25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JK awananga Ukawa

5NA MWANDISHI WETU DAR ES SALAAM

RAIS Jakaya Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ameunanga Umoja wa Katiba ya
Wananchi (Ukawa) kwa kusema mgombea wao ameshindwa kuhutubia mikutano mbalimbali ya kampeni licha
ya kutumia usafiri wa helikopta.

Kauli hiyo aliitoa Dar es Salaam jana wakati CCM ilipofunga kampeni zake katika Viwanja vya Jangwani.
Kikwete aliyepanda jukwaani saa tisa alasiri, alisema mgombea urais wa chama hicho, Dk. John Magufuli, ametumia usafiri wa gari kuzunguka katika mikoa mbalimbali kuomba kura tofauti na mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) ambaye pia anaungwa mkono na Ukawa, Edward Lowassa.

Alisema Magufuli amekuwa akihutubia kwa saa moja katika mikutano yake kumwaga sera lakini wengine waliwaambia wananchi wakaangalie kwenye tovuti.

“Mwananchi wa kawaida huyu anaambiwa nenda ukaangalie kwenye website, nina hakika baada ya mkutano alikuwa anasema hivi alisema twende tukasome wapi, huku website ndiyo wapi,” alisema Kikwete.
Alisema Magufuli ndiye mtu anayefaa kuiongoza nchi kutokana na kuyajua vizuri matatizo ya wananchi kwa kuwa amezunguka kwa kutumia usafiri wa gari na kuona kero zinazowakabili wananchi.

Pia alisema katika kampeni zake moja ya sera alizozinadi ni kupambana na rushwa lakini wagombea wengine
wameshindwa kuizungumzia na hata kulitamka neno rushwa wamekuwa wakipata kigugumizi.

“Magufuli amesema atapambana na rushwa lakini yule mwingine amepata kigugumizi kulitamka neno rushwa hivyo akichaguliwa rushwa itastawi,” alisema Kikwete.

Aliwataka wananchi kujitokeza kupiga kura kesho na kuwahakikishia amani na haki kutendeka.
“Sisi hatutamnyima mtu yeyote haki yake hivyo kesho nendeni mkapige kura msiwe na wasiwasi kwa kuwa amani itakuwepo na hakuna kitu chochote kitatokea,” alisema Kikwete.

Alitumia nafasi hiyo kuwaombea kura wabunge wote wa majimbo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na madiwani
wa chama hicho.

Naye Magufuli ambaye alipanda jukwaani saa 10 alasiri, alisema baadhi ya wafanyakazi wamekuwa wakimtuhumu
kuwa yeye ni mkali lakini amekanusha na kusema alikuwa akitimiza wajibu wake.

“Sipendi unafiki naomba niwe mkweli, mimi ni mpole na sio mkali kama mnavyonifikiria ila kutokana na kuwa
kuna baadhi ya watu hata wakilipwa shilingi milioni 10 kwa mwezi bado watataka kuiba hivyo watu wa aina
hivyo wasitegemee kuwa kama wapo Dar es Salaam watahamishiwa mikoa mingine,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema jua lililomuwakia wakati wa kufanya kampeni litachangia hamasa ya kufanya kazi hasa kutokana na kuwa amezunguka nchi nzima na kuyaona matatizo ya wananchi pamoja na kero zao.

Alisema Kikwete aliwapa uongozi watu waliokuwa hawafai na hawakumsaidia chochote, lakini Serikali yake
itakuwa tofauti kwa kuwa itakuwa kazi tu.

A l i w a t a h a d h a r i s h a mafisadi waliobaki ndani ya CCM waendelee kujiondoa wenyewe kwa kuwa atakapoapishwa atapambana nao.

Katika mkutano huo uliohudhuriwa na maelfu ya wanachama na wafuasi wa CCM, walibeba mabango yenye ujumbe mbalimbali. Viongozi mbalimbali wa kitaifa walihudhuria mkutano huo akiwamo Waziri Mkuu mstaafu, Joseph Warioba, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana na Waziri Mkuu mstaafu, Salim Ahmed Salim.

Habari hii imeandikwa na Koku David, Esther Mnyika na  Victoria Patrick

- Advertisement -
Previous article
Next article

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles