RAIS Jakaya Kikwete, amezua taharuki baada ya kutaja idadi kubwa ya wapiga kura waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kuliko waliotajwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Akizungumza mjini Dodoma jana wakati wa kilele cha sherehe za mbio za Mwenge wa Uhuru na maadhimisho ya Kumbukumbu ya Kifo cha Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Rais Kikwete alisema Watanzania wanaotarajia kupiga kura kwa upande wa Tanzania Bara ni milioni 28 na kwa upande wa Zanzibar ni zaidi ya laki
tano.
Takwimu zilizotajwa na Rais Kikwete kwa upande wa Tanzania Bara, zinatofautiana na takwimu zilizotolewa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Ramadhani Kailima ambaye mwanzoni mwa wiki alisema Watanzania walioandikishwa katika daftari hilo ni milioni 22,751,292.
Kwa upande wa Zanzibar, alisema walioandikishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ni 503,193.
Tofauti ya takwimu hizo za Rais Kikwete zilionekana kuzua taharuki na kuzua mjadala. Miongoni
mwa walioonyesha kushtushwa na takwimu hizo ni Mwenyekiti Mwenza wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Freeman Mbowe ambaye alilazimika kuzungumzia suala hilo alipokuwa wilayani Biharamlo, Mkoa wa Kagera.
Katika mazungumzo yake akiwa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Masumbwe, Jimbo la Mbogwe, Mbowe alisema.
“Leo, Rais Kikwete amezungumza na taifa, kwa niaba ya Ukawa, naomba nimjibu kwa sababu amekuwa si rais wa nchi bali mpiga debe wa Magufuli (Dk. John Magufuli, mgombea urais wa CCM).
Kwa hiyo, namjibu kama mpiga debe wa CCM na Magufuli.
“Rais Kikwete amelitangazia taifa, kwamba watu waliojiandikisha kupiga kura ni milioni 28, lakini tume imesema waliojiandikisha ni milioni 23.
“Tunamuuliza Kikwete, hao watu milioni sita walioongezeka kawapata wapi na hizo kura anapeleka wapi?,” alihoji Mbowe.
“Rais Kikwete amesema wananchi wakipiga kura waondoke vituoni na kwenda nyumbani na wasiofanya hivyo, watashughulikiwa na vyombo vya dola.
“Nchi inaongozwa na sheria na Katiba si mapenzi ya Kikwete wala mtu yeyote.. Kama Kikwete amezoea kuvunja Katiba ya CCM, Watanzania hatutamruhusu avunje Katiba ya nchi kwani Sheria ya Uchaguzi inasema siku ya kura ukishapiga kura, watu wasikae chini ya mita 200 kutoka kituoni,” alisema Mbowe na kuongeza.
“Sisi tunasema uchaguzi ni tukio la kitaifa na ni maisha yetu sote, wananchi wana haki ya kushiriki hatua zote tangu kampeni, kupiga kura, kuhesabu na kusherehekea matokeo.
“Sheria inasema mita 200 kukaa ruksa, kwa sababu wanapanga kuiba kura, kuingiza kura feki wanataka Watanzania mkimbie kituo wakati kuna kura zetu, nasema tarehe 25 ni siku ya kihistoria, tunaenda kubadili historia.
“Piga kura, hesabu mita 200 weka kambi mpango ndio huo hakuna woga,” alisema Mbowe.
IKULU YATOA UFAFANUZI
Pamoja na malalamiko hayo, muda mfupi baada ya Rais Kikwete kuyasema hayo, Ikulu ilitoa ufafanuzi kuhusu takwimu ya idadi ya wapiga kura.
Katika taarifa hiyo iliyotolewa na Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premi Kibanga, Ikulu imesema takwimu sahihi za wapiga kura ni zile zilizotolewa na NEC.
“Taarifa kwa vyombo vya habari, ndugu wahariri. Kilele cha mbio za mwenge wa uhuru, kumbukumbu ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na wiki ya vijana kitaifa, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete katika hotuba yake
amezungumzia idadi ya watu waliojiandikisha
kupiga kura.
“Kwa uhakiki ni kuwa, wapiga kura ni 22,751, 292 kwa upande wa Bara na 503,193 wa Zanzibar na hii ndiyo idadi kamili ambayo imo kwenye hotuba ya mheshimiwa rais na hii ndiyo idadi kamili kama ilivyotolewa na Tume ya Uchaguzi Tanzania, asanteni,” alisema Kibanga katika taarifa yake hiyo.
Wakati hayo yakiendelea, awali Rais Kikwete pia aliwataka wananchi kuwakataa wagombea wanaoomba kura kwa kutumia udini kwa kuwa uongozi wa nchi hautolewi kwa madhehebu.
Alisema kipindi hiki cha uchaguzi ndicho kipindi cha kuenzi wosia wa Mwalimu Nyerere kuhusu kiongozi anayefaa kuliongoza Taifa hili hasa katika hotuba yake aliyoitoa Dar es Salaam mwaka 1995.
“Wapo wagombea wanaoomba kuchaguliwa kuwa wao ni wa dhehebu au dini fulani, hatugawani uongozi kwa madhehebu, ikifika mahali watu wanataka uongozi kwa madhehebu au dini ni hatari, kipimo cha uongozi kinakuwa
siyo uwezo tena.
“Hayati Baba wa Taifa alikuwa ni mwalimu, shujaa na alama ya Taifa letu, Nyerere ni kipimo cha uongozi bora katika nchi yetu, bahati nzuri leo tunakumbuka kifo chake siku 10 kabla ya Uchaguzi Mkuu, ni wakati muafaka wa kutafakari uongozi wa taifa letu,” alisema.
“Mimi namaliza muda wangu, lakini baada ya Oktoba 25 Tanzania inakuwa na sura yangu, kama niliongoza vibaya inakuwa ni sura yangu pamoja na viongozi wa chini yangu wakiwamo mawaziri, wabunge na madiwani.
“Hotuba ya Mwalimu ya mwaka 1995 alihimiza umuhimu wa viongozi watakaojenga umoja, waadilifu, watakaodumisha muungano ikiwamo udugu wa kuishi pamoja bila kujali tofauti zetu za dini,” alisema.
Alisema Mwalimu aliwataka Watanzania kuwaogopa kama ukoma wanaotaka kwenda Ikulu kwa kutumia
uzanzibar na utanganyika wao, ubaguzi wa rangi au rushwa.
“Naamini hadi hapa kampeni za uchaguzi zilipofikia wananchi wameshawasikiliza wagombea na kuona nani anawafaa na nani hawafai,” alisema.
Alisema siku ya uchaguzi ikifika wananchi wamuenzi Mwalimu Nyerere kwa vitendo kwa kuwachagua viongozi waadilifu, wasio na ukabila, udini na ubaguzi kuepuka laana ya Baba wa Taifa.
Rais Kikwete pia alisema Serikali itawashughulikia ipasavyo wote watakaopiga kura Oktoba 25 mwaka huu halafu wakabaki kituoni kwa ajili ya kulinda kura.
“Baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa wametoa matamko kuwataka wanachama wao wawahi wakapige kura halafu wakae mita 100 kwa ajili ya kulinda kura, Tume imekemea hilo,” alisema.
“Mtu yeyote atakayebaki kituoni kulinda kura atachukuliwa hatua za sheria, msiilazimishe Serikali kufanya yale yasiyopendeza, lakini ikibidi tutatimiza wajibu wetu,” alisema.
Rais Kikwete alisemaanasikitishwa na taarifa za watu wanaouza kadi zao za kupigia kura na kueleza kuwa uchunguzi
unaendelea, wale watakaothibitika watachukuliwa hatua za kisheria.