24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

SHULE SITA ZA SERIKALI ZAPENYA 100 BORA KITAIFA

Na Waandishi Wetu – DAR ES SALAAM


WAKATI matokeo ya mtihani wa taifa wa kidato cha nne uliofanyika Oktoba na Novemba 2017 yakitangazwa juzi, shule sita pekee za Serikali zimefanikiwa kuingia katika orodha ya shule 100 bora.

Katika mtihani kama huo wa mwaka 2016, shule za Serikali zilizoingia kwenye kundi hilo la 100 bora zilikuwa saba.

Hali hiyo inaonyesha kuwa shule za Serikali bado ziko kwenye hali mbaya kiushindani, licha ya mwaka huu Ilboru ya Arusha kufanikiwa kuingiza watahiniwa wawili katika orodha ya wanafunzi 10 bora kitaifa.

Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyotangazwa na Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA), Dk. Charles Msonde, shule ya kwanza ya Serikali kwenye orodha ya shule 100 bora ni Mzumbe ya Morogoro iliyoshika nafasi ya 21, ikifuatiwa na Kibaha ya Pwani (31), Ilboru (39), Kilakala ya Morogoro (40), Tabora Boys’ ya Tabora (60) na Tabora Girls’ pia ya Tabora (66).

Katika mtihani wa mwaka 2016,  shule ya kwanza ya Serikali ilikuwa ni Kibaha iliyoshika nafasi ya 16, ikifuatiwa na Mzumbe (27), Kilakala (28), Shule ya Wasichana Kibosho ya Kilimanjaro (36), Tabora Boys’ (41) na Ilboru (42).

 

WADAU WACHAMBUA MATOKEO

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Euginea Kafanabo, akichambua matokeo hayo, alisema kuibuka tena kwa shule za umma kunaweza kusababishwa na kelele ambazo zimekuwa zikipigwa na wadau wa elimu, hivyo wenye shule hizo kuamua kuongeza nguvu kuziwezesha kufanya vizuri.

Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Mameneja na Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), William Magero, alisema: “Sisi tunapowazidi ni kuchuja wanafunzi ili kuhakikisha wanapatikana wanafunzi bora na wenye uwezo pamoja na kuwa na miundombinu mizuri.”

Kuhusu ongezeko la wanafunzi wanaodanganya kwenye mitihani kutoka 86 mwaka uliopita hadi 262 mwaka huu, Magero alisema udanganyifu unasababishwa na wanafunzi kukosa maandalizi ya kutosha kukabiliana na mitihani.

“Ukiangalia waliodanganya wengi ni watahiniwa binafsi na wachache watahiniwa wa shule, naamini wanafanya hivyo kwa sababu hawana maandalizi mazuri, kama wangekuwa wamejiandaa wasingekuwa na hofu ya mtihani, kwahiyo Serikali ijitahidi kuweka mazingira mazuri ya kuwaandaa wanafunzi katika shule zake,” alisema Magero.

 

KILIMANJARO KINARA

Matokeo hayo pia yanaonyesha kuwa Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa wa kwanza kwa shule zilizofanya vizuri kutoka nafasi ya tano mwaka 2016, huku Kaskazini Unguja ikivuta mkia kwa kushika nafasi ya 31 kutoka ya 29 mwaka 2016.

Kwa mujibu wa taarifa ya NECTA inayoainisha mpangilio wa mikoa kwa ubora wa ufaulu, Pwani imekuwa ya pili kutoka nafasi ya saba mwaka 2016, Tabora ya tatu kutoka kumi, Shinyanga ya nne kutoka tisa na Mwanza nafasi ya tano kutoka ya sita.

Mkoa wa Mbeya umekuwa wa sita kutoka 13 mwaka 2016, Arusha ya saba kutoka 11, Geita ya nane kutoka 17, Kagera ya tisa kutoka tatu, Kigoma ya kumi kutoka ya nne.

Mikoa mingine na nafasi zake ni  Simiyu ya 11 kutoka 14, Manyara 12 kutoka 16, Rukwa 13 kutoka 12, Morogoro ya 14 kutoka 21, Njombe ya 15 kutoka namba moja mwaka 2016 na Dar es Salaam imekuwa ya 16 kutoka 18.

Taarifa hiyo inabainisha kuwa Iringa imekuwa ya 17 kutoka nafasi ya pili, Singida ya 18 kutoka 23, Dodoma ya 19 kutoka 24, Mtwara ya 20 kutoka 25, Songea ya 21 kutoka 20, Katavi ya 22 kutoka 19, Mara ya 23 kutoka 22, Tanga 24 kutoka 27 na Ruvuma ya 25 kutoka nafasi ya nane.

Nafasi ya 26 inashikiliwa na Mjini Magharibi kutoka 15 mwaka uliopita, Lindi 27 kutoka 31, Kusini Pemba 28 kutoka 26, Kaskazini Pemba 29 kutoka 28, Kusini Unguja 30 ambayo ilishika pia mwaka 2016 na Kaskazini Unguja inashika mkia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles