25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

JE, TUDAI KATIBA MPYA AU TUJIANDAE NA UCHAGUZI WA MWAKA 2020?- 2

Na Ndahani Mwenda

SEHEMU ya kwanza ya makala haya tuliangalia nguvu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliyopewa na Katiba ya mwaka 1977. Naam, sasa tuingie katika sehemu ya pili na ya mwisho. Kama nilivyosema hapo awali Rais wa Tanzania amepewa mamlaka makubwa sana hivyo anaweza kufanya lolote. Sote mashahidi kuwa Rais Magufuli mwaka jana alipiga marufuku mikutano ya kisiasa kwa kigezo inachelewesha maendeleo.

Aidha, tumeona Jeshi la Polisi likidhibiti vyama vya siasa kwa kutumia amri ya Rais aliyoitoa mapema mwaka jana. Jeshi la Polisi hilo hilo haliwakamati CCM pale wanapofanya mikutano ya hadhara ila wapinzani tu ndio hukamatwa. Ni sawa na kusema Jeshi la Polisi, CCM na Serikali vinakabiliana na upinzani nchini baada ya kukabiliana kwa hoja na kwenye majukwaa ya kisiasa.

Mikutano ya kisiasa kwa vyama vyote nchini ipo kisheria, Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo marekebisho ya mwisho yalifanyika mwaka 2005, katika Ibara ya 3-(1) (2) imezungumzia juu ya uwepo na shughuli za vyama vya siasa.

Ibara hii ipo kwa mujibu wa Tangazo la Nchi yenye mfumo wa vyama vingi Sheria ya mwaka 1992 Ibara ya 5, Sheria Namba 1 Ibara ya 4, vyote vikisomwa kwa pamoja. Sasa kwa vifungu hivyo unakatazaje shughuli za vyama vya siasa? Sheria inaruhusu vyama kufanya shughuli za kisiasa, lakini wamekatazwa! Hivi toka lini mikutano ya siasa ikakwamisha maendeleo ya nchi?

Haingii akilini eti Jacob Zuma na Serikali yake ya ANC wawazuie akina Julius Malema wa Economic Freedom Fighters (EFF) na Mmusi Maimane wa Democratic Alliance (DA) wasiikosoe Serikali, eti wasubiri siku ya uchaguzi. Ni sawa na kumwambia mtu sasa baada ya mkewe kuzaa mtoto mmoja basi asilale tena na mkewe mpaka siku wakitaka kuzaa mtoto mwingine tena.

Rasimu ya Katiba ya Jaji Joseph Sinde Warioba, ilikuwa imesheheni mambo mengi mazuri, madaraka ya Rais pia yamepunguzwa, CCM na Serikali kwa kuona Katiba ile itawabana walitumia ushawishi wao kuhakikisha wanabadilisha sehemu kubwa ya mapendekezo na kuja na mengine kisha kuandika na Rais mstaafu Jakaya Kikwete alikabidhiwa pale uwanja wa Jamhuri Oktoba 08, 2014.

Licha ya juhudi hizo za Rais Dk. Jakaya Kikwete, hakumalizia suala la Katiba Mpya ambalo lilitafuna mabillioni ya walipa kodi, Kikwete alitakiwa ailete kwenye sanduku la kura ya maoni ambayo wananchi wangeikubali au kukataa.

Katiba Pendekezwa ilipaswa kupigiwa kura Aprili 30, 2015 na waliotakiwa kuandaa na kulisimamia zoezi hilo ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) waliamua kuliweka kando kwa hoja kwamba wanajiandaa na uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

Katiba Pendekezwa ilipingwa kuanzia ndani ya Bunge la Katiba (rejea kususa kwa Ukawa) na nje Bunge la Katiba. Nje ya Bunge la Katiba, ilipingwa na Jumuiya mbalimbali kama zile Jumuiya 11 za Kiislamu kama Baraza Kuu la Waislamu, Basuta, Shira, Haiyat Ulamaa, Jasuta na nyinginezo.

Jumuiya hizo zilidai Serikali imewapiga chenga juu ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, ambayo walitaka iendeshwe kwa fedha za umma. “Zipo Mahakama za makundi ya watu maalumu ambazo zinaendeshwa kwa pesa za Serikali ambazo ni kodi za Watanzania wote. Mfano Mahakama ni kama vile Mahakama ya Kazi, Ardhi na Mahakama ya Biashara. Kwanini Mahakama itakayotafsiri Sheria za Kiislamu iwe nongwa?” alihoji Makamu Mwenyekiti wa Haiy Atul-Ulamaa, Sheikh Abdallah Bawazir

Pia makundi mengine yalikuwa ni Jukwaa la Kikristo Tanzania (PCT), Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), hao wote walitoa misimamo yao juu ya hiyo Katiba Pendekezwa.

Askofu Dk. Tracius Ngalalekumtwa (Rais wa TEC), Askofu Dk. Alex Malasusa (CCT), wakiwakilisha Jumuiya za Kikristo walitoa taarifa ya kuwashawishi waumini wao wasiende kupiga kura kwenye hiyo Katiba Pendekezwa.

“Kanisa haliwezi kuunga mkono kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa kutokana na hali hii, hivyo basi Jukwaa linawataka waumini wake wote wajitokeze kwa wingi kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura na waisome Katiba inayopendekezwa na kushiriki kikamilifu vipindi vya elimu ya juu ya Katiba Inayopendekezwa na kisha wajitokeze kwa wingi kupiga kura ya hapana,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo ya Machi 12, 2015.

Serikali ya Awamu ya Nne kwa kuliona hili ilijibu mapigo ya maazimio ya makundi ya kidini. Waziri wa Mambo ya Ndani kipindi hicho, Mathias Chikawe, alizungumza na waandishi kuhusiana na mvutano huo ambapo alisema: “Kuanzia Aprili 20 mwaka huu (2015) taasisi zitakazoshindwa kuwasilisha taarifa za ukaguzi wa fedha za mwaka pamoja na kulipa ada zitachukuliwa hatua,” Waziri Chikawe alidai wangezishughulikia taasisi hizo kwa mujibu wa Sheria ya vyama vya kijamii aura ya 337.

Ukiachana na kushindwa kwa Serikali ya Awamu ya Nne, Serikali ya Awamu ya Tano nayo tumeshasema kuwa haina mpango na Katiba Mpya yenyewe imejikita kuleta huduma za jamii kwa wananchi, hayo yalisemwa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa hivi karibuni  Bungeni.

Akihutubia Bunge kwa mara ya kwanza Novemba 20, 2015 baada ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais John Magufuli, alilihakikishia Bunge kuwa watatekeleza suala la Katiba mpya.

“Napenda kuwahakikishia kuwa tunatambua na kutathmini kazi kubwa ya kizalendo iliyofanywa na wananchi walioshiriki hatua ya awali ya ukusanyaji wa maoni kuhusu Katiba Mpya, Tume ya marekebisho ya Katiba na Bunge la Katiba lilitupatia Katiba Inayopendekezwa. Tutatekeleza wajibu wetu kama ilivyoainishwa katika Sheria ya marekebisho ya Katiba,” alisema Rais Magufuli.

Serikali kwa ujumla wanadai kuwa mchakato wa Katiba Mpya ni gharama sana ilihali wanajenga barabara na kununua ndege kwa mapesa mengi tu. Kwa hiyo Rais anaona Katiba Mpya si muhimu. Hili linashangaza kwa sababu Katiba Mpya ni haki ya wananchi na si viongozi na haiwezi kuja hivi hivi bila kudai.

Katiba ya sasa Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi na Makamu wake wote ni wateule wa Rais kwa mujibu wa Ibara ya 74 (1)  (a) (b) na Ibara ndogo ya (2) ) halafu hapo hapo Ibara ya 74 (7) inasema Tume ya Uchaguzi itakuwa ni idara huru. Hivi idara huru, Mkuu wake anateuliwaje na mtu anayegombea urais?

Tunahitaji tume huru ambayo Mwenyekiti wa Tume, Makamu Mwenyekiti na Mkurugenzi wa Uchaguzi waombe kazi kupitia Mahakama Kuu ama Bunge, halafu Bunge liwahoji juu ya watakavyoendesha hiyo Tume, Bunge likiridhia basi wanaapishwa tayari kwa kazi.

Katiba iliyopo haiongelei ulazima wa haki ya kupata elimu.  Kwa mfano nchini Afrika Kusini, Korea Kusini na hata nchi zilizoendelea elimu ni haki ya msingi. Sote ni mashahidi kuwa watu wengi wanaachwa katika mlolongo wetu wa elimu yetu kwa sababu ya umasikini.

Ndani ya nchi hii tunashuhudia kituko kwamba mtu anaweza kusoma hadi kidato cha sita lakini ananyimwa mkopo wa kuendelea na masomo ya elimu ya juu. Mwaka wa masomo 2014/2015 zilitengwa shilingi bilioni 341 kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu na waombaji wapatao 99,000 walipata.

Mwaka wa masomo wa 2015/2016 zilitengwa shilingi billioni 450 na waombaji wenye vigezo wapatao 122,000 walipata lakini ghafla idadi ya wanafunzi kupata mkopo ikapungua mwaka wa masomo 2016/2017 waombaji walikuwa 48,000 lakini waliopata ni 25,000 tu.

Mwaka 2017/2018 Serikali ilitenga kiasi cha bilioni 147 tu wakati waombaji ni 67,737 na waliopata hawazidi 35,000 hadi sasa. Idadi kubwa ya wanafunzi wamekosa mikopo. Hii yote ni kwamba suala hili halijapewa uzito katika Katiba yetu.

Akihutubia katika mkutano wa kampeni Septemba 14, 2015 katika Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Magufuli ambaye ni Rais kwa sasa aliahidi kuwa hakuna mwanafunzi atakayekosa mkopo wa elimu ya juu, lakini leo ni vingine. Tusifanye mikopo hii kama msaada wakati ni haki ya kila Mtanzania.

Katiba Mpya ni muhimu kwa kipindi cha sasa, wananchi bila kujali itikadi zetu na tofauti zetu ni lazima tuungane kudai Katiba Mpya.  Katiba yetu ya sasa inakataza kuyapinga matokeo ya urais mara baada ya kutangazwa na Tume ya Uchaguzi, rejea Ibara ya 41(7).

Kenya, Ufaransa, Liberia na Benin lazima mgombea afikishe asilimia 51+ ya kura ndipo atatangazwa mshindi na hata akitangazwa mshindi kama ushindi wake una mashaka unaweza kwenda mahakamani. Hiyo ndiyo demokrasia.

E-mail: [email protected]/ Twitter: @ndahani_mwenda

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles