26.3 C
Dar es Salaam
Monday, December 6, 2021

Kijana adaiwa kupiga Sh bil 188 kwa EFD

*Afikishwa mahakamani akidaiwa kujifanya amesajiliwakukusanya kodi ya VAT kwa niaba ya TRA

NA PATRICIA KIMELEMETA

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imempandisha kizimbani mfanyabiashara, Mustapha Kambangwa (34), mkazi wa Kongowe Mbagala, Dar es Salaam na kumsomea mashtaka manne ikiwemo ya kujipatia shilingi  bilioni 188.9 kupitia mashine ya kielektroniki ya EFD.

Akisoma mashtaka jana mbele ya Hakimu Mkazi, Janeth Mtenga, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Christopher Msigwa, alidai mshtakiwa huyo alitenda makosa hayo kwa siku tofauti kati ya Juni mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu.

Alidai Kambangwa alijifanya kama mtu aliyesajiliwa kuwa mlipa kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

Alidai katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa alijifanya kuwa amesajiliwa kukusanya kodi ya VAT Sh 188,928,752,166 kwa kujifanya anakusanya fedha hizo kwa niaba ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Katika shtaka la pili kati ya Juni mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu, kwa udanganyifu alitumia mashine ya kielektroniki ya EFD yenye namba 03TZ842011315 iliyosajiliwa kwa jina la Kampuni ya Abraham’s Group LTD kukwepa kodi ya VAT yenye thamani ya fedha hiyo.

Katika shtaka la utakatishaji fedha, tarehe na kipindi hicho, maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, alijipatia au kujimilikisha fedha hizo alizozipata kutokana na makato ya kodi ya VAT ambazo zilipaswa kutolewa kwa Kamishna wa TRA na mshtakiwa huyo alipaswa kujua kuwa fedha hizo ni zao la kosa la ukwepaji kodi.

Wakili Msigwa alidai katika tarehe tofauti kati ya Juni mosi, 2016 na Novemba 2, mwaka huu maeneo ya Dar es Salaam kwa vitendo vya makusudi vya kukwepa kodi alitumia mashine ya kielektroniki  ya EFD na huku akijua kwamba hajasajiliwa kama mlipakodi ya VAT aliisababishia TRA hasara ya Sh 188,928,752,166.

Alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.

Hakimu Mtega alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo hadi itakapopata kibali.

Hata hivyo, Wakili wa Utetezi, Shamo Shadrack, aliiomba mahakama kupanga tarehe ya karibu ili kupinga mashtaka hayo dhidi ya mshtakiwa.

Upande wa mashtaka ulikubaliana na hoja hiyo na kudai kuwa hauna pingamizi kwa sababu hawajui ni mapingamizi gani yatakayowasilishwa.

Hakimu Mtega aliahirisha kesi hiyo hadi Desemba 17, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa na kuamuru mshtakiwa kwenda rumande kwa sababu mashtaka hayo hayana dhamana.

- Advertisement -
bestbettingafrica

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
168,340FollowersFollow
527,000SubscribersSubscribe
- Advertisement -
10Bet

Latest Articles