25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

JPM AKERWA UCHELEWESHAJI BOMBA LA MAFUTA UGANDA-TANGA

 

ANDREW MSECHU Na NORA DAMIAN, Dar es Salaam


RAIS Dk. John Magufuli, amewataka mawaziri na wataalamu wote wanaohusika na ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga, kuharakisha mradi huo ili historia ya ujenzi wake ikamilike.

Mradi wa bomba la mafuta ghafi unatekelezwa katika nchi mbili ambapo kilometa 1,445 zitakuwa Tanzania na 298 zitakuwa nchini Uganda na unakadiriwa kugharimu Dola za Marekani bilioni 3.55.

Akizungumza jana baada ya kukutana na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Ikulu Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema pamekuwepo na ucheleweshaji wa ujenzi wa bomba hilo.

“Mawaziri na wataalamu wote wanaohusika na mradi huu, waupeleke kwa ‘speed’ kubwa kwa sababu pamekuwa na ucheleweshaji kidogo.

“Wahakikishe unaanza mapema ili historia ya kujenga mradi huu iweze kukamilika,” alisema Rais Magufuli.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli, ametahadharisha kuwa sukari ya magendo isipodhibitiwa, nchi za Afrika Mashariki zitaendelea kuwa dampo na kuathiri viwanda vya ndani.

Rais Magufuli alisema utandawazi wa biashara ni mzuri, lakini ni lazima kuwa makini na anapenda bidhaa za nchi nyingine zije Tanzania na za kutoka Tanzania ziende katika nchi nyingine za EAC.

Alisema taarifa alizonazo, kila siku kuna malori zaidi ya 20 yenye sukari ya magendo yanayoingia katika mpaka wa Sirari.

“Sukari ikija nyingi kutoka nje inaua viwanda na kupunguza ajira, lazima pengo la sukari liangiliwe vizuri ili kusudi nchi zetu zisije kuwa dampo.

“Tuliwatuma mawaziri wa biashara wakakutana Mtukula, wanalishughulikia suala hili, lakini kama tunataka kujenga viwanda na uwezo wa Watanzania na Waganda kupata ajira, hili suala lazima tuliangalie kwa weledi mkubwa kwa kuzingatia sheria zetu ili kuepuka nchi yetu kuwa dampo,” alisema Rais Magufuli.

Alisema kuna wakati sukari nyingi iliingia Kenya na Uganda na nyingine ilipitia Tanzania, lakini haikutengenezwa na viwanda vya Uganda bali kuna watu walikuwa wakiingiza na kuharibu soko la viwanda vya Uganda.

“Sukari ya aina hiyo ilitaka kuingia kupitia Zanzibar ambapo mahitaji ya Zanzibar ni tani 20,000, kiwanda kinatengeneza tani 4,000 hadi 5,000. Lakini walitaka kuleta huku kuuza. Tatizo hilo hilo lilitokea sukari nyingine ilipita Kenya nyingine ni mbovu, tumeona hili tuliangalie upya,” alisema.

Hata hivyo, alisema kwa sasa viwanda vya ndani kikiwamo Kagera Sugar vina sukari ya kutosha na maghala yamejaa hadi nyingine wanaiweka nje.

Alisema pia wamekubaliana kuimarisha biashara kati ya Uganda na Tanzania, ikiwemo suala la kuwa na treni ya kutoka Dar hadi Uganda baada ya kusimama kwa miaka 10.

Kulingana na Rais Magufuli, safari moja ya kwanza ilibeba tani zaidi ya 1,000 ambazo ni sawa na kubeba semi-trela kati ya 40 na 50 na kwa gharama nafuu.

Alisema kwa pamoja wamefurahi kuona wakimbizi wa Burundi wanarudi kwao, ishara ya kwamba sasa kumetulia suala ambalo linawafurahisha wanachama wote wa EAC.

Rais Magufuli alisema anamwona Museveni kama Mtanzania na mfuasi mzuri wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, hivyo Watanzania washirikiane kujenga nchi zao kwa kuwa wote ni ndugu.

Alisema pia mpango wa ujenzi wa Stigler’s Gorge wa megawati zaidi ya 2,100 ukikamilika wataangalia namna ya kupunguza bei ya umeme kwa sababu umeme unaotengenezwa kwa kutumia nguvu za maji na usiolipiwa gharama za huduma utasaidia nchi kuondokana na matatizo ya umeme.

Rais Magufuli alisema pia wana mpango wa kununua meli kubwa katika Ziwa Victoria na ununuzi wa ndege saba ambazo tayari nne zimeshawasili na zitakapokamilika suala la usafiri katika Afrika Mashariki litakuwa limesaidiwa.

 MUSEVENI

Rais Museveni alimshukuru Rais Magufuli kwa ujenzi wa reli ya kisasa, ambayo itasaidia kupunguza gharama za usafirishaji wa mizigo tofauti na ilivyo sasa.

Alisema hatua ya kufufua usafiri wa gari moshi itasaidia nchi yake kupunguza gharama kubwa za usafirishaji wa barabara ambazo wamekuwa wakiingia kwa sasa.

Musevani alisema japokuwa kwa sasa barabara zimetengemaa kwa kiasi kikubwa, lakini gharama za kusafirisha bidhaa bado zimeendelea kuwa kubwa.

“Wakati mwingine tamaa inaua akili, tamaa inakuwa ya juu zaidi kuliko akili ya watu. Hili jambo la kusafirisha mizigo kwa malori, wafanyabiashara wanapata fedha lakini tunaharibu uchumi kwa sababu kusafirisha bidhaa kwa magari gharama inakuwa juu karibu mara tatu kuliko kutumia gari moshi, kwa hiyo namshukuru Magufuli kwa uamuzi huo,” alisema.

Museveni ambaye aliwasili nchini kwa ziara ya siku moja, alisema mambo mengine waliyozungumza na kukubaliana kuyaharakisha ni ujenzi wa mitambo ya umeme kwenye Mto Kagera wa Muriongo na wa Kigagati ambayo wamekubaliana iharakishwe.

Alisema pia walizungumzia suala la Burundi, hasa baada ya kuimarika kwa usalama na wakimbizi wakiwemo wa Bulyankulu waliokuwepo nchini tangu mwaka 1972 wameanza kurudi kwao.

Kuhusu Sudan Kusini ambao wamekuwa na vita ya kikabila, alisema sasa wamefanya mkataba hali inayoonyesha wamechoka kupigana.

“Watu wakipigana sana huchoka, hivyo hatua ya kufikia makubaliano ni mwanzo mpya wa safari ya kupata amani,” alisema.

Alisema kuna wakimbizi milioni 1.4 kutoka Sudan walio Uganda na ana matumaini watarudi kwao, lakini wanapanga Umoja wa Mataifa uwapatie chakula, vifaa vya kilimo na mbegu ili mvua zitakapoanza Machi mwakani, waanze kujishughulisha na kilimo.

Museveni alielezea pia uwakilishi wake kwenye mkutano wa BRICS nchini Afrika Kusini ambako aliwakilisha Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kama mwenyekiti wake.

Alisema alihimiza utamu wa Afrika Mashariki kibiashara na kuwaeleza ni kwa namna gani kampuni zao zitapata faida kwa kuwekeza katika nchi za Afrika Mashariki.

Museveni alisema mapato ya uwekezaji Afrika Mashariki yako juu kuliko Bara la Ulaya, Amerika ya Kusini na Asia, ikiwa ni njia yake ya kuuza uzuri wa Afrika Mashariki kwa wale wanaotaka kufanya biashara.

Alisema kampuni za nchi hizo zikiweka biashara ni katika miundombinu ya barabara, garimoshi, usafiri kwenye ziwa na umeme.

“Wachina wanajenga mabwawa mawili ya umeme Uganda, moja ni Kauma na Isimba, ni mifano kuwa wanaweza kufanya katika nchi nyingine Afrika Mashariki,” alisema.

Musevani alisema eneo jingine ni biashara katika viwanda, ambako kuna kampuni ya Wachina imejenga kiwanda cha kutengeneza vyuma (iron ore) vitakavyosaidia ujenzi wa mabwawa na garimoshi, ambavyo vyote vinataka saruji na chuma.

“Kwa sasa hivi vitu hivyo vinapatikana kutoka China kwa sababu wanasema saruji kutoka hapa si nzuri kwa ujenzi wa mabwawa, viwanda sasa vinatengeneza na vimeongezeka kwa sababu mabwawa na garimoshi vinataka bidhaa hiyo,” alisema.

Museveni alisema pia alimwomba rais wa China alete Wachina milioni moja katika nchi za Afrika na kwamba wamefufua tena kampuni ya ndege ya Serikali ambayo ilikufa na wanatarajia kuanza safari za kwenda nje, ikiwamo China ili kurahisisha biashara ya utalii.

 

 

 

 

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles