28.2 C
Dar es Salaam
Thursday, October 17, 2024

Contact us: [email protected]

JKCI kuwafikishia wananchi wengi huduma za kibingwa

Na Mwandishi Wetu, Arusha

Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), imesema itahakikisha wananchi wengi wanafikiwa na huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kupitia program yake ya tiba mkoba ya Dk. Samia Suluhu Hasssan.

Hayo yamesemwa leo Oktoba 17,2024 jijini Arusha na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Dk. Peter Kisenge wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu kambi maalumu ya uchunguzi na matibabu ya moyo inayofanyika Arusha Lutheran Medical Center.

Dk. Kisenge amesema kufanyika kwa kambi hiyo kunatokana na kambi ya uchunguzi na matibabu ya magonjwa ya moyo iliyofanyika mwezi wa sita mwaka huu jijini Arusha.

Amesema wamerudi tena mkoani Arusha kufanya kambi ya uchunguzi na matibabu ya moyo ili kuwapima watu wenye matatizo ya moyo na kutoa elimu ya magonjwa yasiyoambukiza ambapo watu 200 sawa na asilimia 30 ya waliojiandikisha kwa siku mbili wamegundulika kuwa na magonjwa ya moyo.

“Kambi ya kwanza tuliyoifanya Arusha tuliona watu 1350 tuliowakuta na matatizo ambao ni watu wazima walikuwa asilimia 14 na watoto asilimia tisa, sasa hivi asilimia imekuwa 18 ni kubwa ukilinganisha na wakati ule hii inatokana na tunaowaona hivi sasa wengi wao ni wagonjwa na wakati ule tuliona wasio wagonjwa na wagonjwa”.

“Vitu vinavyosababisha magonjwa ya moyo ni pamoja na unywaji pombe kupitiliza, kutokula vyakula bora, kutokufanya mazoezi na uvutaji wa sigara hivyo ni vizuri wananchi wafanye mazoezi ili kupunguza kupata magonjwa yasiyoambukiza yakiwemo ya moyo”, amesema Dk. Kisenge.

Ameeleza kuwa sababu nyingine ya kwenda Arusha ni kutokana na kuwa mkoa wa utalii, hivyo wanaimarisha afya ya utalii kwa watalii, watatoa elimu kwa wataalamu wa afya waliopo katika hospitali za Mt. Meru, Arusha Lutheran Medical Centre na Arusha International Conference Centre (AICC) ili waweze kutoa huduma za kibingwa za matibabu ya moyo kwa wananchi wa mkoa huo.

Aidha amewasisitiza wananchi kujiunga na bima ya afya kwa wote pindi itakapoanza kwani gharama ya matibabu ya moyo ni kubwa lakini kama mtu akiwa na bima ya afya itampunguzia gharama ya kulipia matibabu hayo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Arusha Lutheran Medical Center Dk. Goodwill Kivuyo amewashukuru wataalamu wa JKCI kwa kufanya kambi ya matibabu ya moyo katika hospitali hiyo ambayo imewasaidia wananchi kupata huduma pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu wa afya wa hospitali hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles