25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM asamehe wafungwa 4,477

Na AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM

KUELEKEA maadhimisho ya Uhuru Desemba 9, Rais Dk. John Magufuli, ametoa msamaha kwa wafungwa 4,477 ambao kati ya hao 1,176 watatoka kesho.

Wafungwa hao wamesamehewa kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa Rais kupitia Ibara ya 45 (1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wakati akitoa salamu za kumbukumbu ya miaka 57 ya Uhuru.

Akizungumza Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakati wa kutoa salamu za maadhimisho ya miaka 57 ya Uhuru, Rais Magufuli, alisema msamaha huo utawahusu wafungwa ambao ni wagonjwa, wazee kuanzia miaka 70 na zaidi, wafungwa wa kike walioingia gerezani wakiwa wajawazito na walioingia na watoto wanaonyonya au wasionyonya pamoja na wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili.

“Halikadhalika nimeamua kwa wafungwa waliotumikia robo ya adhabu zao, wapunguziwe robo ya adhabu zao baada ya punguzo la kawaida la theluthi moja linalotolewa kwenye kifungu namba 49 (1) cha Sheria ya magereza sura ya 58,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hata hivyo, msamaha huo hautawahusu wafungwa wanaotumikia baadhi ya adhabu zikiwemo kunyongwa, kifungo cha maisha, biashara ya dawa za kulevya na binadamu.

Alisema wafungwa wengine ambao hawahusiki na msamaha huo ni wenye  makosa ya unyang’anyi, kukutwa na viungo vya binadamu, makosa ya kupatikana na silaha, risasi, milipuko isivyo halali, makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti.

“Makosa ya kuwapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, uhujumu uchumi, rushwa, ubadhirifu, ujangili, waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa rais, wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole, wenye makosa ya kutoroka au kujaribu ama kusaidia kutoroka chini ya ulinzi halali, msamaha huu hautawahusu,” alisema Magufuli.

Alisema wafungwa wengine ambao hawatahusika ni walioingia gerezani baada ya Desemba mosi mwaka huu au  waliowahi kufungwa na kurudi tena gerezani pamoja na wenye makosa ya kinadhamu magerezani.

Mbali na hilo, Rais Magufuli, pia alibainisha kuwa fedha zilizopangwa kufanya sherehe za maadhimisho ya Uhuru ambazo ni takribani Sh bilioni moja, ameagiza zitumike kwa ajili ya kujenga hospitali mkoani Dodoma.

“Kama mlivyosikia kutoka kwa Waziri Mkuu (Kassim Majaliwa), nilitoa maelekezo kwamba mwaka huu tusifanye sherehe badala yake fedha hizo zikajenge hospitali katika makao makuu ya nchi,” alisema Magufuli.

Alisema wananchi wanapaswa kuitumia siku hiyo ambayo ni ya mapumziko kutafakari Uhuru walionao, mahali walipotoka, mahali walipo na wanapoelekea.

Alisema Uhuru uliopatikana Desemba 9, 1961, ulikuwa mwanzo tu wa kuanza harakati za kutafuta uhuru mwingine.

 Rais Magufuli alisema uhuru unaopiganiwa sasa wa kiuchumi pengine ni mgumu zaidi kuliko ule wa mwanzo.

“Napenda kutumia fursa hii kuzipongeza Serikali za awamu zote za nchi yetu pamoja na Watanzania kwa mafanikio makubwa ya kiuchumi yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 57 iliyopita, sio siri kuwa Tanzania ya sasa si sawa na ile ya mwaka 1961, mambo mengi makubwa yamefanyika nchini mwetu,” alisema Magufuli.

Alisema pamoja na ukweli huo, ni wazi nchi bado ina safari ndefu ya kufika kule wananchi wanakotamani kufika ambako ni kujenga Tanzania iliyo imara zaidi, yenye amani na umoja.

Alisema wananchi wanatamani kuiona Tanzania yenye maendeleo ya kiuchumi na inayojitegemea.

“Tanzania ambayo huduma za kijamii zinapatikana kwa urahisi zaidi, Tanzania yenye watu walioelimika na Tanzania yenye watu wenye kipato kizuri,” alisema Magufuli.

Alisema anafarijika kuona katika kipindi cha miaka mitatu iliyokaa Serikali ya Awamu ya Tano, imetekeleza ndoto za  amani, umoja na Muungano wa Tanzania Bara na Zanzibar pamoja na kuendeleza juhudi za kukuza uchumi.

Alisema kwa sasa Tanzania ni miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakua kwa kasi barani Afrika.

Katika hilo alisema Serikali imefanikiwa  kuwavutia wawekezaji ambapo mitaji yenye thamani ya zaidi ya Sh trilioni 30 imeingia nchini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles