27.9 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

JK avumisha upepo mpya urais 2015

Rais KikweteNa Elias Msuya

WIKI chache baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema anatamani kurithiwa na kijana mwenye haiba yake alipokuwa akigombea urais mwaka 2005, sasa amebadili upepo na kusema vijana wajitokeze kugombea urais  kama alivyofanya yeye mwaka 1995, lakini hawatapitishwa.

Katika maadhimisho ya Siku ya Mwalimu Nyerere Oktoba 14, akiwa mkoani Tabora, Rais Kikwete alisema vijana ndio chachu ya maendeleo ya taifa lolote, hivyo washiriki katika kugombea nafasi mbalimbali za uongozi na kushiriki kupiga kura kumchagua rais anayefanana na kijana kama alivyokuwa yeye wakati akigombea urais wakati huo akiwa na umri wa miaka 55.

“Siyo kijana wa chini ya miaka 35, Katiba yetu hairuhusu, lakini mtu ambaye anaonekana kijana kama nilivyokuwa mimi wakati nagombea nafasi hiyo mwaka 2005,”  alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo, akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dodoma jana, alisema: “Unajua hili la vijana nililisema kule Tabora na halikuwapendeza sana baadhi ya watu. Basi leo nasema wote mjitokeze. Ipo siku mtajikuta mko wazee watupu na wakati wenu umepita na hamkutayarisha vijana basi na mjue chama chenu kinaondoka.

“Vijana watajitokeze tu watashindwa, watajiondokea na kuendelea na shughuli zao, lakini ukirudi wanakuuliza umerudi tena? Wewe sasa wakati wako.”

Aliendelea kufafanua: “Kwahiyo nilipolisema hilo nina maana hii. Lazima tuwe na safari ya kuwekeza, waacheni wajitokeze mtawaambia tu vijana bado wakati wenu, lakini wameshajitokeza mnajua hapa huyu hapa ni rasilimali,  huyu ni mlevi, kijana huyu lakini hana maana, ee unaweza kuwa kijana, lakini huna maana.

“Lazime nieleze hivyo, tunachukua watu wazima, lakini lazima tuwekeze kwa vijana wanaokuja, tusipofanya hivyo ‘future’ yetu iko shakani.”

Hivi karibuni kumekuwa na mfululizo wa makada wa CCM wanaotangaza nia ya kugombea urais kwa kete ya ujana.

Hadi sasa makada wa CCM waliotangaza nia na wanaotajwa kuwania urais kupitia chama hicho ni pamoja na Naibu Waziri wa Sayansi, Teknolojia na Mawasiliano, January Makamba (40), Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba (39), Mbunge wa Nzega, Dk. Khamis Kigwangala (39), Mbunge wa Songea Mjini, Dk. Emmanuel Nchimbi (43) na Mbunge wa Sengerema William Ngeleja (47).

Wengine ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe (61), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta (72), Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa (61), Waziri Mkuu mstaafu Fredrick Sumaye (64) na Waziri Mkuu wa sasa, Mizengo Pinda (66).

VIJANA NI HAZINA

Alisema vijana wanapaswa kuwa hazina ya uongozi, hivyo jamii iwaandae kwa kuwaruhusu kujitokeza kugombea tangu Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Mkiwa na jamii haina mpango mzuri wa kujenga vijana wake hawa, mtapoteza tu. Mtakuwa mnakazania ninyi wenyewe, mnachosha kwenye jamii, watasema hawa bwana tunawaheshimu, lakini ni mizee tu,” alisema Rais Kikwete.

Huku akijitolea mfano, Rais Kikwete alisema alijitokeza kugombea urais akiwa kijana, lakini hakupitishwa, hivyo hata vijana wanaweza wasipitishwe.

“Mimi mwaka 1995 nilijitokeza, pale nilikuwa na miaka 44 wakati ule, kijana kweli kweli, unajua vijana wanavutia. Lakini nilikuwa bado, haya sasa naambiwa subiri,” alisema na kuongeza:

“Mpaka nilipokuwa mtu mzima nikaambiwa wakati unatosha, lakini ndiyo uwekezaji ule. Kama ninyi hamna utaratibu wa kuwekeza na mkadhani kuwa tukitaja vijana tunakosea, hatukosei hata kidogo.”

Aliendelea kusisitiza umuhimu wa watu wa makundi yote kujitokeza katika uchaguzi huo na umuhimu wa kuwekeza kwa vijana katika uongozi.

“Lakini bado napenda sana kuwashawishi vijana wajitokeze. Unajua jamii hii lazima tutengeneze utaratibu wa kurithishana vizuri. Sisi ndio tulikuwa Tanu Youth League, tukapokea CCM Youth League. Sisi tukachukuliwa na Tanu. Mimi mwaka 1975 nikapelekwa Singida kuwa Katibu Msaidizi wa Mkoa. Tanu kiliwekeza Zanzibar tukaanzisha pale kuunganisha Tanu na ASP, baada ya hapo nikarudi Dar es Salaam, nikaenda Tabora, Monduli, Nachingwea, nikawa naibu waziri, waziri,” alisema.

Aliongeza: “Lakini hatimaye sasa ndiyo sisi hawa, uwekezaji ule wa Tanu na ASP, ule wa miaka 30, 40 iliyopita ndiyo sisi viongozi.”

UCHAGUZI WA SERIKALI ZA MITAA

Kuhusu  ratiba ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, alisema imeshatolewa na Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ambayo inaonyesha mikutano ya kampeni ya kuwanadi wagombea ni siku 14 itakayoanza Novemba 30 hadi Desemba 13.

“Mfumo wa utawala wa nchi yetu unaanzia kwenye shina, kitongoji na kijiji, baada ya hapo unafika kwenye kata, wilaya, mkoa na unamalizikia na taifa,” alisema.

Alisisitiza uchaguzi huo ni wa msingi kwani unajenga uongozi tangu shina hadi taifa.

“Tutakuwa tumehakikisha maendeleo ya nchi yetu, tunaimarisha utawala bora. Rai yangu kwenu mjitokeze kwa wingi kwenye kampeni muwasikilize wagombea wenu wakijinadi, wakijinasibu kisha mchague viongozi mnaoona wanatufaa. Tukiwapata watu wazuri tutakuwa na msingi mzuri na imara katika taifa letu,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles