29.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

JPM aitwisha mzigo TPA

magufuli1*Ataka inunue mashine nne haraka

*Aagiza mkataba wa TICS uangaliwe upya

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Rais Dk. John Magufuli, ametoa miezi miwili kwa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) kununua mashine nne za kukagulia mizigo bandarini (Scanning Mashine).

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Mkurugenzi wa Mawasilino Ikulu, Dar es Salaam jana, ilisema Rais Dk. Magufuli alitoa maagizo haya baada ya kutembelea Bandari ya Dar es Salaam, kisha kuzungumza na viongozi na wafanyakazi.

Rais alifikia uamuzi huo, baada ya kubaini  kati ya mashine nne za ukaguzi wa mizigo zilizopo, ni  mbili tu ndiyo zinazofanya kazi na hazina uwezo wa kukagua mizigo yote inayotoka na kuingia nchini kupitia bandari hiyo hali inayosababisha kutokuwapo kwa udhibiti wa uhakika wa udanganyifu.

“Kwa hiyo nawaagiza TPA, na Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Profesa  Mbarawa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mpo hapa, hakikisheni mnanunua mashine za kukagulia mizigo nne ndani ya miezi miwili na ikifika miezi mitano muwe mmenunua mashine sita, lazima mizigo yote ikaguliwe kwa mashine” alisema Rais Dk. Magufuli

Pia aliiagiza TPA kwa kushirikiana na wizara husika kuanza mazungumzo na Kampuni ya Kimataifa ya Kuhudumia Makasha bandarini (TICTS) ambayo inapakia na kupakua mizigo katika gati namba nane hadi kumi na moja ili kurekebisha mkataba ambao kampuni hiyo imeingia na Serikali kwa lengo la kuhakikisha nchi inapata manufaa yanayostahili.

Rais Magufuli alitembelea eneo la mita za kupimia mafuta yanayopakuliwa melini (Flow Meters) na kubaini  mita hizo hazifanyi kazi.

Ameiagiza TPA kuharakisha mchakato wa kununua mita mpya na kuzifunga katika eneo hilo ili kudhibiti ukusanyaji wa mapato ya kodi ya mafuta.

Kutokana na hali hiyo, Rais Dk. Magufuli ameitaka TPA kujipanga kujenga bandari kavu (ICD) eneo la Ruvu mkoani Pwani  ili kuachana na bandari kavu zilizoanzishwa na watu binafsi hapa jijini Dar es Salaam ambazo zimekuwa zikitumika kukwepa kodi.

Akizungumza na wafanyakazi  baada ya kumaliza kutembelea bandari, Rais Magufuli amewatoa shaka wafanyakazi hao na  wengine serikalini, kuwa kazi ya kuhakiki vyeti inayoendelea nchi nzima haina lengo la kuwafukuza kazi, bali inafanywa kwa lengo la kukabiliana na tatizo la wafanyakazi hewa ambao wamefikia 17,500 na pia kuondoa tatizo la wafanyakazi wanaotumia vyeti vya kufoji.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alimwapisha Dk. Zainab Chaula kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Dk. Zainab amejaza nafasi iliyoachwa wazi na Dk. Deodatus Mtasiwa ambaye amestaafu utumishi wa umma. Kabla ya uteuzi huo, Dk. Zainab alikuwa Mganga Mfawidhi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles