MKALI wa muziki wa kizazi kipya aliyekuwa akitumia lafudhi ya ulevi, John Walker, amefariki dunia jana asubuhi kwa ajali ya kugongwa na kitu kizito katika paji lake la uso.
Mmoja wa ndugu wa msanii huyo aliyekuwa katika kundi la Watukutu Family, alisema John Walker aligongwa na kitu kizito kwenye paji la uso alipokuwa gereji maeneo ya Sinza alipokuwa akitengeneza gari lake lakini kwa bahati mbaya mtungi wa gesi ulilipuka na moja ya kipande cha chuma chenye ncha kali kilimchoma kichwani ndipo akakimbizwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa matibabu lakini alifariki dunia.
Wakati familia ikiandaa taratibu za mazishi ya msanii huyo aliyejipatia umaarufu mkubwa kwa nyimbo zake za ‘Sophia’, ‘Baby girl’, ‘Mganga’ na nyingine nyingi, wasanii mbalimbali wamesikitishwa na kifo cha msanii huyo wakiwemo kundi la Wagosi wa Kaya.
Akizungumza jana mmoja wa wasanii ambaye anaunda kundi hilo, John Simba ‘Dr. John’ alisema kifo cha msanii huyo kimekuwa pigo sana kwenye tasnia ya muziki huo kwa sababu alikuwa kijana mwenye ndoto kubwa za kimaisha.
“Wagosi wa Kaya tumepoteza nguzo kubwa kwa kuwa msanii huyo aliwahi kufanyakazi nasi katika nyimbo zetu ukiwemo wimbo wa ‘Lidandasi’ na ‘Tutamtambuaje’ ambazo zinapatikana kwenye albamu yao ya ‘Ukweli mtupu’.
Naye rafiki wake wa karibu, Royi Erio, alisema wiki tatu zilizopita alikutana na msanii huyo jijini Dar es Salaam na akamueleza kuhusiana na mipango yake mikubwa katika maisha lakini hakuitimiza amefariki dunia.