29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

JOYCE MUJURU ANACHEKA, GRACE MUGABE AMENUNA

HARARE, ZIMBABWE

NOVEMBA 15, mwaka huu, ilikuwa siku ngumu kwa mawaziri wote wa taifa la Zimbabwe. Ilikuwa ngumu pia kwa wananchi wa nchi hiyo baada ya kushuhudia jeshi lao likiwazuia kufanya shughuli ndani ya saa 24.

Jeshi hilo lilisababisha baadhi ya watu kugoma kutoka nje ya nyumba zao wakihofia usalama wa maisha yao. Ilikuwa siku ngumu pia kwa mke wa Rais Robert Mugabe, Grace Mugabe, ambaye alijikuta kwenye taharuki baada ya jeshi la nchi hiyo, likiongozwa na Jenerali Constantine Chiwenga, kuzingira nyumba ya Rais Robert Mugabe.

Jeshi hilo lilidhibiti barabara zote za Mtaa wa Samora Machel ambazo zinaingia moja kwa moja hadi kwenye makazi ya Rais Mugabe.

Uamuzi wa kuzingira nyumba ya Rais Mugabe ulikuja siku chache baada ya Jenerali Chiwenga kuwaonya wanasiasa wa chama tawala cha ZANU-PF kutokana na mgogoro wa ndani uliokuwa ukiendelea na kusababishwa na kundi la G40 (Generation 40) au kundi la kizazi kipya.

Kundi la G40 lilikuwa linamuunga mkono Grace Mugabe kuwa mrithi wa kiti cha urais nchini humo. Hata hivyo, ndoto hizo hazikutimia.

Kuanzia usiku wa Novemba 14 na alfajiri ya Novemba 15, Jeshi la Zimbabwe lilikuwa limemaliza kudhibiti kila eneo muhimu ili kuweka mambo sawa.

Taarifa ya vyombo vya habari nchini Zimbabwe zilieleza kuwa, palikuwa na milio ya risasi na sauti za mabomu, lakini Jeshi hilo lilikanusha na kudai halifanyi mapinduzi, badala yake linawasaka wahalifu waliomzunguka Rais Robert Mugabe.

Hekaheka hizo zilishuhudia kukamatwa kwa Waziri wa Fedha wa Zimbabwe, Ignatius Chombo na Jeshi la nchi hiyo na walinzi watatu wa waziri huyo walioua. Nalo gazeti la NewsDay toleo la Novemba 15 liliripoti kuwa, Jeshi hilo pia lilimtembelea nyumbani kwake Profesa Jonathan Moyo ambaye ni waziri wa elimu ya juu na kumkamata.

Baadhi ya mawaziri waliripotiwa kutoroka, wakiwamo Saviour Kasukuwere na Makamu wa Rais Phelekezela Mphoko, aliyedaiwa kukimbilia Afrika Kusini. Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje, Walter Mzembi, amekwenda Zambia kukutana na Rais Edgar Lungu kwaajili ya kupata ushauri.

Taarifa zaidi zinasema kuwa, kiongozi wa Umoja wa Vijana wa chama cha ZANU-PF, Kudzanai Chipanga, ambaye aliitisha mkutano na vyombo vya habari kulipinga Jeshi la nchi hiyo, alikamatwa na Polisi akiwa nyumbani kwake mjini Harare.

Viongozi watatu wa kundi la G40 linalofanya kazi ndani ya chama cha ZANU-PF na kusababisha migogoro waliripotiwa kukamatwa na Jeshi. G40 ndilo kundi lililosababisha kufukuzwa Makamu wa Rais, Emmerson Mnangagwa. Pia wanajeshi waliulinda Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Robert Mugabe.

Jeshi hilo lilidhibiti Barabara ya Samora Machel na barabara ya Mtaa wa Sam Nujoma ambayo inakwenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Robert Mugabe, maarufu kwa jina la Munhu Mutapa.

Ikumbukwe Mkutano Mkuu wa Chama cha ZANU-PF ulitarajiwa kufanyika mwezi ujao, ambapo pamoja na mengine, ungetumika kumchagua Makamu mpya wa rais, huku Grace Mugabe akiwa na matumiani kuwa angekabidhiwa wadhifa huo.

WAHUSIKA WA MGOGORO WA ZIMBABWE

Grace Mugabe ni mhusika nambari moja. Ni mke wa pili wa Robert Mugabe, baada ya mkewe wa kwanza, Sally kufariki kwa ugonjwa wa saratani. Anadaiwa kuwa na kiu sana ya maisha ya kifahari na vitu vya thamani. Pia amekuwa akiendesha juhudi za kujitajirisha na kujilimbikizia mamlaka.

Kama mmoja wa watu walio karibu sana na Rais, Grace amewekewa vikwazo na EU na Marekani sawa na mumewe. Maneno yake ya wiki iliyopita alimweleza mpinzani wake, Makamu wa Rais Emmerson Mnangagwa, kama “nyoka” ambaye “lazima agongwe kichwani”. Siku iliyofuata, Rais Mugabe alimfuta kazi Mnangagwa.

Mhusika nambari mbili ni Emmerson Mnangagwa, ambaye kabla ya ushawishi wa Grace Mugabe kuzidi ndani ya ZANU-PFi, alikuwa akitazamwa na wengi kama mrithi mtarajiwa wa Rais Mugabe.

Mhusika nambari tatu ni Jenerali Constantino Chiwenga, mwenye umri wa miaka 61. Ni mshirika wa karibu wa Mnangagwa na ameongoza majeshi ya Zimbabwe tangu 1994.

Jenerali Chiwenga alikuwa kwenye vita ya uhuru na alipokea mafunzo akiwa na Jeshi la Ukombozi wa Zimbabwe nchini Msumbiji.

Mwaka 2002, Chiwenga na washirika wengine 18 wa karibu wa Mugabe waliwekewa vikwazo na Umoja wa Ulaya, Marekani na New Zealand, ikiwa ni pamoja na marufuku ya usafiri na kuzuiliwa kwa mali yao. Vikwazo hivyo vimekuwa vikiongezwa muda wake.

Mwaka 2003, alipandishwa cheo na kufanywa kamanda jenerali wa Majeshi ya Ulinzi ya Zimbabwe.  Aliwashangaza raia wengi wa Zimbabwe Jumatatu alipotoa onyo hadharani kwa wale waliokuwa wanawatimua wengine waliohusika vita vya ukombozi dhidi ya wakoloni katika chama tawala cha Zanu-PF, akisema jeshi lingeingilia kati.

G40 YA GRACE NA G4 YA JIANG

Kundi la G40 linajumuisha wanasiasa wengi ambao kwa namna moja au nyingine wanakubalika na mke wa Rais Mugabe, Grace Mugabe.

Lengo la kuunda kundi hilo lililikuwa kusaka madaraka, ikiwamo kuwa warithi wa Rais Mugabe. Kulikuwa na wanasiasa kama Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa chama cha ZANU-PF, Kudzanai Chipanga, Mhariri wa zamani wa gazeti la serikali The Herald , Edmund Kudzayi, Waziri wa Elimu ya Juu, Profesa Jonathan Moyo, Mhariri wa gazeti la Chronicle, Mduduzi Mathuthu, Waziri wa Fedha Ignatius Chombo na wengineo.

Kwa muda mrefu Grace Mugabe alijitayarisha kushika madaraka ya juu nchini Zimbabwe. Alikuwa tayari kuwadhalilisha wanasiasa wenzake ndani ya ZANU-PF na wale wote waliokuwa wakijaribu kuweka kikwazo cha yeye kupanda ngazi.

Miongoni mwao walioshughulikiwa na Grace ni Joyce Mujuru, ambaye alitimuliwa umakamu wa rais, kabla ya zahama hiyo kumkuta Emmerson Mnangagwa.

Kuanguka kwa Grace Mugabe na kundi lake la G40 kunafananishwa na kile kilichomtokea Jiang Qing, mke wa rais wa zamani wa China, Mao Tse Tung wa China. Malengo ya G40 ya Zimbabwe na G4 ya China; kushika madaraka ya juu, ikiwamo urais wa nchi zao.

Kile alichokifanya Grace Mugabe kwa Emmerson Mnangagwa na Joyce Mujuru kinafanana pia na kitendo cha Jiang Qing, mke wa Mao Tse Tung kwa mwanasiasa na rais wa zamani Deng Xiaoping huko China. Deng Xiaoping baada ya kufukuzwa serikalini, alirudi madarakani muda mchache baadaye na kubadili kabisa sera za Mao na kuipeleka China kwenye mwelekeo mwingine wa kiuchumi. Je, Mnangagwa atakuwa Den wa Zimbabwe?

RHODESIA YA KUSINI

Zimbabwe ilifahamika kwa jina la Rhodesia ya Kusini katika kipindi cha ukoloni. Ilipata Uhuru wake mwaka 1980, baada ya kuwa kwenye utawala wa Kilowezi kwa miaka mingi. Wapigania Uhuru wa nchi hiyo chini ya chama cha ZANU PF kama vile Joshua Nkomo, Robert Mugabe na kadhalika, hakika walifanya kazi kubwa. Zimbabwe ni miongoni mwa nchi nyingi za Afrika zilizopata Uhuru kwa mtutu wa bunduki.

Tangu ilipopata uhuru na kuwa chini ya utawala wa Robert Mugabe na chama cha ZANU PF, Zimbabwe imepita katika vipindi vya neema na taabu. Mugabe ni mwanasiasa mwenye misimamo mikali, hasa dhidi ya siasa za nchi za Kibeberu za Magharibi. Ametaifisha mashamba makubwa yanayomilikiwa na Wazungu nk. Zimbabwe ni nchi iliyokumbwa na dhoruba na adhabu za vikwazo vya kiuchumi kwa miaka mingi sasa.

Mwaka 2008, Zimbabwe iliingia kwenye uchaguzi mkuu wenye ushindani wa kisiasa kati ya chama Tawala cha ZANU PF cha Robert Mugabe dhidi ya Morgan Tsvangirai wa chama Upinzani cha MDC-T. Uchaguzi ulisababisha vurugu za kisiasa zilisobabisha kuundwa kwa serikali ya Mseto.

Miaka michache iliyopita, Chama cha ZANU PF kilipata msukosuko baada ya Rais Mugabe kumwondoa madarakani kada na mwanasiasa shupavu, mwanamama Joyce Mujuru, aliyekuwa makamu wa rais wa nchi kwa madai ya kutaka kuipindua serikali yake. Pengine Mujuru anaweza kutajwa kuwa hakuwa na nguvu kubwa za kutosha kuitikisa nchi wala Mugabe mwenyewe.

Hivi karibuni Rais Mugabe alimfuta kazi makamu wa Rais wa nchi hiyo, Emerson Mnangwaga na viongozi kadhaa wa ZANU PF, hali iliyosababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama Tawala cha ZANU PF na ndani ya Serikali ya Rais Mugabe.

Emerson Mnangwaga ni mwanasiasa mwenye ushawishi mkubwa mno ndani ya chama cha ZANU PF na serikalini pamoja na ndani ya vyombo vya dola.

EMMERSON MNANGAGWA NI NANI?

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya Zimbabwe, vimekariri msimamo wa chama cha Zanu-PF kuwa Emmerson Mnangagwa ndiye chaguo lao la kuwa rais wa mpito. Aidha, uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwakani utaahirishwa ili kutoa nafasi kwa viongozi kujiandaa kabla ya kuitisha tena.

Mnangagwa, mwenye umri wa miaka 75, alifukuzwa katika wadhifa wake wa umakamu wa rais kutokana na kile serikali ilichosema kuwa kutokuwa mtiifu kwa Rais Robert Mugabe.

Kufukuzwa kwake kulionekana kama njia ya kumwezesha mke wa Rais Mugabe, Grace Mugabe, kufuata nyayo za mumewe na kuwa kiongozi wa Zimbabwe. Awali alikuwa ametoa wito kwa mumewe kumfukuza makamu huyo.

Mnangagwa amewahi kuwa Mkurugenzi wa Ujasusi wa Zimbabwe. Baada ya kupokea mafunzo ya kijeshi Misri na China, alisaidia kuelekeza vita ya ukombozi kabla ya uhuru 1980. Alifungwa jela na kuteswa. Amekuwa kwenye serikali tangu uhuru.

FURAHA YA JOYCE MUJURU

Pengine mtu mwenye furaha zaidi kwa kadhia iliyotokea nchini Zimbabwe na kupeperusha matumaini ya Grace Mugabe kumrithi mumewe ni Makamu wa zamani wa rais, Joyce Mujuru. Mujuru alifukuzwa uongozini kwa fitina za Grace, pengine huko aliko anacheka sana, wakati Grace Mugabe akihangaika kutafuta pa kuficha sura.

GRACE MUGABE NI NANI?

MAPINDUZI ya kijeshi yaliyofanyika nchini Zimbabwe chini ya Jenerali Constantine Chiwenga hayawezi kuelezewa bila kutaja jina la Grace Mugabe. Huyu ni mke wa Rais Robert Mugabe tangu mwaka 1996. Kabla ya kuwa mke wa rais na baadaye ‘First Lady’, Grace alikuwa Katibu Muhtasi wa Rais Mugabe. Swali kuu hapa, Grace Mugabe ni nani?

Jina lake kamili ni Grace Ntombizodwa Marufu ‘Mugabe’. Kwa sasa ana umri wa miaka 52. Alizaliwa Julai 23, mwaka 1965, katika Kijiji cha Benoni, huko Afrika Kusini. Baba yake ni Johnson Marufu na mama ni Idah Marufu.

Kama walivyo raia wengi wa Zimbabwe, Marufu na mkewe walikwenda nchini Afrika Kusini kutafuta maisha ili kujikwamua kiuchumi. Wazazi wake walihamia huko kutafuta kazi katika kipindi cha utawala wa makaburu nchini humo, huku Zimbabwe ikitawaliwa na walowezi, iliaminika Afrika Kusini zipo fursa nyingi kuliko mataifa mengine ya Kiafrika.

Grace Mugabe ni mtoto wa mwisho kati ya watano wa Johnson Marufu na Idah Marufu, waliokulia katika Kijiji cha Sadza, kilichopo katika Jimbo la Mashonaland, kilomita 150 kutoka jiji la Harare.

ELIMU

Familia ya Mafuru ilirudi nchini Zimbabwe mwaka 1970, kipindi ambacho Grace alikuwa na miaka mitano. Familia hiyo iliweka makazi yao katika Jimbo la Mashonaland, ambako Grace alianzia safari yake ya maisha na elimu. Alisoma katika Shule ya Mtakatifu Francis wa Assisi ya Kanisa Katoliki iliyopo Madondo katika kipindi cha ukoloni. Baadaye alijiunga na kidato cha tano katika Shule ya Kriste Mambo (Kriste Mambo High School) iliyopo mji wa Rusape, katika Jimbo la Manicaland. Mara baada ya kuhitimu kidato cha sita, alijiunga na Chuo cha Kikristo cha Kusini (Christian College of Southern Africa), ambako alisomea masomo ya ukatibu muhtasi (mhazili).

Mwaka 2007 alijiunga na Chuo Kikuu cha Renmin cha China kusomea shahada ya lugha ya Kichina. Alihitimu shahada hiyo mwaka 2011. Mwaka 2014 alitunukiwa shahada ya udaktari wa falsafa katika fani ya saikolojia (PhD) na Chuo Kikuu cha Zimbabwe. Wakati akitunukiwa udaktari huo, Mkuu wa Chuo hicho alikuwa mumewe, Robert Mugabe. Anadaiwa kusomea kwa muda wa miezi minne kisha kutunukiwa udaktari wa falsafa.

Minong’ono juu ya shahada hiyo ilisambaa nchini kote Zimbabwe, ambapo ilidaiwa hakusoma somo lolote katika tasnifu yake (Thesis). Jambo hilo linafananishwa na Shahada ya Udaktari wa Falsafa ya Elena Ceausescu, mke wa Rais Nicolae Ceausescu, aliyetunukiwa shahada yenye utata ya udaktari wa falsafa.

KATIBU MUHTASI WA RAIS HADI NDOA

Grace Mugabe alifanya kazi ya Ukatibu Muhtasi kwenye Ikulu ya Robert Mugabe. Akiwa na miaka 20 aliolewa na rubani wa ndege za jeshi, Stanley Goreraza na kufanikiwa kupata mtoto mmoja aitwaye Russell. Katika kipindi hicho, Robert Mugabe alikuwa kwenye ndoa yake na Sally Hayfron, mwenye asili ya Ghana. Mwaka 1992 Sally Mugabe alifariki dunia kutokana na ugonjwa wa mapafu. Hata hivyo, kabla ya kifo hicho, alimruhusu Mugabe kuwa na mwanamke mwingine, ndipo alipoanza uhusiano wake na Grace mnamo mwaka 1988. Ndoa ya Mugabe na Grace ilishuhudia tofauti ya umri wa miaka 41 kati yao, ambapo sasa wamejaliwa kuwa na watoto watatu, Bona, Robert na Chatunga.

NDANI YA SIASA

Grace Mugabe aliibuka kuwa miongoni mwa wanasiasa wenye nguvu ndani ya chama cha ZANU-PF. Mwaka 2014 alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa chama cha ZANU-PF. Baadaye aliteuliwa kuwa mjumbe wa Kamati Kuu.

Tangu mwaka 2016 amekuwa akihusishwa na mpango wa kuwa rais wa Zimbabwe. Katika kutekeleza mkakati huo, alianzisha kundi la kizazi kipya cha siasa maarufu kama G40 (Generation 40). Kundi hilo lilijumuisha wanasiasa wanaomuunga mkono pamoja na wafuasi wake.

Grace Mugabe anahusika moja kwa moja kufukuzwa kazi Makamu wa Rais Joice Mujuru na baadaye Emmerson Mnangagwa kutokana na vita ya kuwania madaraka ya kumrithi Rais Mugabe. Mara zote Grace aliwatuhumuwa Mnangagwa na Mujuru kutokuwa watiifu na kupanga njama za kumpindua Mugabe.

VIKWAZO

Grace Mugabe ni miongoni mwa wanasiasa waandamizi wa chama tawala waliowekewa vikwazo vya kusafiri na Umoja wa Ulaya tangu mwaka 2002. Vikwazo hivyo vilihusisa maofisa 20 wa Zimbabwe, kabla ya kuongezeka wengine hadi kufika 51 sasa ambao hawaruhusiwi kutembelea nchi za Ulaya.

MATANUZI

Mwanamama huyo anatajwa kuwa mpenda matanuzi kwa kiasi kikubwa na mmiliki wa majengo mbalimbali katika nchi tofauti. Nyumba yake maarufu kama Gracelands alimuuzia marehemu Gaddafi. Pia anamiliki nyumba nyingine nchini Malaysia. Mwaka 2008 alitarajiwa kuhamia nchini Malaysia na familia yake, akihofia kuuawa. Anamiliki nyumba nyingine huko Hong Kong pamoja na biashara ya almasi. Anapendelea kusafiri kwenda miji ya Paris, London na Johannesburg kufanya manunuzi ya mavazi na vitu mbalimbali.

ANAKOWEZA KWENDA

Kutokana na hali iliyopo Zimbabwe, Grace Mugabe anadhaniwa anaweza kwenda kuishi katika nchi za Botswana, Dubai na Malaysia, ambako anamiliki mali mbalimbali pamoja na biashara, huku akiwa na uhusiano nazo mzuri.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles