26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JPM ampa ujumbe mzito Lowassa

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM



RAIS Dk. John Magufuli, amemtaka Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuwaeleza viongozi wenzake wa chama chake watulie na kufuata sheria, vinginevyo wataishia gerezani.

Rais Magufuli alitoa kauli hiyo kabla ya kuzindua maktaba ya kisasa ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), iliyojengwa kwa msaada wa Serikali ya China wa Sh bilioni 90.

Katika hafla hiyo ambayo Lowassa pia alihudhuria, Rais Magufuli alimpongeza na kusema ni mwanasiasa mstaarabu ambaye hata baada ya kushindwa katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 alitulia.

Lowassa alihamia Chadema mwaka 2015 na kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho chini ya mwamvuli wa Ukawa baaada ya Kamati Kuu ya CCM kuondoa jina lake kwenye orodha ya watu walioomba kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Kabla ya kuanza hotuba yake, Rais Magufuli alianza kumpongeza Lowassa kuwa ni mwanasiasa mzalendo na mtulivu na kwamba taifa linahitaji wanasiasa waliokomaa wa aina ya waziri mkuu huyo wa zamani.

“Mzee Lowassa nakupongeza kwanza kwa utulivu wako, wewe tuligombea urais wote lakini nilipokutupa chini ukaenda kupumzika mzee wa watu.

“Ambao hata hawakugombea wakawa wanapiga kelele, wewe ukatulia mzee wangu kwa sababu unajua katika mashindano yoyote kuna kushindwa na kushinda.

“Mimi nakupongeza kwa moyo wako wa uzalendo wa kweli wa kitanzania na hili nalisema kwa dhati, tunahitaji watu wa vyama mbalimbali waliokomaa kama wewe kwa kweli wewe ni ‘super man’.

“Hongera na ndiyo maana umeweza kuja hapa kwa upendo mkubwa kuja kushiriki maendeleo ya Watanzania. Maendeleo hayana chama, hii ndiyo Tanzania ninayoitaka kuijenga, Tanzania ya Watanzania wa vyama vyote, waumini wote na inayojumuisha makabila yote, ninakupongeza sana Lowassa.

“Vyama vyetu kamwe visiwe chanzo cha kututenganisha bali viwe chachu ya kuleta maendeleo, kwa hiyo nimeona hili nilizungumze kwa heshima kubwa ili wale unaowaongoza kule ukawashauri otherwise (vinginevyo) wataishia kwenye magereza ili wakajifunze namna ya kuheshimu sheria za Watanzania,”alisema Rais Magufuli.

Pamoja na mambo mengine, Rais Magufuli alikipongeza chuo hicho cha Dar es Salaam, kwa kuendelea kuilinda heshima yake tangu ilipoanzishwa.

“Viongozi mbalimbali wamesoma katika chuo hiki cha Dar es Salaam, tunaweza kusema UDSM ni baba lao au mama lao, kwa hiyo hakuna njia ya kukwepa tusitafute mchawi hiki ndicho chuo kikuu cha kwanza cha Tanzania.

“Chuo hiki kwa sasa kina jumla ya wanafunzi 41,000 ukiunganisha DUCE na Mkwawa. Kwa hiyo ninaposema USDM hoyee! vyuo vikuu vingine ambao ni watoto wa UDSM msione wivu ninafanya kwa nia njema na bahati nzuri vyuo vyote vya elimu ya juu kuanzia elimu ya msingi vya serikali na binafsi vyote ni vyangu. Kwa hiyo wote ninawapenda lakini mzee katika hao ni UDSM,”alisema Rais Magufuli.

Alisema maktaba hiyo ni nyumba ya maarifa na ni kitu muhimu kwa maendeleo ya kielimu kwa sababu inatoa utulivu wa mtu kujisomea na kupata maarifa.

Alisema kuanzia mwakani Watanzania watakuwa wakinufaika na mafunzo ya uhudumu wa maktaba kupitia ufadhili huo uliotolewa na serikali ya China.

Aliitaka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kutoa mikopo ya wanafunzi kwa wakati kwa kuwa ni haki yao.

“Naambiwa asilimia 60 ya wanafunzi ndiyo wamepata mikopo wengine bado, Wizara ya Elimu na Bodi ya Mikopo mko hapa mwendelee kuwashughulikia wale ambao hawajapata mikopo.

“Pia naipongeza Bodi ya Mikopo kwa ufuatiliaji wa madeni ya mikopo, mwaka juzi walikusanya Sh bilioni 21, mwaka jana walikusanya zaidi ya bilioni 181 endeleeni hivyo hivyo ili fedha zinazopatikana ziendelee kuwakopesha hawa wanafunzi,”alisema.

Alitoa wito kwa wahadhiri wa chuo hicho kuwasimamia vizuri wanafunzi na kwamba yapo mambo madogo madogo ambayo ameanza kuyasikia lakini hatayasema kwa sababu ana imani uongozi wa chuo utayasimamia.

“Nitoe wito kwa walimu kusimamia wanafunzi; yapo mambo ambayo nimeanza kuyasikia madogo yanayofanyika nina uhakika mkuu wa chuo utayasimamia nisingependa kusema sana lakini yapo wenye kusikia wamenisikia,”alisema.

Alisema maktaba hiyo ambayo ina uwezo wa kuhudumia wasomaji 2001, makasha ya kuweka vitabu 800,000, ana imani sasa elimu ya vyuo vikuu itapanda.

“Wito wangu mwingine hakikisheni mnaitunza maktaba hii, iwe jengo lililojaa vitabu na chapisho lolote liweze kupatikana kwa wakati, hivyo muitunze iweze kutumika vizazi na vizazi.

“Jukumu letu watanzania ni kutumia vizuri misaada hii iweze kuleta maendeleo, nitashangaa siku nije nikute imechorwachorwa, vitabu vimeharibika kwa sababu inatakiwa iwe ukumbusho hii ni ushindi mkubwa wa maendeleo,”alisema.

Alimpongeza mkandarasi aliyejenga jengo hilo na serikali ya China, akisema imejengwa kwa kiwango cha juu.

“Shukrani zangu nyingi ziende kwa serikali ya China ni ndugu zetu na marafiki wa kweli wametoa zaidi ya Sh bilioni 90 za walipa kodi wa wananchi wa China wakatupa bure.

“Wangekuwa wengine tungepewa masharti ya ajabu, tungeambiwa tutembee migongo imeinama au tutembee kifudifudi tungepewa masharti ya kila aina lakini hawa wenzetu wanakupa kitu bila sharti lolote,”alisema.

Alisema maandalizi ya ujenzi wa maktaba hiyo yalianza katika awamu ya nne chini ya Jakaya Kikwete ambaye ndiye aliyetengeneza mazingira ya kupatikana fedha hizo.

“Unajua sisi wanasiasa wakati mwingine tuna tabia ya kusahau kazi zilizofanywa na wengine…maandalizi haya yalifanywa kwenye awamu ya nne chini ya mzee Kikwete,”alisema.

Awali, Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye alimshukuru Rais Magufuli kwa niaba ya chuo kukifanyia mambo makubwa chuo hicho.

Profesa Anangisye alisema thamani na vifaa vyote muhimu kwa ajili ya maktaba hiyo vipo na baada ya uzinduzi huo itakuwa tayari kutumika.

Mkuu huyo wa chuo, alimwahidi Rais Magufuli kuwa wataitunza maktaba hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa na uadilifu mkubwa.

Naye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema maktaba hiyo itakuwa chachu ya kuboresha kiwango cha elimu hapa nchini na kwamba wataimarisha ulinzi.

Alisema wote ambao watabainika kuihujumu maktaba hiyo ya kisasa watachukuliwa hatua kali za kisheria.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles