23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

JPM ATANGAZA KIAMA KWA MAOFISA UHAMIAJI MIKOA YAO ITAKAYOPITISHA WAHAMIAJI HARAMU

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM


RAIS Dk. John Magufuli ameagiza makamanda wa uhamiaji ambao mikoa yao itabainika kupitisha wahamiaji haramu washushwe vyeo mara moja.

Amesema juzi waliingia wahamiaji zaidi ya 1,500 kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), lakini walioripoti kwenye kambi ya wakimbizi ni chini ya 1,000 hatua inayoashiria kuwa wengine wameingia mtaani.

Dk. Magufuli alitoa agizo hilo jijini Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Uhamiaji Mtandao (e-Immigration).

Alisema, idara hiyo ni muhimu hasa katika suala la ulinzi na usalama lakini katika miaka ya hivi karibuni ililegalega na kusababisha nchi kugeuka na kuwa uchochoro wa wahamiaji haramu.

“Nafurahi sana ninapoona maofisa wa uhamiaji wakishughulika, sitaki kuwataja lakini nimekuwa nikiona mara Mbeya unakuta watu wameshikwa kutoka nchi jirani wanakwenda kukamatiwa Mbeya au Iringa.

“Wanapoulizwa unakuta wamepita labda kuanzia Kilimanjaro, ni lazima mkurugenzi mkuu ujiulize huko Kilimanjaro, Singida, Manyara na maeneo mengine walipitaje?

“Ifike mahali anaposhikwa mhamiaji haramu na anapoulizwa taarifa zake kwenye mikoa aliyopitia, mchukue hatua kwa wakuu wa uhamiaji katika mikoa husika, uwapunguze vyeo…hata nyota zipungue ili waanze kujifunza majukumu yao ya kufanya kazi.

“Kama amepita Chato, Mwanza halafu akakamatwa Singida je, kule Chato, Bukoba na kwingineko hakuna ma– immigration officer? Maana yake hawakutimiza wajibu wao,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alisema pia awali hati za kusafiria zilikuwa zikigawiwa kiholela na kuwapa fursa wahalifu kuzitumia vibaya wakiwamo wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

“Wengine wamepewa hati za Tanzania huku wakimiliki hati za nchi nyingine kinyume kabisa na sheria za nchi, vibali vya ukaazi na uraia wa nchi yetu vilitolewa bila kuzingatia utaratibu, raia wengi wa kigeni walipata uraia bila kuwa na sifa stahiki na wengine walipata vyeo vikubwa serikalini,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kutokana na mapungufu hayo ndiyo maana alimteua Dk. Anna Makakala kuiongoza idara hiyo akiamini kuwa wanawake huwa ni waaminifu.

“Nilimteua mwanamama Dk. Makakala kuwa kamishna mkuu, wanamama wengi ni waaminifu, nina uhakika atazingatia uaminifu wake katika kusimamia kazi hii.

“Ameanza vizuri na nafahamu bado kuna mapungufu lakini kutokana na jitihada alizoanza kuzichukua yataweza kupungua kabisa. Namuhimiza aendelee kuyashughulikia bila woga wowote,” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli pia aliahidi kutoa Sh bilioni 10 kwa ajili ya kujenga ofisi ya makao makuu ya idara hiyo Mjini Dodoma.

“Ninajua kuna baadhi ya wafanyakazi watalaumu kuhama hapa kwa sababu ya mabanda wanayotumia mbinu zao za kutengeneza ‘michuzi’ lakini ni lazima tuwe na jengo zuri.

“Dk. Makakala katafute eneo nitawapa Sh bilioni 10 wakati wowote mtakapozihitaji muanze kujenga makao makuu, ninazitoa hizi kwa shukrani kutokana na kazi kubwa unayoifanya wewe na watendaji wako.

“Endeleeni kubadilisha jina la Uhamiaji, kushughulikia wahamiaji haramu bila kumwogopa mtu yeyote,” alisema.

Kuhusu hati za kielektroniki alisema zitasaidia kupunguza au kuondoa uwezekano wa kugushiwa tofauti na hati za zamani ambazo hazikuwa na usalama wa kutosha na kusababisha kugushiwa.

MABILIONI YAOKOLEWA

Awali mradi huo  wa e-Immigration ulikadiriwa kugharimu Sh bilioni 400 hatua iliyosababisha kushindwa kutekelezwa baada ya gharama kuonekana kuwa kubwa.

Akizungumza katika sherehe hizo Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, alisema  mchakato wa mradi huo ulianza mwaka 2013 ambapo Kampuni ya DTB iliyo chini ya Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), ilipewa jukumu la kufanya upembuzi yakinifu.

Kampuni hiyo ilieleza kuwa gharama ya mradi huo ni Dola za Marekani milioni 226 (zaidi ya Sh bilioni 400).

“Hata hivyo utekelezaji wa mradi huu ulishindikana kwa wakati huo baada ya watengenezaji waliojitokeza kuonyesha gharama kubwa,” alisema Dk. Makakala.

Alisema mchakato wa mradi huo ulianza tena Juni 2017 baada ya timu ya wataalamu kutembelea nchi mbalimbali ili kujifunza na kuangalia gharama namna nchi hizo zinavyotekeleza mfumo wa uhamiaji mtandao.

Baada ya uchambuzi wa kina Kampuni ya HID Global ilikidhi vigezo kutokana na kuwa na uzoefu wa muda mrefu katika utoaji wa pasipoti za kielektroniki kwa gharama ya Sh bilioni 127.

Rais Magufuli alisema anaufahamu vizuri mradi huo na kwamba amekuwa akiufuatilia kwa karibu na hata alipomteua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Mwigulu Nchemba, alimwagiza aufuatilie.

“Haikuwa jambo rahisi kufikia hatua hii, nilipomteua Waziri wa Mambo ya Ndani nilimwambia kuna mchezo mchafu unachezwa pale, hii ndiyo bongo land

“Walipanga kutupiga kwenye fedha za Watanzania, msishangae siku za nyuma palikuwa na watu wakizunguka sana wakipiga vita mchakato huu kwa sababu walijua wanataka kutengeneza bilioni 400.

“Walijua Tanzania bado ni eneo la kuchuma, tumewazuia na waendelee kuzunguka sana tulishirikisha vyombo vya dola Uhamiaji, Polisi, Usalama wa Taifa, Serikali Mtandao na wengine wakafanya uchambuzi wa ndani wa kutosha,” alisema.

MFUMO WA UHAMIAJI

Kuhusu mfumo wa uhamiaji mtandao, Dk. Anna Makakala, alisema ni mwunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji.

Alisema kupitia mfumo huo idara ya uhamiaji inatarajia kutoa pasipoti za kielektronikia (e-Passport), viza za kielektronikia (e-Visa), vibali vya ukaazi vya kielektronikia (e-Permit) na udhibiti wa mipaka wa kielektronikia (e-Border Management) kwa awamu nne hadi ifikapo mwisho wa mwaka huu 2018, pamoja na kutoa pasipoti ya kielektronikia ya Afrika Mashariki ya Tanzania.

Alisema lengo la mradi huo ni kuimarisha ulinzi na usalama wa mipaka ya nchi, kudhibiti ukusanyaji wa maduhuli ya serikali pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma za kiuhamiaji kwa raia wa Tanzania na wageni wanaoingia na kuishi nchini.

Alisema mradi huo unatekelezwa kwa awamu nne na wanatarajia kumaliza awamu zote kabla ya mwisho wa mwaka huu.

“Hati hizi mpya ni imara, zina kurasa nyingi zaidi ukilinganisha na za zamani hivyo, kumwongezea mwananchi nafasi ya matumizi zaidi ndani ya miaka 10,” alisema Dk. Makalaka.

Hati hizo mpya zitatolewa kwa gharama ya Sh 150,000 na muhusika atatakiwa kuwa na kitambulisho cha taifa.

Alisema hati za kusafiria za kawaida zilizopo sasa zitaendelea kutumika hadi Januari 2020 na hati za Afrika Mashariki zilizokuwa zikitumika awali hazitatolewa tena.

Naye Balozi wa Ireland, Paul Sherlock, aliipongeza Serikali kwa kufanikisha mradi huo na kueleza kuwa mfumo huu wa uhamiaji mtandao ni alama muhimu ya Taifa.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Seif Ali Iddi,  Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Dk. Ali Hassan Mwinyi na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles