28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JPM afichua siri ya wakwepa kodi

ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM



RAIS Dk. John Magufuli amefichua siri ya wafanyabiashara wanaokwepa kodi huku akiitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kutumia mbinu za kisasa kukusanya mapato,badala ya zile za zamani.

Alisema wafanyabiashara wakubwa wamekuwa wakiwatumia wamachinga kuuza bidhaa zao ili wasilipe kodi, kitendo ambacho kinaikosesha Serikali mapato.

Kutokana na hali hiyo, aliitaka TRA ijitathmini sababu za watu kukwepa kodi.

Rais alitoa kauli hiyo jana wakati akiweka jiwe la msingi katika mradi wa kuboresha huduma za majisafi na taka katika Kijiji cha Kimnyaki mkoani Arusha.

Mradi huo  utakaogharimu Sh bilioni 20 unahusisha visima vitakavyochimbwa kumaliza tatizo la maji katika Jiji la Arusha.

Dk. Magufuli alisema wakati mwingine TRA imekuwa ikiweka kiwango kikubwa cha kodi hata kwa mtu anayefanya biashara ndogo.

“Natoa wito kwa TRA mbali na kuchukua hatua kali kwa wakwepa kodi, inafaa pia mtathmini sababu zinazofanya watu kukwepa kodi, wakati mwingine chanzo ni ninyi wenyewe TRA.

“Mnaweka viwango vikubwa mno ambavyo havilipiki…unakuta mtu una kaduka kadogo lakini kodi unaambiwa kubwa zaidi kwa hiyo mwenye duka anaamua kukwepa.

“TRA mliangalie hilo, ni bora kuweka kiwango kidogo kidogo chenye kulipika kuliko kuwa na viwango vikubwa ambavyo watu wachache ndiyo wanaomudu kulipa.

“Ndiyo maana maeneo mengi TRA hamkusanyi kodi kwa sababu mipango yenu imekuwa ya  zamani badala ya kujenga urafiki na walipa kodi.

“Ninyi mnajenga uadui na walipa kodi  badala ya kukaa na kuzungumza nao, ninyi mnawapelekea polisi kuwashika.

“Sasa ninawasihi TRA na Wizara ya Fedha, hebu mkae mjenge mkakati wa kweli ‘fair play’ ya kodi mnazokusanya   wananchi wanaotaka kwenda kulipa kodi waone ni fahari kulipa kodi badala ya kukimbia kulipa kodi.

“Toeni elimu na faida ya kulipa kodi kwa wananchi, kweli kodi nyingine za TRA zinaudhi na wako wengine wanakwenda kule wanazungumza hapa kazi tu niliwatuma kukusanya kwa namna hiyo za dhuluma?

“Niwaombe viongozi wa mikoa na wilaya na maeneo mengine tunahitaji kodi lakini si ya dhuluma, hatuwezi kujenga taifa la namna hiyo.

“Wafanyakazi wa namna hiyo wa TRA hawana nafasi katika serikali, kwa hiyo sisi sote ni walipa kodi na watoza kodi  kwa kutambua kwamba hizi fedha zinahitajika kwa maendeleo yetu.

“Watanzania tulipe kodi, nasikitika sana kwa tabia iliyoshamiri ya kukwepa kodi katika maeneo mbalimbali.

“Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mbinu mbalimbali kukwepa kodi ikiwamo kuwatumia wafanyabiashara wadogo wadogo kuwauzia bidhaa, kuacha kutumia mashine za EFDs na kutumia risti feki ambazo si ya thamani halisi ya bidhaa.

“Mtu anakuwa na duka lake kubwa anachukua wafanyabiashara wadogo wadogo kama 10, kila siku asubuhi anawapa hizo bidhaa na kwa sababu tumetoa ruhusa ya wamachinga kufanya biashara kila mahali sasa umekuwa ndiyo mchezo.

“Tabia ya namna hiyo inakosesha sana serikali mapato ambayo ingetumika kutengeneza miradi ya maendeleo kama huu wa maji.

“Hivyo ninawasihi sana wananchi watambue umuhimu wa kulipa kodi na niwaombe rafiki zangu machinga msikubali kutumika kukwepa kodi.

“Serikali iliamua kuwaruhusu kuendelea kufanya shughuli zenu sehemu mbalimbali  mjipatie kipato sasa msitumie vibaya fursa mliyopewa na serikali.

“Tunataka wamachinga na mamalishe wafanikiwe, lakini mnapokwenda dukani kuchukua bidhaa zaidi ya Sh milioni 60 unakaa nayo pale halafu mwenye duka anakusubiri jioni umletee fedha na mwenye duka tajiri anakwepa kodi hapo tunaenda vibaya.

“Serikali isiyokusanya mapato ni mfilisi kwa hiyo niwaombe sana wafichueni watu wenye tabia hiyo  wasiwaharibie.

“Leo tumekopa mkopo wa Sh bilioni  20 na baada ya muda tutaanza kulipa deni, wakati huo wananchi wawe na maji hivyo wananchi wasaidie kulipa hili deni bila vikwazo vyovyote,”alisema Rais Magufuli.

Alisema kama ilivyokuwa kwa mikopo mingine inavyolipwa na watu kutoka sehemu mbalimbali ndivyo hivyo itakuwa katika fedha hizo.

“Tena mradi huu tumeuleta katika eneo ambalo nilikuwa natukanwa lakini yote ni kwa sababu maendeleo hayachagui chama wala kabila,”alisema.

Rais Magufuli alisema maji yanayozalishwa katika eneo hilo ni lazima yawanufaishe watu wote ambao mradi huo utapita kuhakikisha  dhana halisi ya mradi mkubwa inazaa matunda.

Aliishukuru Benki ya Maendeleo ya Afrika ambayo inatoa mikopo isiyo na masharti kama ilivyokuwa kwa benki nyingine ambazo hutoa mikopo isiyokuwa na faida.

Alisema hakuna sababu ya kucheleweshwa mradi huo kutokana na uzembe na kwamba wakandarasi ambao hawatimizi wajibu wao wafukuzwe.

“Wakati nikiwa waziri nilifukuza wakandarasi wengi na walioenda kuniombea laana haikunipata kwa sababu Mungu anataka kazi zifanyike.

“Kwa hiyo na wewe Waziri wa Maji (Profesa Makame Mbarawa) usiogope ukiona kandarasi ambaye amepewa kazi na akashindwa kutimiza wajibu fukuza kwa sababu anachelewesha wananchi hawa kupata maji.

“Tumekopa fedha hizi ambazo baadaye tutakuja kuzilipa kwa ajili ya wananchi hawa wanyonge, wameteseka mno.

“Wapo watu ambao tangu dunia ianze hawajawahi kuona maji ya bomba ni lazima tuwahudumie hilo ndilo jukumu letu na jukumu la serikali yangu.

Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa alisema mpaka ifikapo Juni mwaka 2020 miradi ya maji 1801 itakuwa imetekelezwa.

Profesa Mbarawa alisema mpaka sasa miradi 500 iko katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Alisema miradi hiyo imeelekezwa katika maeneo mbalimbali ya nchi yaliyo na changamoto ya maji  kuhakikisha lengo la serikali la kuwapatia wananchi maji safi linafanikiwa.

“Miradi hii inatuhakikishia kuwa ifikapo 2020 kupitia ilani ya CCM ambayo inasema watu wote wanaoishi katika mikoa wapate maji kwa asilimia 95, wilaya asilimia 90 na vijiji asilimia 85,”alisema.

Alisema mradi huo uliozinduliwa na utakaogharimu Sh bilioni 520, ni miongoni mwa miradi inayotekelezwa hivi sasa huku akiwahakikishia wananchi kuwa watapata maji saa 24, siku saba kwa wiki.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles