KATIKATI ya hizi lawama za hela kuamidika, mheshimiwa ana bana, kuna somo kubwa tunapata ambalo hatukuwahi kulipata huko nyuma. Somo la kuwa fedha na nafasi ni vitu vinavyotakiwa kutumiwa kwa umakini mno. Ukipewa nafasi na ukaichezea basi baadaye lazima ujute. Hali hiyo iko katika fedha pia.
Somo hili hatukuwahi kulipata hapo kabla. Zamani, enzi za utawala wa baba yake Ridhiwani ungeweza kupata pesa leo ukaichezea na katika mazingira ya ‘ajabu’ ukapata tena kesho. Hali hiyo haiko sasa. Hali ya kupata fedha pesa katika mazingira ya ajabu hata bila kuifanyia kazi ililemaza akili za wengi na kuona maisha ni kitu cha mchezo tu.
Namtafakari dada yangu Wema Sepetu. Kwa takribani miaka kumi ya umaarufu wake wa kiwango cha juu hakuna lolote kubwa la maana alilofanya. Hali hii imetokana na kutofunzwa nidhamu ya nafasi, fedha na mazingira aliyoyakuta.
Baada ya kuibuka mshindi wa Miss Tanzania 2016 kila kitu kwake kikaonekana rahisi. Baada ya ushindi wake miezi kadhaa baadaye akawa msanii maarufu wa filamu. Kumbuka njia aliyotumia kufika katika usanii maarufu ni tofauti sana na aliyotumia Monalisa, Thea na Riyama. Hawa ilibidi wahangaike sana ila kwa Wema ilikuwa rahisi sana kama kunywa maji.
Akiwa katika umaarufu wa filamu mara tukasikia ana uhusiano na Kanumba, mara wakaachana mara tukasikia ana uhusiano na Yusuph Jumbe mara wakaachana, tukasikia yuko na kigogo wa Ikulu. Kwa kuwa na huyo jamaa, Wema akajipambanua kwa matumizi yake kuwa naye ni miongoni mwa wasichana wa mjini wenye fedha.
Badala ya kufanya cha maana na hizo fedha ziliozokuwa zinamimika kwake kutoka kwenye walleti ya Clement iliyokosa zipu, huyo jamaa wa Ikulu, yeye akawa anafanya fujo za matumizi.
Leo ungesikia Wema kafanya kile, kesho ungesikia kaenda kule. Ni hapa ndipo tukawahi kusikia alikodi ndege akajaza marafiki zake wakaenda Arusha kutalii. Ni katika fujo hizi ndipo akakwea pipa akaenda China kufanya marekebisho ya ngozi yake.
Huwezi kumlaumu sana Wema kwa kufanya haya. Wema kawa maarufu akiwa bado kinda huku akikosa mazingira ya kumfunza nidhamu ya kutumia nafasi na pesa. Kwa kukosa nidhamu hiyo Wema aliona kila kitu kwake rahisi. Hata bila kuingiza ama kufanya kazi yoyote.
Clement angempa milioni kumi akaweke kwenye akaunti yake. Mazingira haya yalimpofusha na kujikuta akishindwa kutumia nafasi na kipaji chake inavyotakiwa.
Mwaka ajana nilisikia Wema yuko katika maandalizi ya kutoa filamu na kina Van Vicker. Hayo Wema alitakiwa kuyafanya miaka kadhaa iliyopita na sasa angekuwa maarufu Afrika huku akaunti yake ikionesha kufurika noti ambazo zingetokana na matangazo na mauzo ya filamu zake.
Ila Wema alilala, alipumbaa, Wema anashtuka leo baada ya Magufuli kuingia madarakani na kuwapoteza watu aina ya Clement ambao walikuwa wakimwaga pesa bila sababu kutoka vyanzo visivyo na maelezo ya kina.
Kwa somo hili analotoa Magufuli kuwa bila kazi hakuna pesa, Wema angepata umisi enzi za Magufuli sina sababu ya kutoamini kama angetumia vipaji vyake na nafasi yake ipasavyo na kumpa matunda maridhawa.
Anachofanya muheshimiwa mkuu wa nchi ni kutoa somo tu la umuhimu wa kutumia nafasi na kuwa na nidhamu sahihi ya pesa. Somo hili Wema lilimpita kando enzi za baba Ridhi kwa sababu bila kazi ya maana ungepata pesa kuliko aliyejipinda akifanya kazi usiku na mchana.