27.6 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JK: Sihusiki na ufisadi TRA

jk*Asema hajawahi kuagiza mfanyabiashara yeyote asamehewe kulipa kodi
*Aikingia kifua familia yake, awashukia wanaomtuhumu

NA FREDY AZZAH, DAR ES SALAAM
RAIS mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete, amevunja ukimya na kusema hausiki yeye wala familia yake katika ukwepaji kodi kwa kutorosha makontena bandarini.

Pamoja na hali hiyo, amesema kuwa hajawahi katika utawala wake kuagiza mtu yeyote anayestahili kulipa kodi asilipe na wala haamini kwamba kuna mtu kwenye familia yake anaweza kufanya hivyo.

Kauli hiyo ya Rais Kikwete, imekuja siku chache baada ya Serikali ya awamu ya tano kuwasimamisha kazi watumishi 59 wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na 23 kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) na kuvunjwa kwa bodi ya mamlaka hiyo.

Baadhi ya watumishi hao wamefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutoa makontena 2,716 bandarini na kuisababishia hasara Serikali ya zaidi ya Sh bilioni 500.
Baadhi ya vyombo vya habari vimekuwa vikimuhusisha Rais mstaafu Kikwete na familia yake katika ukwepaji huo wa kodi.

Akizungumza na wananchi wa Jimbo la Chalinze mkoani Pwani jana baada ya kushiriki usafi kama ambavyo Rais Dk. John Magufuli aliagiza, Kikwete alisema: “Tusiondolewe kwenye mstari na maneno haya yasiyokuwa na kichwa wala miguu.

“Nataka kuwaambia wanapoteza wakati wao bure, nimeongeza mapato kutoka Sh bilioni 177 mpaka bilioni 900 wakati naondoka, ni matokeo ya jitihada za kuimarisha mifumo ya ukusanyaji wa mapato na kubana mianya ya ukwepaji wa kodi.

“Lakini wale wanaokwepa kodi hawataacha, wataendelea wakati wote kupambana na ndiyo maana mapambano haya lazima yaendelee, na ndiyo maana tunamuunga mkono rais kuendeleza mapambano haya.

“Sijawahi wakati wangu kuagiza mtu yeyote asamehewe kontena lake lisilipiwe kodi, ningefanya biashara hiyo isingefika bilioni 900.

“Wamekaa wanachonga tu, wanasumbuka bure, wasinilaumu miye, Magufuli ndiye kawashinda, mgombea mzuri, wananchi wamemkubali, sasa wana kisa na miye, lakini afadhali miye, nishambulieni miye mwacheni Magufuli atimize wajibu wake.
“Mimi nishambulieni, mwacheni Magufuli afanye kazi yake na mkinishambulia mie mnapoteza wakati kwa sababu mimi sigombei tena, mnapoteza nguvu zenu bure,” alisema.
Alisema urais ulikuwa wake, hakuwa na ubia na mke wake, familia yake, wala mtu yeyote, kwamba alichaguliwa yeye na akatimiza wajibu wake.

“Wanasema na familia yangu nao wanaagiza tu huko watu wanaachiwa kodi, nikashangaa, mie mwenyewe rais sikuagiza, siamini kama mke wangu anaweza kufanya au mwanangu Ridhiwani anaweza akafanya na watu wakamsikiliza.

“Nasema lakini ni siasa za maji taka, lakini ni siasa za watu walioshindwa, sasa hawana tena la kusema basi huvambanya, kuzoza, wanaangaika tu wanatapatapa, nataka kuwahakikisha Watanzania sijawahi kutoa agizo kwa mtu yeyote anayepaswa kulipa kodi asilipe.

“Hayo wanayosema wanastarehesha baraza, wanapoteza wakati wao, mmoja anasema JK hachoi, kwani nimechomeka nini? Sina nilichochomeka kwahiyo sina cha kuchomoa,” alisema Kikwete.
Baada ya kashfa ya makontena bandarini kuanza kuibuliwa, baadhi ya watu kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari walianza kuhoji kwanini Serikali ya awamu ya nne ilishindwa kuchukua hatua na hata kudhibiti utoroshwaji wa makontena bila kulipiwa kodi.

Kutokana na mijadala hiyo, baadhi ya watu na vyombo hivyo, walidai kuwa watu hao walikuwa wanakwepa kodi kiurahisi kutokana na kuwa na mkono wa Kikwete na familia yake.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alifanya ziara ya kushtukiza katika bandari ya Dar es Salaam Novemba 27, mwaka huu na kubaini kuwapo kwa makontena 329 yaliyotolewa bila kulipiwa kodi.

Ziara kama hiyo ya kushtukiza aliifanya tena Desemba 4, mwaka huu na kubaini kuwapo kwa makontena 2,387 yaliyotolewa bandarini na kupelekwa katika bandari kavu (ICD), kisha yakapelekwa kwa wateja bila kulipiwa kodi.

“Ziara yangu ilinipitisha hatua zote za upitishaji mizigo ambazo pia kwa mujibu wa taarifa ya uchunguzi wa ndani wa tarehe 30 Julai, 2015 TPA iligundua kuwepo kwa mianya mingi ya ukwepaji wa kodi, ikiwamo na makontena 2,387 yaliyopitishwa kati ya Machi na Septemba 2014 kinyume cha taratibu,” alisema Majaliwa hivi karibuni alipotangaza kuvunjwa kwa bodi ya TPA.

Kutokana na upotevu wa makontena 329, maofisa 36 wa TRA na TPA, akiwamo Kamishna wa TRA, Rished Bade, walisimamishwa kazi na tayari baadhi yao wamefikishwa mahakamani.

Kasi hiyo ya Rais Magufuli, iliendelea hivi karibuni ambapo panga lake lilirudi TPA, na kufyeka vigogo 23 ikiwa ni pamoja na kuvunja bodi ya mamlaka hiyo iliyokuwa na wajumbe wanane.

Gazeti moja la kila wiki (Si MTANZANIA), liliripoti jana kuwa Rais mstaafu Jakaya Kikwete, ndiye chanzo cha mwendelezo wa ufisadi wa kutisha katika TRA na TPA na kudai kwamba majalada ya siri ya ufisadi yaliwasilishwa ofisini kwake, lakini hakuna hatua madhubuti zilizochukuliwa.

Pamoja na kupelekewa vielelezo vya wazi vikitaja wahusika kwa majina kutokana na uchunguzi uliofanywa na vyombo vya dola, hatua hiyo ilitajwa kuwa iliwahi kuwavunja moyo maofisa waadilifu wa juu wa vyombo vya dola, ambao iliwabidi wasubiri ujio wa rais mpya wa awamu ya tano ili aweze kufanya kazi iliyofumbiwa macho na Rais Kikwete.
Gazeti jingine la kila wiki katika toleo lake la juzi liliripoti hatua ya kuwapo kwa taarifa kwamba familia hiyo ya Rais mstaafu Kikwete, imekuwa ikizibeba kampuni zilizokwepa kodi ikiwamo ile iliyotangaza kufilisika ya Home Shopping Centre.

Rais Magufuli, akizungumza na wafanyabiashara Ikulu wiki iliyopita, aligusia kampuni inayotumiwa na wafanyabiashara kukwepa kodi. Ingawa hakuitaja kwa jina, wafuatiliaji wa mambo wanasema mlengwa ni Home Shopping Centre.

Katika mkutano na wafanyabiashara uliofanyika wiki iliyopita Ikulu, Dar es Salaam, Rais Magufuli alisema: “Nafahamu, katika mchezo huo wa kukwepa kodi, baadhi ya wafanyabiashara wadogo hutakiwa kukusanya fedha na kumpatia mtu mmoja fulani ili huyo ndiye akawakombolee mizigo yao bandarini.

“Kutokana na hali hiyo, ninatoa siku saba kwa wale waliokwepa kodi kulipa haraka na wasipofanya hivyo watashtakiwa kwa mujibu wa sheria.”

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles