32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATETA NA AGA KHAN

Na MWANDISHI WETU-DAR ES SALAAM


RAIS John Magufuli amemwomba Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia, Mtukufu Karim Al-Hussaini Aga Khan, kupunguza gharama za huduma zake kwa wananchi  waweze kumudu, kwa vile  taasisi hiyo imekuwa ikipata msamaha wa kodi kutoka serikalini.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo Ikulu   Dar es Salaam jana, alipofanya mazungumzo na Mtukufu Karim Al-Hussaini Aga Khan.

Alimshukuru  kiongozi huyo kwa taasisi zae kutoa huduma za jamii  nchini.

“Lakini nitoe wito kwa taasisi zako kupunguza gharama za huduma zake kwa wananchi   waweze kumudu hasa ikizingatiwa kuwa zimekuwa zikipata msamaha wa kodi kutoka serikalini,”alisema Rais Magufuli.

Alisema Serikali yake ipo tayari kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na Aga Khan.

Alimwomba kiongozi huyo kuendelea kupanua wigo wa huduma za taasisi zake ikiwa ni pamoja na kuwekeza Dodoma yaliko makao makuu.

Aga Khan Foundation ina taasisi mbalimbali   nchini ikiwamo hospitali, shule, vyuo na kampuni nyingine.

Naye kiongozi huyo  alisema jumuiya hiyo imedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupanua Hospitali ya Aga Khan   Dar es Salaam na kujenga chuo kikuu kikubwa Afrika Mashariki mkoani Arusha.

“Upanuzi wa hospitali ya Aga Khan utahusisha kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi kufikia vitanda 172, utaimarisha matibabu ya moyo na kansa na utaongeza ufundishaji wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.

“Jumuiya imedhamiria kujenga chuo kikuu kikubwa ambacho kitafundisha viongozi si tu wa Tanzania na Afrika Mashariki, bali pia Afrika nzima  waweze kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ya Afrika,”alisema.

Akizungumzia  u vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Aga Khan, alisema yeye haamini kuwa ni kipaumbele kwa vyombo vya habari   kujikita katika masuala ya siasa bali anaamini vyombo hivyo vina wajibu mpana katika masuala ya maendeleo.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amekutana na kuwa na mazungumzo na ujumbe wa Maseneta wa Baraza la Seneti la Marekani ambao ni wajumbe wa kamati ya mazingira inayoshughulikia hifadhi ya taifa, wanyamapori na misitu ya Marekani ambao wamekuwapo   nchini kwa siku tatu   kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro.

Maseneta hao ni  James Inhofe, Mike Enzi, David Perdue, Luther Strange, Tim Scott na John Thune.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles