NA FLORENCE SANAWA- MTWARA
RAIS, Dk. John Magufuli, ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na Wizara ya Viwanda na Biashara kuhakisha mwekezaji Alhaji Aliko Dangote, anapata makaa ya mawe na gesi asilia ili uzalishaji uwe mkubwa.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa magari 580 ya kiwanda hicho, Rais Magufuli alisema kumekuwa na utaratibu mbaya wa upatikanaji wa nishati hizo hali ambayo imekuwa ikikwamisha uzalishaji wa saruji katika kiwanda hicho.
Alisema TPDC inapaswa kuwa na usimamizi mzuri katika utoaji wa gesi bila kutumia kampuni nyingine ambazo zimekuwa zikiharibu utaratibu wa mwekezaji katika kiwanda hicho, hivyo kufifisha uzalishaji mkubwa unaotakiwa kufanywa.
Magufuli alisema kitendo cha Kampuni ya Aqual kupata zabuni ya kuzalisha umeme na kumuuzia Dangote hakikubaliki, hivyo aliwataka TPDC kusimamia zoezi hilo na kuzungumza na mwekezaji huyo moja kwa moja bila kutumia watu wengine ambao wako kibiashara zaidi.
Rais Magufuli alisema kitendo cha kampuni hiyo kukosa gesi wakati kiko kilomita 10 kutoka inapochimbwa gesi hiyo hakileti picha nzuri kwa wawekezaji wengine wakati kilomita 500 hadi Dar es Salam gesi imeweza kufika.
“Haiwezekani gesi inatoka Mtwara imetumia kilomita 500 hadi Dar lakini eneo la kilomita 10 imeshindwa kufika, leo nasema tumalizane hapa hapa gesi isipitie kwenye kampuni yoyote ipo kampuni imejiingiza katikati inataka kuingia mkataba na TPDC ili inunue gesi yenyewe iuze kwa Dangote ndani ya kilomita 10, kwanini hawakuingia mkataba ilipokuwa inaenda Dar es Salaam.
“Aqual wanafanya biashara ya ajabu kweli, huu ni utapeli walioleta, Aqual ni wawakilishi wa Dangote wengine wako hapa ndio wanachelewesha uwekezaji wa kiwanda na mimi nitasema mbele yake.
“Msizungumze na Aqual, achaneni nao zungumzeni moja kwa moja na Dangote mwenyewe, fungeni gesi hiyo ndani ya hizo kilomita 10 ifike hapa ili wawe wanaamua kutumia gesi ama makaa ya mawe,” alisema Magufuli.
Alisema hata kwenye kuajiri madereva ni tatizo kubwa, magari yameletwa, madereva wapo Serikali imesema inataka kutengeneza ajira lakini kuna kampuni imetengezwa katikati ambayo inachukua hadi rushwa ili kupata ajira, wanatumia mbinu za hovyo.
“Wewe ni mtu mzuri lakini watu uliowaweka hapa sio watu wazuri inawezekana wanaokuwakilisha wakawa na matatizo, wasije wakawa wanatumiwa na watu wengine katika kuua biashara yako, kuwa mwangalifu na watu unaowaweka hapa,” alisema Magufuli.
“Dangote apewe eneo achimbe mwenyewe, ndani ya siku saba awe amepewa eneo hawa Tancol ni kampuni ya hovyo hawajazalisha chochote tunachezewa na watu wa hovyo, ikiwezekana vyombo vya dola viichunguze hii kampuni ,ikiwezekana wafukuzwe moja kwa moja hatuwezi kukaa na matapeli katika nchi hii tumetapeliwa vyakutosha, NDC hawanifurahishi sana, hawawezi kuwa wanaingia mikata na matapeli,”alisema.
Kwa upande wake Bilionea Alhaji Aliko Dangote alisema kuwa kiwanda hicho kinatarajia kuzalisa tani milioni tatu kwa mwaka, ni kiwanda kikubwa kuliko vyote Afrika Mashariki.