28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JPM aguswa na msimamo wa Askofu Chengula

Mwandishi wetu-Dar es Salaam



RAIS Dk. John Magufuli, ameguswa na msimamo aliokuwa nao marehemu Askofu wa Jimbo Katoliki la Mbeya, Evalisto Chengula, akisema ni viongozi wachache wanaoweza kusimama na kusema ukweli.

Rais Magufuli ametoa sifa hiyo jana alipoungana na Maaskofu, Mapadre, Watawa na Waumini wa Kanisa Katoliki kutoa heshima za mwisho kwa Askofu Chengula aliyefariki dunia Novemba 21, mwaka huu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa Matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, jana katika misa hiyo iliyofanyika kwenye Kanisa lililopo Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu, Kurasini Jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema pamoja na majukumu yake ya kutoa huduma za kiroho, marehemu Chengula alisimamia ukweli ikiwemo kupinga hadharani ndoa na mapenzi ya jinsia moja licha ya kuwepo mashinikizo mbalimbali.

“Baba Askofu Chengula ameitangaza injili kweli kweli, amekuwa mkweli kwa kuhuburi injili kwa kweli, hakusita kuzungumza ukweli na hivi karibuni nafikiri katika mwezi huu alizungumza kuhusu kupinga hadharani ushoga.

“Ni watu wachache sana viongozi ambao wanaweza kujitokeza hadharani na kuzungumza ukweli ulioko kwenye biblia takatifu, tuendelee kumuombea baba askofu lakini kazi yake ya kuitangaza ijili kwa ukweli ameitimiza salama, sisi wote tumezaliwa na sote tutaondoka,” alisema Rais Magufuli kwenye misa hiyo.

Misa Takatifu ya kumuaga Marehemu Askofu Chengula iliongozwa na Askofu Mkuu Mwandamizi Jude Thadaeus Ruwaichi na kuhudhuriwa pia na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu Benjamin Mkapa na mkewe Mama Anna Mkapa.

Akitoa salamu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Makamu wa Rais wa TEC, Askofu Flavian Kasalla, alimshukuru  Rais Magufuli kwa ushirikiano alioutoa wakati wa kuuguza na baada ya kifo cha Askofu Chengula na pia amewashukuru madaktari na wauguzi, viongozi na wote waliokuwa wakimuombea kabla na baada ya kifo.

Askofu Chengula amefariki dunia kwa ugonjwa wa moyo na baada ya misa hiyo ya kuuaga mwili wake umesafirishwa kwenda Mbeya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles