24.5 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

JK, JMP kuna kitu

kikwete1Na Agatha Charles

KWA mara nyingine tena Rais Mstaafu wa awamu wa nne, Jakaya Kikwete jana alikutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam na kufanya naye mazungumzo ambayo hata hivyo yamefanywa kuwa siri.

Hii ni mara ya tatu kwa Kikwete kumtembelea Rais Magufuli Ikulu tangu alipomkabidhi ofisi hiyo Novemba mwaka jana.

Licha ya mazungumzo hayo kufanywa kuwa siri,  katika picha zilizotumwa kwenye vyombo vya habari na Kitengo cha Mawasiliano Ikulu ziliwaonyesha wawili hao wakizungumza na kufurahia jambo fulani pamoja.

Ingawa haijajulikana kilichowakutanisha viongozi hao kwa sasa, lakini Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho kwa sasa Mwenyekiti wake ni Kikwete kinatarajia kukabidhi nafasi hiyo ya uongozi kwa Rais Magufuli kati ya mwezi Juni au Julai.

Si hilo tu kukutana kwa viongozi hao kumekuja wakati ambako mwenendo wa utendaji kazi pamoja kauli za Rais Magufuli zimekuwa zikitafsiriwa na baadhi ya watu kwamba huenda wawili hao wanatofautiana katika mambo mengi ya kiutendaji.

Jana baadhi ya magazeti yalimkariri Rais Magufuli katika mkutano wa Mashauriano wa Bodi ya Makandarasi akitamka maneno mazito kwamba kiti chake cha urais hajapewa na mtu yeyote bali kimetoka kwa Mungu hivyo yupo tayari kutoa sadaka mwili wake kwa ajili ya watanzania wengi ambao ni maskini.

Zaidi Rais Magufuli alikwenda mbali zaidi akituma ujumbe mzito dhidi ya wala rushwa na watu wanaodhulumu Taifa akisema ni mara kumi akachunge hata ndege, kuliko awe Rais halafu anavumilia uozo unaofanyika.

Akisisitiza katika hilo alisema ataendelea na vita aliyoianzisha ya kuwashughulikia kikamilifu watu hao wanaodhulumu Taifa na zaidi akiwanyooshea vidole wale aliowaita wazee wenzake kwamba wameharibu Taifa hili.

Kauli hizo za Magufuli tayari zimeleta mjadala mkubwa huku baadhi ya watu wakiamini kuwa mbali na kufikisha salamu kwa watu wanaohujumu Taifa lakini pia alituma ujumbe wa kwa watangulizi wake.

Awali Kikwete alimtembelea Rais Magufuli Januari 6, mwaka huu ambapo pamoja na mambo mengine alimtakia kheri ya mwaka mpya na kumpongeza kwa uongozi wake mzuri.

Mwezi huo huo pia Rais Magufuli alikutana na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba.

Safari nyingine iliyowakutanisha Kikwete na Magufuli Ikulu ni Februari mwaka huu ambapo rais huyo mstaafu alimtembea Rais Magufuli na kufanya naye tena mazungumzo ambayo yalielezwa kuwa ni ya siri.

Pamoja na kwamba upo uwezekano wa Rais Magufuli kukutana na viongozi hao wastaafu pasipo chombo chochote cha habari kufahamu, lakini kumbukumbu zinaonyesha kuwa mbali na Kikwete, Rais Magufuli pia alikutana na Mkapa mwezi huo huo wa Februari.

Kwa kumbukumbu zilizopo hadharani hadi kufikia jana katika kundi la viongozi wastaafu Kikwete ndiye anayeongoza kukutana na Rais Magufuli na mara zote wawili hao wanapokutana maneno na hisia huwa ni nyingi miongoni mwa wafuatiliaji wa mambo nchini.

Wakati Kikwete na Magufuli walipokutana Februari baadhi ya wasomi, wachambuzi na wafuatiliaji wa mambo nchini walijenga hisia kwamba huenda Rais huyo mstaafu alikwenda Ikulu kutuliza upepo uliokuwa unavuma vibaya dhidi ya watendaji waliokuwa wakitumbuliwa ambao kwa njia moja ama nyingine walikuwa ni wateule wake.

MTANZANIA Jumamosi jana lilimtafuta Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Gerson Msigwa ili kufahamu kilichozungumzwa baina ya viongozi hao wawili alisema mazungumzo yaliwahusu wao wenyewe.

“Walizungumza wao wawili wenyewe, sisi tumeambulia picha tukaona tu‘share’ na ninyi wenzetu,” alisema kwa kifupi Msigwa.

Itakumbukwa kuwa mtumishi wa serikali wa mwisho kutumbuliwa na Rais Magufuli hadi sasa ni aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na Mbunge wa Misungwi, Charles Kitwanga ambaye nafasi yake ilitenguliwa kutokana na madai ya ulevi.

Kitwanga aliondolewa katika Baraza la Mawaziri Mei 20, mwaka huu baada ya kudaiwa kusimama bungeni kujibu swali la mbunge akiwa amelewa.

Tangu aingie madarakani Rais Magufuli amekuwa akipambana na uzembe pamoja na kuziba mianya ya matumizi mabaya ya fedha za umma huku akiweka wazi namna nchi ilivyofika pabaya kutokana na ufisadi, watumishi hewa, wakwepa kodi na mambo mengine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles