzia leo, ukisafirisha mzigo wako kutoka hapa (Ngara) kupeleka Biharamulo, Bukoba au Kigoma unaruhusiwa bila kulipa ushuru wowote mpaka tani moja.
“Tukikuta mtu ametozwa kodi amepakia mzigo wa tani moja, huyo mkurugenzi na DC (Mkuu wa Wilaya), watakipata cha mtemakuni,” alisema.
Alisema pia wameanza kufanya uchambuzi wa pembejeo hewa na kwamba watakaobainika kuhusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Kuhusu kero ya maji wilayani humo, Rais Magufuli aliahidi kutoa Sh milioni 13 kwa ajili ya kununua mota na kwamba chombo hicho kikiungua tena na wao wataungua.
Rais Magufuli alilazimika kuwaita mhandisi wa maji na mkurugenzi wa wilaya hiyo na kuwahoji mbele ya hadhara namna walivyojipanga kutatua kero hiyo.
Mkurugenzi wa wilaya alisema wametenga zaidi ya Sh milioni 200 na kwamba walilenga katika maeneo ya jeshi.
Mhandisi alisema tatizo la maji ni kubwa kwani awali miundombinu ilikuwa ikihudumia watu 400 na kwa sasa inahudumia watu 20,758. Alisema pampu iliyoungua Juni 25 mwaka huu tayari ilifungwa Julai 8 na kuanza kufanya kazi Julai 15.
Pia alisema kisima kimoja kati ya vitatu hakifanyi kazi kutokana na kutokuwa na pampu na kwamba kunahitajika kujengwa tanki lenye uwezo wa kubeba lita 650,000 ambalo litagharimu Sh milioni 500.
“Unajipendekeza kwa wanajeshi kwa sababu wako hapa, wamekuambia hawawezi kuleta maji, hawa wako 250 wananchi zaidi ya 20,000 kwanini hukupeleka kwa wananchi?
“Wanajeshi niachie mimi na CDF (Mkuu wa Majeshi) nitawatafutia maji yao,” alisema Rais Magufuli.
Jaribio la Mei 13 la kumpindua Nkurunziza muda mfupi baada ya kuwasili Dar es Salaam kuhudhuria kikao cha kutafuta suluhu ya mgogoro wa nchi hiyo kuhusu dhamira yake ya kuwania urais kwa kipindi cha tatu, ilishindwa na maofisa wa jeshi walioshiriki jaribio hilo baadhi walikamatwa.
Ofisa mmoja wa jeshi la nchi hiyo, Meja Jenerali Godefroid Niyombare alitangaza kuwa Jeshi la Burundi ‘limemtimua’ Rais Nkurunziza na kwamba limeunda Serikali ya mpito kuiongoza nchi hiyo.
Mara tu baada ya taarifa hizo kuzagaa, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alilaani mapinduzi hayo na kuitaka nchi hiyo kuahirisha uchaguzi hadi amani ya nchi hiyo itakapotengamaa.
Tangazo la mapinduzi
Akizungumza kwenye redio moja binafsi ya Bonesha FM, Jenerali Niyombare alisema: “Rais amekiuka Katiba na amekiuka mazungumzo ya amani ya Arusha.
“Kwa kuwa Rais Nkurunziza anajiamini na amepuuza jumuiya za kimataifa zilizomshauri kuheshimu katiba na mkataba wa amani wa Arusha, tumemuondoa katika wadhifa wake pamoja na serikali yake.
“Ni muhimu kwa ajili ya kulinda heshima ya nchi… Rais Pierre Nkurunziza ameondolewa madarakani,” alisema Jenerali Niyombare ambaye alitimuliwa kazi na rais huyo mapema Februari mwaka huu akiwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Usalama nchini humo.