27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JPM ATAJA KASHFA TANO ANAZOTAKA IZISHUGHULIKIE

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kutokuwa na kigugumizi cha kuchukua hatua wanapokuwa na ushahidi dhidi ya watu wanaojihusisha na vitendo vya rushwa.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa, ilisema Rais Magufuli alitoa kauli hiyo  jana alipotembelea na kuzungumza na wafanyakazi wa  taasisi hiyo katika ofisi za makao makuu, Dar es Salaam.

“Kuna mambo mengi ya hovyo yanafanyika, tumehakiki pembejeo za ruzuku na kubaini madai ya Sh bilioni 48 ni hewa, wafanyakazi hewa zaidi ya 19,500, masikini hewa 56,000 zilizopaswa kupata fedha TASAF, wanafunzi hewa 5,850 waliotakiwa kupata mkopo, kuna vichwa vya treni 11 vimeletwa bila kuwapo mkataba na mengine mengi, haya yote yanafanyika kwa rushwa, nataka kuwaona mnachukua hatua stahiki,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ana imani na taasisi hiyo na kuwataka wafanyakazi kufanya kazi kwa kuzingatia weledi, uzalendo na uadilifu mkubwa na kwamba Serikali itafanyia kazi changamoto zinazowakabili.

Katika mkutano huo, Rais Magufuli, alipokea masuala mbalimbali kutoka kwa wafanyakazi na kuwaahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha masilahi yao na mazingira ya kazi.

Mkutano huo, ulihudhuriwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Anjellah Kairuki, Katibu Mkuu Dk. Laurian Ndumbaro na Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Valentino Mlowola.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi na wataalamu wanaosimamia utekelezaji wa miradi mikubwa, ikiwamo ujenzi wa mradi wa umeme katika maporomoko ya Mto Rufiji (Stieglers’ Gorge Hydropower Project), ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa barabara mbalimbali, Ikulu Dar es Salaam.

Katika Mkutano huo, Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dk. Medard Kalemani alitoa taarifa ya maandalizi ya awali ya kuanza kwa ujenzi wa mradi wa umeme wa Stiegler’ Gorge na kwamba zabuni ya kuanza itatangazwa kesho.

Rais Magufuli, alisema fedha za kuanza ujenzi wa mradi huo mkubwa utakaozalisha megawati 2,100 zitakazoingizwa katika gridi ya taifa zipo.

Wiki iliyopita, Rais Magufuli, alimteua Brigedia Jenerali John Mbungo kuwa Naibu Mkurugenzi Takukuru.

Uteuzi wa Brigedia Jenerali Mbungo, ulianza Agosti 21, mwaka huu, akitokea kwenye nafasi ya Mkuu wa Tawi la Sheria la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na anajaza nafasi iliyokuwa wazi tangu Desemba 16, 2015.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles