31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

JK awabeza waliodharau shule za kata

Rais Jakaya KikweteNA RAMADHAN HASSAN, DODOMA

RAIS Jakaya Kikwete amewabeza wale walioziita shule za kata kwa jina la yebo yebo kwa kuwa sasa ndizo zinazofanya vizuri katika ufaulu kwa shule za Serikali.

Kauli hiyo aliitoa mjini hapa jana, wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Elimu yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma.

Alizitolea mfano shule tatu za Mkoa wa Kilimanjaro zilizofanya vizuri katika ufaulu wa mtihani wa kidato cha nne kitaifa.

“Tulikosea wakati tunajenga madarasa, niliwaagiza wajenge madarasa manne na tukaja kukumbuka hatuna majengo kwa ajili ya masomo ya sayansi, ila kwa sasa tunakwenda vizuri pamoja na watu kuziita shule hizo ni za yebo yebo, ila kwa sasa ndizo zinafanya vizuri,’’ alisema Rais Kikwete.

Aliwahimiza wadau wa elimu na wazazi kuhakikisha wanajenga madarasa kwa ajili ya kidato cha tano na sita kutokana na uhitaji wa madarasa.

Alisema uhitaji huo unakuja kutokana na ongezeko kubwa la wanafunzi wanaojiunga na kidato cha tano na sita, hivyo zinahitajika nguvu za ziada ili kutimiza malengo waliyojiwekea.

Aliwataka wazazi kushirikiana na Serikali kuhakikisha mwanafunzi anapata elimu bora badala ya kuliona suala hilo ni la mwalimu.

“Na nyie wazazi muwe hata mnaangalia madaftari ya watoto wenu pindi wanaporudi nyumbani, msifikiri suala hili ni la Serikali tu, tunatakiwa tusaidiane ili mwanafunzi apate elimu bora,’’ alisema Rais Kikwete.

Alisema kwa sasa Serikali imefikisha asilimia 80 ya mahitaji ya walimu, huku zikiwa zimebaki 20 ili kuweza kumaliza tatizo la walimu, huku akikiri uhaba wa walimu wa sayansi.

Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema maadhimisho hayo yanalenga kutoa elimu bora pamoja na kutoa tuzo kwa wanafunzi, shule, halmashauri, mikoa na walimu waliofanya vizuri katika elimu ya msingi na sekondari.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles