Na AGATHA CHARLES – DAR ES SALAAM
RAIS Dk. John Magufuli, amefuta maelekezo yaliyotolewa kwa njia ya barua na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwenda kwa wakuu wa vyuo vya ualimu,vyuo vya maendeleo ya jamii, vyuo vikuu na vyuo vikuu vishiriki na taasisi zilizo chini ya wizara hiyo, kuhusu matumizi sahihi ya rangi ya bendera na wimbo wa Taifa.
Katika taarifa yake iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Gerson Msigwa, Rais Magufuli alifuta barua hiyo iliyokuwa na kichwa cha habari ‘Matumizi sahihi ya bendera,nembo na wimbo wa taifa’ kutokana na kutoa maelekezo yanayoathiri uzalendo wa Watanzania na kuleta mkanganyiko wa tafsiri ya rangi na alama zilizomo katika bendera ya Taifa.
“Hata mimi (Rais) tangu nasoma shule hadi leo, na fahamu kuwa Bendera ya Taifa ina rangi ya njano na si rangi ya dhahabu. Rangi hiyo inawakilisha madini yote si dhahabu pekee. Kwahiyo nimeamua kuifuta barua hiyo na kama kuna mabadiliko basi ni lazima yafanyike kwa kuzingatia taratibu zote kwa kuwa jambo hili ni la kitaifa, si la mtummoja,” alisema Rais Magufuli.
Kutokana na hilo, Rais Magufuli aliagiza Bendera, Nembo na Wimbo wa Taifa viendelee kutumika kama ilivyokuwa kabla ya kuandikwa kwa barua hiyo.
Rais Magufuli alitoa wito kwaWatanzania kuendelea kuwa wazalendo, kuipenda nchi na kuitangaza popote walipo ilimradi wazingatie sheria na masilahi ya Taifa.
Barua hiyo iliyoandikwa naWizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia (baada ya kupokea maelekezo ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi), ilikuwa na kumbukumbu namba CH.56/193/02/16 ya Nov 23,2018.
Maelekezo katika barua hiyo yalieleza kuwa kumekuwa na matumizi yasiyo sahihi yanayofanywa na taasisi za Serikali.
Sehemu ya barua hiyo ya wizara ilisomeka: “Wimbo wa Taifa utapigwa kwenye dhifa za kitaifa, endapo hadhi ya sherehe haitambuliki, taasisi italazimika kuomba kibali kwa waziri mwenye dhamana.”
Kuhusu rangi za bendera ya Taifa, barua hiyo ilielekeza “Rangi za bendera ya Taifa ni kijani, dhahabu, nyeusi na bluu. Ni makosa kutumia rangi ya njano na uwiano wa bendera ni 2/3 katika urefu na upana.”