28.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, March 19, 2024

Contact us: [email protected]

…Awataka kina Warioba waache biashara yao

Jaji Joseph Warioba
Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba

Na Fredy Azzah, Dar es Salaam

SIKU tatu baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba kupigwa na watu waliodaiwa kuwa ni wafuasi wa CCM, Rais Jakaya Kikwete amewaonya watu na vikundi vinavyoanza kufanya kampeni dhidi ya Katiba inayopendekezwa akisema muda wa kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria haujafika.

Mdahalo wa kujadili katiba inayopendekezwa ulioandaliwa na Taasisi ya Mwalimu Nyerere ulivunjika mwishoni mwa wiki baada ya kundi la vijana kufanya vurugu wakati Jaji Warioba aliyekuwa msemaji mkuu akihitimisha mada yake.

Kabla ya Jaji Warioba kutoa mada yake, Mwenyekiti wa taasisi hiyo, Joseph Butiku, alisema baada ya mdahalo huo watafanya mingine kwenye mikoa ya Mwanza, Zanzibar, Mbeya na Tanga.

Akizungumza na wazee wa Mkoa wa Dodoma jana, Rais Kikwete alisema kampeni za kuipinga ama kuikubali Katiba inayopendekezwa zitaanza Machi 30 na kufikia tamati Aprili 29 mwakani.

“Kulikuwa na dhana ya kampeni siku 60, na mimi nilidhani hivyo nikaongea na wanasheria wakasema siku za kampeni zinaamuliwa na rais.

“Lile la siku 60 lipo, lakini lipo kwenye mamlaka ya Tume ya Uchaguzi kuhusu vyama vya kijamii na kiraia kutoa elimu ya umma ndani ya siku 60 kabla ya siku ya kura ya maoni, tume imepewa mamlaka hayo kwa kifungu cha tano, kifungu kidogo cha nne cha sheria ya kura ya maoni.

“Kwa sababu hiyo, nawaomba Watanzania wenzangu tuzingatie matakwa ya sheria ya kura ya maoni, ambayo imeelekeza vizuri lini kura ya maoni itafanyika, lini kampeni zitafanyika, lini wadau watatoa elimu, naomba tuwe na subira, tuizingatie sheria hii, tukiizingatia hii hakuna ugomvi, tume itakapotoa maelekezo ya utekelezaji wa fursa husika kwa wadau tuzitumie.

“Tukienda kinyume cha hapo ndiyo mnafika mahali mnagombana, wakati wa kampeni bado, wakati wa elimu kwa umma kwa mujibu wa sheria bado, sheria hii imezipanga siku, siku 60 kabla ya kura ya maoni, vyama vya kijamii na kiraia ruksa kuelimisha jamii, siku 30 kabla kufanya kampeni ya kuunga mkono ama kukataa, mwisho kura kama “ndiyo” imeshinda ama “hapana”,” alisema Rais Kikwete.

Alisema mchakato wa Katiba unaongozwa na sheria ya kura ya maoni ambayo inaainisha wakati wa kuhamasisha, kuelimisha na kupiga kura.

“Tukizingatia hayo hakuna ugomvi,” alisema Rais Kikwete.

Akifafanua zaidi juu ya mchakato unavyoendelea hivi sasa, alisema sheria inataka ndani ya siku saba baada ya kukabidhiwa Katiba inayopendekezwa, aitangaze kwenye gazeti la Serikali jambo ambalo ameshalitekeleza.

Alisema sheria hiyo pia inataka ndani ya siku 14 baada ya kutoka kwenye gazeti la Serikali, itangazwe kwenye magazeti ya kawaida jambo alilosema linaendelea hadi wakati wa kura ya maoni.

“Hizi siku 14, unaongeza tena siku 70 zinakuwa 84, baada ya hapo inatakiwa mchezo uwe umekwisha,” alisema.

Alisema Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ndiye mwenye dhamana na Tume ya Uchaguzi na upigaji kura, aliwasiliana na chombo hicho na kikasema hakiwezi kuendesha kura ndani ya muda huo kwa sababu wanahitaji kurekebisha daftari la wapigakura.

Kikwete alisema chombo hicho kilisema hadi Desemba kitakuwa kimeshajiandaa kwa vifaa na miezi minne baada ya hapo kitakuwa kimemaliza kuwaandikisha zaidi ya watu milioni 23.

“Baada ya kutazama tukasema tuwape nafasi, Oktoba 3,  2014  Waziri Mkuu kwa kutumia mamlaka aliyonayo alitangaza kufanya mabadiliko kubadilisha sharti la siku 70,  na Oktoba 10 nikasaini hati ya kuagiza tume ihitishe kura ya maoni Aprili 30 mwaka 2015.

“Hatuna sababu ya kwenda zaidi ya hapo, kwa sababu tume walitaka miezi mitatu kuanzia Desemba, sheria inasema kama hatukupata turudie, tutarudia Juni, tusipofanikiwa tutaendelea na Katiba iliyopo na tutafanya Uchaguzi Mkuu Oktoba kama inavyotarajiwa,” alisema Rais Kikwete.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles