31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

BUTIKU: NYERERE HAKUWA MJINGA KUFA MASIKINI

 

Na EVANS MAGEGE


MWENYEKITI wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku amesema,  Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hakuwa mjinga kufa masikini.

Butiku alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana wakati akichangia maada kwenye kongamano la Kibweta cha Mwalimu Nyerere kilichoandaliwa na Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere   Kigamboni.

Maada kuu ya kongamano hilo   ilisema, “Mtazamo wa Mwalimu Nyerere katika Uchumi wa Viwanda na Maendeleo ya Jamii”.

Akichangia, Butiku alisema Nyerere alikuwa muumini wa usawa hivyo alijituma kuweka misingi ya maendeleo kwa utaifa wa Watanzania wote.

Alisema  kama Baba wa Taifa angekuwa na moyo wa ubinafsi na mroho wa mali, angeanza kwa kujilimbikizia mali kabla ya maendeleo ya nchi na asingekufa masikini.

Alisema Nyerere aliona mbali katika kuleta maendeleo yenye usawa kwa wananchi kwa kuanzisha viwanda.

Butiku alisema kwa sasa yapo malengo ya kuanzisha  viwanda kama alivyofanya Baba wa Taifa.

Alisema wakati malengo hayo yakiwapo, Watanzania wanatakiwa kujua kwamba viwanda siyo maendeleo bali ni matokeo ya watu   walioendelea.

“Mwalimu alikuwa ni mtu anaona huko, anaona watu wake, anaona watu anaowaongoza, ametokea miongoni mwao, anajua mahitaji yao,  kwa hiyo alikua anajua afanye nini   watu wote wapate.

“Viwanda vyetu vipo? Na kama havipo kwa nini? Tukubali makosa, kung’ang’ania kitu ambacho hakijafika halafu kikakushinda… Kwa hiyo ukipewa usisahau kuwa si vyako kwa hiyo usiibe,” alisema Butiku.

Alisema Hayati Baba wa Taifa alipokuwa anaiweka nchi iwe ya Watanzania wote alikuwa na maana ya wananchi wote kushiriki kwa usawa katika kujenga maendeleo yenye umoja na usawa.

Alisema bila amani   viwanda  haviwezi kuwapo badala yake ni kushindania  na kugombania vyeo.

“Nawauliza mnaendelea kushughulika na viwanda au mnaendelea kushughulika na vyeo vyenu? Mnaendelea kushughulika na viwanda, elimu na afya au mnaendelea kushughulika na kula?.

“Haya ni maswali magumu. Nyerere huyu tunayemzungumza leo alikufa masikini, kwani alikuwa mpumbavu?  Alikuwa mjinga au alikuwa hana elimu?  Jibu utapata, aliwapendeni ninyi,” alisema Butiku.

Kwa muktadha huo, alisema Nyerere aligombania amani na utulivu ili   wananchi wote wapate chao.

“Kuwa na nchi mnajenga Chuo Kikuu Dodoma halafu mnapeleka watoto wajinga 7000,  Je hayo ni maendeleo?” aliuliza.

Alisema kama nchi haijaendelea kutakuwa na msululu wa viwanda vya watu wageni na Watanzania watakuwa makuwadi.

Alisema viwanda ambavyo Hayati Baba wa Taifa alivijenga vilikuwa ni viwanda vidogo  ambavyo vinaendana na kilimo.

“Kwa sasa  tumetilia mkazo sana viwanda vinavyotumia fedha nyingi kuviendesha, hayo mabilioni ya kuviendesha mnayo?

“Lakini nimeona sera ya serikali… tuipongeze kwa sababu imeanza kutufufulia viwanda katika sekta ya kilimo,” alisema.

Alisema viwanda vya kilimo vitawapa Watanzania fedha za mifukoni lakini viwanda vya mafuta na gesi ndivyo vitampa fedha Rais Magufuli.

Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo Cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Profesa Mark Mwandosya, alisema Watanzania wanatakiwa kujiuliza kwamba unapozungumzia ujenzi wa viwanda, vinajengwa kwa nini, sehemu gani vinajengwa na kwa faida ya nani?

Mwanasiasa mwingine mkongwe, Ibrahim Kaduma ambaye alifungua kongamano hilo, alisema unafiki umelifikisha taifa mahali pabaya.

Alisema Hayati Baba wa Taifa alijenga misingi ya taifa lakini viongozi waliofuata wamesuasua kuujenga ukuta.

Alisema wakati Hayati Baba wa Taifa na wenzake wanatafuta uhuru wa nchi hii, hawakuthamini fedha kuupata kwa sababu fikra yao ilikuwa ni ukombozi  wa nchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles