Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
RAIS Dk. John Magufuli amefanya uteuzi mzito wa majaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani, huku akitengua nafasi mbili za wakuu wa wilaya.
Akitangaza uteuzi huo Ikulu Dar es Salaam jana jioni, Katibu Mkuu Kiongozi, John Kijazi, alisema katika uteuzi huo, Rais Dk. Magufuli amewatea majaji sita wa Mahakama ya Rufani.
Aliwataja kuwa ni Jaji Sahel Barike, Jaji Dk. Marry Levira, Jaji Rehema Sameji, Jaji Winnie Koroso, Jaji Ignas Kitusi na Lugano Mwandambo.
Alisema majaji wa Mahakaama Kuu walioteuliwa ni Cyprian Mkeha, Dustan Ndunguru, Seif Kulita, Dk. Ntemi Kirikamajenga, Zepharine Maleba, Dk. Juliana Masabo, Mustapha Ismail, Upendo Madeha, Wilbad Mashauri, Yohane Masara, Dk. Lilian Mongera, Fahamu Mtulya, John Kahyoza, Athman Kirati na Suzan Mkapa.
Kuhusu uteuzi wa wakuu wa wilaya, Balozi Kijazi alisema Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Glorious Luoga na nafasi yake kuchukuliwa na Charles Kabeho.
Pia alisema Rais Magufuli ametengua uteuzi wa Mkuu wa Wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro, Aron Mbogho na kumteua Thomas Apson kuchukua nafasi hiyo.
Alisema Rais ameteua wakurugenzi watendaji 10 kujaza nafasi zilizokuwa wazi.
Walioteuliwa ni Halmashauri ya wilaya ya Pangani, Isaya Benje, Dk. Fatuma Mganga (Bahi), Regina Byeda (Tunduma) na Jonas Marosa (Ulanga).
Wengine ni Ally Juma Ally (Njombe), Misana Kangura (Nkasi), Deogretius Lutema (Kibondo), Neto Ndilito (Mufindi), Elizabeth Gumbo (Itilima) na Stephen Ndani (Kishapu).
Alisema majaji wote walioteuliwa wataapishwa Ikulu kesho saa 3 asubuhi, wakuu wa wilaya nao wanaotakiwa kufika Ikulu kesho kwa ajili ya kupewa kiapo cha kazi na kula kiapo cha maadili.