*WATOFAUTIANA JUU YA MSIMAMO ULIOTOLEWA NA TLS
*LISSU AMSHANGAA JAJI MKUU, ATOA NENO KWA WATAKAOENDA MAHAKAMANI
Na Waandishi Wetu – Dar es Salaam
MGOMO wa siku mbili uliotangzwa na Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS) sasa ni pasua kichwa.
Ndivyo unavyoweza kusema baada ya baadhi ya mawakili kukubali kugoma, wengine wakisema wataendelea na kazi, huku Kaimu Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma, akisema atawachukulia hatua watakaogoma.
Kwa upande mwingine, Rais wa TLS, Tundu Lissu, amemjia juu Prof. Juma na kusema mawakili ambao watasaliti chama, nao watatengwa wakipata matatizo.
Juzi Baraza la Uongozi la TLS, lilitangaza mgomo wa siku mbili kuanzia leo, lengo likiwa ni kuwaunga mkono mawakili wa Kampuni ya IMMMA, ambao ofisi zao zilizopo Upanga, Dar es Salaam usiku wa kumkia Jumamosi zililipuliwa na kitu kinachodhaniwa kuwa bomu.
Jana, gazeti hili lilifanya mazungumzo na mawawiki mbalimbali kutoka mikoa tofauti nchini, ambao baadhi yao walisema watafuata kile kilichosemwa na chama chao, huku wengine wakisema wataendelea na kazi ya kuwatetea wateja wao.
LISSU
Baada ya kuzungumza na mawakili hao, gazeti hili pia lilimtafuta Lissu aliyesoma maazimio ya Baraza Kuu, ambaye alisema hakuna kampuni iliyolazimishwa kugoma, lakini wale watakaofuata azimio la chama watashirikiana nao.
Alisema wanajua wapo baadhi ya mawakili watakaidi agizo hilo na wakifanya hivyo, TLS haitawasaidia pindi watakapopata matatizo.
Lissu alisema lengo la mgomo ni kuonyesha kwamba kilichotokea kwa Kampuni ya IMMMA si kitendo cha kiungwana, hivyo wanaungana nao ili kuonyesha mshikamano.
“Kama kuna mawakili wanaona kuwa kitendo kilichotokea kwenye Kampuni ya IMMMA ni sawa sawa, hatuwezi kuwafanya chochote, lakini wakumbuke kuwa wakipata matatizo hatutawasaidia,” alisema.
AMJIA JUU KAIMU JAJI MKUU
Profesa Juma juzi alipozungumza na gazeti linalomilikiwa na Serikali, alisema endapo wateja watalalamika kwamba mawakili wao hawajafika mahakamani watachukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kupelekwa kwenye Kamati ya Maadili ya Mawakili.
Akizungumzia kauli hiyo, Lissu alimshangaa akisema tangu tukio hilo litokee, hajasema chochote cha kulaani badala yake anawatisha mawakili.
Alisema kuvamiwa kwa Kampuni ya IMMMA ni sawa na ugaidi, hivyo kila mwananchi mwenye mapenzi mema anapaswa kukemea na kulaani.
“Nimeshangazwa sana na kitendo cha Jaji Mkuu cha kushindwa kulaani, kukemea, kuwapa pole au kuzungumza lolote kuhusu suala hili wakati mawakili waliopata matatizo anafanya kazi nao,” alisema Lissu.
NI BOMU LA KUTENGENEZA KIENYEJI
Wakati huohuo, Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limesema uchunguzi wa awali uliofanywa katika ofisi za Kampuni ya IMMMA, umebaini mlipuko ulitokana na bomu lililotengenezwa kienyeji.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Kamishna Mwandamizi wa Polisi (SACP), Benedict Kitalika, alisema katika tukio hilo watu wasiojulikana walifika katika ofisi hizo wakiwa na magari mawili wakijifanya ni askari na kuwarubuni kisha kuwachukua walinzi wa jengo zilipo ofisi hizo, ambao baadae walikutwa maeneo ya Kawe wilayani Kinondoni wakiwa hawajitambui.
”Baada ya kuondoka, kundi lililobaki liliingia ndani ya ofisi hizo na kuweka milipuko iliyotengenezwa, ambayo baada ya watu hao kuondoka ililipuka na kusababisha uharibifu wa mali na jengo la ofisi hiyo pamoja na majengo ya jirani,” alisema SACP Kitalika.
Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kuwabaini waliotekeleza tukio hilo na dhamira yao ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya sheria.
Aliwataka waathirika wa tukio hilo na wananchi kwa ujumla kuwa watulivu wakati vyombo vya dola vikiendelea na upelelezi.
”Ifahamike kuwa wajibu wa Jeshi la Polisi ni kulinda maisha ya watu na mali zao, hivyo kamwe haliwezi kutumika kuhujumu maisha ya watu na mali za wananchi. Tunatoa rai kwa wananchi wenye taarifa zinazoweza kusaidia katika upelelezi waziwasilishe kwa Jeshi la Polisi ili zifanyiwe kazi,” alisema Kitalika.
WALICHOSEMA MAWAKILI DAR
Wakizungumza Dar es Salaam kwa masharti ya kutotajwa majina yao kwa nyakati tofauti, mawakili wa kujitegemea walisema ukiona mwenzio ananyolewa wewe tia maji.
“Leo wameanza kurusha bomu kwa IMMMA, siwezi kujua kwangu itakuwa lini, naunga mkono na nitagoma, kesho sitafika mahakamani.
“Kuna kauli zimeshawahi kutolewa kwamba anayemtetea mwizi anashughulikiwa, mimi kuna kesi natetea watuhumiwa fulani, siwezi kujua huenda zamu yangu inakuja,” alisema.
Mawakili wa Jamhuri, baadhi walidai hali hiyo si ya kuikalia kimya, lazima ikemewe kwani inahatarisha usalama wa mawakili wote.
Alidai kila upande ukiamua kufanya maamuzi kama hayo ya kulipua ofisi hakuna atakayenusurika.
“Ukiliangalia suala hili kwa macho mawili, huwezi kukaa kimya bila kulikemea, si jambo lenye afya kwa fani ya sheria, linatishia utendaji kazi wa mawakili, likiachwa lazima litahamia na kwa wengine,” alisema.
ARUSHA
Baadhi ya mawakili wa mkoani Arusha, walisema wanaunga mkono tamko la TLS, na kuwa hawataenda mahakamani, huku wegine wakisema wataomba tume huru ya vyombo vya kimataifa ichunguze tukio hilo.
Wakili Mwandamizi Colman Ngalo, alisema agizo la TLS lina lengo la kuonyesha mshikamano miongoni mwa wanachama, lakini yeye binafsi haoni kama litasaidia kubadilisha chochote katika uchunguzi unaoendelea.
“Kitendo cha kuvamia ofisi za mawakili na kuilipua hakikubaliki ndiyo maana Lissu ametoa tamko lile kwa niaba yetu, isipokuwa mimi nashauri yeyote mwenye taarifa itakayosaidia vyombo vya dola kubaini ukweli apeleke. Haya mengine hayatasaidia sana,” alisema.
Kwa upande wake, Wakili Regold Nkya, alisema hawatakwenda mahakamani kwa sababu wana haki ya kulinda uhuru wa mawakili na uhuru wa sheria.
Alisema wataomba kuundwa tume huru ya vyombo vya kimataifa ili kuchunguza tukio hilo ikiwamo Chama cha Mawakili Afrika, Chama cha Wanasheria wa Afrika Mashariki (EALS) na Chama cha Wanasheria kutoka nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika (SADC).
“Hatutakwenda mahakamani kwa sababu tuna haki za kulinda uhuru wa mawakili na sheria, kama wakili atapigwa bomu mwananchi wa kawaida atafanywa kitu kibaya zaidi.
“Tuna wajibu wa kutaka tume huru ya vyombo vya kimataifa iundwe kwani tunakuwa hatuna imani na vyombo vyetu vya ndani,” alisema.
Wakili Sheck Mfinanga, alisema hawataenda mahakamani kwa siku hizo mbili na kuwa watatoa notisi kwa mahakama.
“Hatutaingia mahakamani na tutatoa notisi kwa mahakama kuwa tuna mgomo, sisi ni maofisa wa mahakama na tuna wajibu wa kwanza kwa mahakama halafu wajibu wa pili kwa mteja,” alisema.
Edmund Ngemela, alisema yeye hakubaliani na agizo hilo, hivyo hatagoma kama agizo la Rais wa TLS linavyotaka na kuwa ataendelea na majukumu yake kama kawaida.
“Nani wa kugoma bwana, hamna mtu atakayegoma na ungekuwepo kwenye ‘group la whatsapp’ la mawakili ungeona jinsi watu wanavyoponda tamko hilo, ni tamko la kipuuzi, mimi nitakwenda mahakamani, nina mkataba na wateja wangu,” alisema Ngemela.
Alipoulizwa msimamo wa wanachama, Mwenyekiti wa TLS Kanda ya Arusha, Elibariki Maeda, alisema bado hawajakubaliana iwapo watatii agizo hilo au la.
IRINGA
Mwenyekiti TLS Kanda ya Iringa, Rwezaula Kaijage alisema: “Watu wanapotosha juu ya jambo hili, wapo ambao wanatamani kuona mgomo wetu umekwama kwa kuwa Lisu katangaza.
“Lazima mawakili wenzangu Mkoa wa Iringa kutambua kuwa hatufanyi mgomo kwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Lissu kasema, tunafanya mgomo kuonyesha umoja wetu kama wanachama wa TLS na waliopatwa na mkasa wa ofisi zao kuungua moto ni wanachama wenzetu.
“Lissu ametoa tamko ambalo limepitishwa na baraza letu, kimsingi tamko hilo hata bila yeye kutangaza lingetekelezwa, tuache kuchukulia kila jambo kwa misingi ya kisiasa, tuangalie kwa mapana yake.
“Sisi hatugomi kama migomo ya wanafunzi, sisi ni mawakili wasomi, mgomo wetu sio wa kusukumana ama kuzuia wengine kutimiza wajibu wao… Ofisi zetu zitafunguliwa kama kawaida na wale wenye kesi za kufungua mahakamani wataendelea kama kawaida na hata hapa katika viwanja vya mahakama mawakili watakuwepo kwa shughuli zao ila sio kwamba watakuwepo kwa ajili ya kuonyesha mgomo huo,” alisema.
MOROGORO
Wakizungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti kwa sharti la kutotajwa majina, baadhi ya mawakili wamesema wana mikataba na wateja wao na pia taarifa za mgumo bado hawajazipata rasmi.
Hivyo walisema hadi sasa kuna sintofahamu kuhusu tukio hilo.
“Sasa mgomo huo bado hatujui tunashinikiza nini maana polisi bado hawajasema wahusika,” alisema mmoja wa mawakili.
Mawakili hao wameshauri kusubiri kwanza kusikia taarifa ya uchunguzi wa polisi, kwani kufanya mgomo ni kuonesha tayari wameshamjua mtuhumiwa wa tukio.
Hata hivyo, mawakili hao wamekumbushana suala la ofisi zao kuwa na bima kubwa ili kuepukana na madhara ya namna hiyo.
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA YAALANI
NayoTume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), imetoa tamko la kulaani kitendo cha kupigwa bomu ofisi hizo.
Taarifa ya mwenyekiti wa tume hiyo, Bahame Nyanduga, iliyotolewa jana, ilisema imesikitishwa na kitendo hicho ambacho kinaashiria uhalifu wenye nia ya kutisha wanasheria wasitekeleze majukumu yao ya kisheria ya kutetea wateja wao.
“Tume inasisitiza kuwa dhana ya utawala bora inategemea utawala wa sheria, ambao utaathirika iwapo wanasheria watatishwa na matukio kama ya kupigwa mabomu au vitendo vinginevyo vitakavyowanyima uhuru wa kufanya kazi zao.
“Tume inalitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha linakamilisha upelelezi wa tukio hilo na kuwapeleka wahusika katika vyombo vya sheria,” ilisema.
Hata hivyo, iliitaka TLS kusitisha tangazo la mgomo kwani hautakuwa na maana kwa vile vyombo vya usalama vimeishaanza kufanya uchunguzi.
“Pia ni vyema TLS ikasitisha mgomo huo kwani utawaathiri zaidi wateja wao ambao hawahusiki na tukio la kupiga bomu,” ilisema.
Du , kila kitu kinakuwa uwanja wa mapambano ya kisiasa. Masikini Tanzania. Lakini Mungu atatuvusha kwenye majaribu haya