30.8 C
Dar es Salaam
Thursday, November 14, 2024

Contact us: [email protected]

Wastaafu wavuna mabilioni

PATRICIA KIMELEMETA



TANGU kuanza Agosti mosi ilipoanza kutumika Sheria Mpya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, wastaafu 4,900 wamelipwa pensheni zaidi ya Sh bilioni 379.

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Dk. Irene Isaka, kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Jijini Dar es Salaam jana.

Alisema wastaafu hao wamelipwa pensheni hizo baada ya kukokotolewa fedha zao kulingana na sheria mpya ambayo inawataka kuwalipa wastaafu hao asilimia 25 kwa mkupuo huku asilimia 75 iliyobaki ikilipwa kama mshahara wa kila mwezi kwa muda wote wa uhai wa msfaafu.

“Tunapenda kusisitiza kwamba pensheni hailipwi kwa miaka 12.5 tu bali kwa muda wote wa uhai wa wastaafu. Na hata baada ya hapo wategemezi wataendelea kulipwa kwa kipindi cha miezi 36 (miaka mitatu),” alisema.

Akizungumzia wastaafu waliolipwa pensheni zao, alisema ni wale waliokua kwenye mifuko mbalimbali ya hifadhi ya jamii, lengo ni kuhakikisha kuwa, wanapata fedha zao kwa wakati ili waweze kuendeleza shughuli zao, zikiwamo kilimo na biashara.

“Sheria ilipitishwa Agosti Mosi mwaka huu, ambapo mpaka sasa tumeweza kulipa zaidi ya Sh bilioni 397 kwa wastaafu waliokua kwenye mifuko mbalimbali ikiwamo ya NSSF na PPF,”alisema Isaka.

Kuhusu wanaolalamikia ukokotoaji mpya, alisema. “Malalamiko ambayo yamekuwa yakitokea kutoka kwa wanachama na yale ambayo yamepokelewa rasmi na SSRA mengi yanaonyesha kwamba ni yale yanayotokana na wanachama wa PSPF waliokopa mikopo ya nyumba kwa kutegemea kwamba watalipwa mkupuo wa asilimia 50.

“Hivyo kwa kuwa sasa wanapokea asilimia 25 wanaona kwamba mkupuo huo hautoshi kulipa deni la nyumba na kubakiwa na kiasi cha kuweza kutosheleza mahitaji yao mengine.

“Jambo hili tunalifanyia kazi kwa lengo la kuhakikisha mifuko inabuni namna bora zaidi yenye unafuu katika ulipaji wa deni la nyumba mathalani kwa kuongeza muda wa marejesho ambao utaleta nafuu kwa wanachama,” alisema Dk Isaka.

Alisema, lengo la Serikali la kuunganisha mifuko ya hifadhi ya jamii ni pamoja na kuweka usawa wa wanachama kwa kuwa wote wanachangia asilimia 20 ya mshahara wao katika kipindi chote cha utumishi ambapo Serikali inachangia asilimia 15 na mtumishi anachangia asilimia 5 kutoka kwenye mshahara wake (wale wa umma).

Alisema mkakati wa serikali ni kuhakikisha, wanachama wananufaika na mifuko hiyo baada ya kuwepo kwa mafao mbalimbali likiwamo la mkopo wa biashara, kilimo na ujenzi wa nyumba.

Alisema katika mikopo hiyo, mwanachama anaweza kuchukua fedha ili aweze kuwekeza, jambo ambalo linaweza kusaidia kuendesha biashara au kilimo pindi anapostaafu.

“Tumebaini kuwa, wafanyakazi wengi wanafariki mara baada ya kustaafu wakiwamo viongozi wa Serikali, kwa sababu wanakuwa hawajawekeza popote, hali ambao inamfanya kuishi kwenye mazingira magumu, hivyo basi kuanzishwa kwa mifuko hii kutawasaidia wafanyakazi hao kupata mitaji ya kuendesha shughuli mbalimbali,”alisema.

Aliongeza, mkakati wa Serikali ni kuendelea kuhamasisha sekta binafsi ili waweze kujiunga na mifuko ya hifadhi ya jamii ili waweze kunufaika na mafao mbalimbali yanayotolewa.

Juzi Dk Isaka alisema kilichobadilika ni kiwango cha mkupuo kwa kundi dogo la wanachama takriban asilimia 20 ya wanachama waliokuwa wakipokea mkupuo wa asilimia 50 kwamba sasa ili wawe sawa na wanachama wenzao wa mifuko mingine wanaopokea asilimia 25.

Alifafanua kuwa haikuwa sahihi kundi dogo la wanachama kulipwa mkupuo mkubwa.

“Taarifa halisi za malipo zinaonesha kwamba mwanachama wa PSPF /LAPF anapokea mkupuo ambao ni zaidi ya mara tatu ya michango aliyochanga kwa kipindi chote cha ajira yake tofauti na wanachama wenzake waliopo mifuko mingine kama vile NSSF na PPF,” alisema.

Alisisitiza kuwa asilimia 25 iliyopunguzwa kwenye mkupuo imewekwa kwenye pensheni ya mwezi ambapo imeongezeka kwa asilimia 50.  “Kwa hiyo si sahihi kusema wanachama wamepunjwa mafao yao,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema lengo la kuinganisha mifuko ni pamoja na kuweka usawa kwa wanachama kwa kuwa wote wanachangia asilimia 20.

“Je ni sawa mwanachama wa NSSF anayechangia  asilimia 10 apate mkupuo asilimia 25 wakati mwenzake wa PSPF anayechangia asilimia 5 apate asilimia 50 kwa nchi inayofuata misingi ya hifadhi ya jamii” ?alihoji Dk. Isaka.

“Hili si jambo gumu kwani kunaweza kufanyika makubaliano na mfuko kuona namna ya kuondokana na changamoto hiyo,” alisema.

Alisema pia ili kuhakikisha kwamba wastaafu hawapunjwi na mfuko mpya wa PSSSF, wametuma wakaguzi maalumu kujiridhisha kwamba ukokotoaji umefanyika kwa mujibu wa kanuni na taratibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles