25.5 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

JK atema wakuu wa wilaya 19

Rais Jakaya KikweteNa Debora Sanja, Dodoma
RAIS Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya wakuu wa wilaya kwa kuwateua wapya 27, huku akiwahamisha 64 katika vituo vyao na wengine 42 amewabakisha katika maeneo yao ya zamani.
Akitangaza mabadiliko hayo jana mjini hapa, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alisema mabadiliko hayo yamesababishwa na kuwapo kwa nafasi 27 zilizokuwa wazi kutokana na wakuu wake wa wilaya watatu kufariki dunia na wengine kupandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa.
“Wakuu wa wilaya 27 wameteuliwa kuziba nafasi zilizoachwa kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo wengine kufariki dunia, kupandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa, kupangiwa majukumu mengine na wengine uteuzi wao kutenguliwa,” alisema Pinda.

WAKUU WA WILAYA WAPYA
Waziri Mkuu aliwataja wakuu wa wilaya wapya pamoja na vituo vyao vya kazi kuwa ni Mariam Mtima (Ruangwa), Dk. Jasmini Tisiike (Mpwapwa), Paloleti Mgema (Nachingwea), Fadhili Nkurlu (Misenyi), Felix Lyaniva (Rorya), Fredrick Mwakalebela (Wanging’ombe) na Zainab Mbussi (Rungwe).
Wengine ni Francis Mwonga (Bahi), Kanali Kimiang’ombe Nzoka (Kiteto), Husna Msangi (Handeni), Emmanuel Uhaula (Tandahimba), Mboni Mhita (Mufindi), Hashim Mngandilwa (Ngorongoro), Mariam Juma (Lushoto), Thea Ntara (Kyela), Ahmad Nammohe (Mbozi) na Shaaban Kissu (Kondoa).
Pia wapo Zelothe Stephen (Musoma), Pili Moshi (Kwimba), Mahmoud Kambona (Simanjiro), Glorius Luoga (Tarime), Zainab Telack (Sengerema), Bernard Nduta (Masasi), Zuhura Mustapha Ally (Uyui), Paul Makonda (Kinondoni), Mwajuma Nyirika (Misungwi) na Maftah Ally Mohamed (Serengeti).

WALIOHAMISHWA
Pinda, alisema wakuu wa wilaya waliobadilishwa vituo vya kazi ni Nyerembe Munasa anayetoka Arumeru kwenda Mbeya, Jordan Rugimbana, Kinondoni kwenda Morogoro, Fatma Salum Ally kutoka Chamwino kwenda Mtwara, Lephy Gembe kutoka Dodoma Mjini kwenda Kilombero na Christopher Kangoye kutoka Mpwapwa kwenda Arusha.
Wengine ni Omar Kwaang’ kutoka Kondoa kwenda Karatu, Francis Mtinga kutoka Chemba kwenda Muleba, Elizabeth Mkwasa kutoka Bahi kwenda Dodoma, Agnes Hokororo kutoka Ruangwa kwenda Namtumbo, Regina Chonjo kutoka Nachingwea kwenda Pangani, Husna Mwilima kutoka Mbogwe kwenda Arumeru na Gerald Guninita kutoka Kilolo kwenda Kasulu.
Aliwataja wengine waliobadilishwa vituo vya kazi ni Zipora Pangani kutoka Bukoba kwenda Igunga, Kanali Issa Njiku kutoka Misenyi kwenda Melele, Richard Mbeho kutoka Biharamulo kwenda Momba, Lembris Kipuyo kutoka Muleba kwenda Rombo, Ramadhani Maneno kutoka Kigoma kwenda Chemba, Venance Mwamoto kutoka Kibondo kwenda Kaliua, Gishuli Charles kutoka Buhigwe kwenda Ikungi, Novatus Makunga kutoka Hai kwenda Moshi na Anatory Choya kutoka Mbulu kwenda Ludewa.
Wengine ni Christine Mndeme kutoka Hanang’ kwenda Ulanga, Jackson Musome kutoka Musoma kwenda Bukoba, John Henjewele kutoka Tarime kwenda Kilosa, Dk. Norman Sigalla kutoka Mbeya kwenda Songea, Dk. Michael Kadeghe kutoka Mbozi kwenda Mbulu, Cripin Meela kutoka Rungwe kwenda Babati na Magreth Malenga kutoka Kyela kwenda Nyasa.
Said Amanzi kutoka Morogoro kwenda Singida, Antony Mtaka kutoka Mvomero kwenda Hai, Elias Tarimo kutoka Kilosa kwenda Biharamulo, Francis Miti kutoka Ulanga kwenda Hanang’, Hassan Masala kutoka Kilombero kwenda Kibondo, Angelina Mabula kutoka Butiama kwenda Iringa, Farida Mgomi Kutoka Masasi kwenda Chamwino, Wilman Ndile kutoka Mtwara kwenda Kalambo.
Pinda aliwataja wengine waliobadilishwa ni Ponsian Nyami kutoka Tandahimba kwenda Bariadi,Mariam Lugaila kutoka Misungwi kwenda Mbogwe, Mary Onesmo kutoka Ukerewe kwenda Buhigwe, Karen Yunus kutoka Sengerema kwenda Magu, Josephine Matiro kutoka Makete kwenda Shinyanga, Joseph Mkirikiti kutoka Songea kwenda Ukerewe.
Wengine ni Abdullah Lutavi kutoka Namtumbo kwenda Tanga, Ernest Kahindi kutoka Nyasa kwenda Longido, Anna Nyamubi kutoka Shinyanga kwenda Butiama na Rosemary Kirigini kutoka Meatu kwenda Maswa huku Abdallah Kihato akitoka Maswa kwenda Mkuranga.
Mabadiliko hayo pia yamewakumba aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Erasto Sima ambaye sasa anakwenda Meatu, Queen Mulozi kutoka Singida kwenda Urambo, Yahaya Nawanda kutoka Iramba kwenda Lindi, Manju Msambya kutoka Ikungi kwenda Ilemela, Saveli Maketta kutoka Kaliua kwenda Kigoma, Bituni Msangi kutoka Nzega kwenda Kongwa na Lucy Mayenga kutoka Uyui kwenda Iramba.
Wengine ni Majid Mwanga kutoka Lushoto kwenda Bagamoyo, Muhingo Rweyemamu kutoka Handeni kwenda Makete, Hafsa Mtasiwa kutoka Pangani kwenda Korogwe, Dk. Nassoro Ali Hamid kutoka Lindi kwenda Mafia, Festo Kiswaga kutoka Nanyumbu kwenda Mvomero, Sauda Mtondoo kutoka Mafia kwenda Nanyumbu, Seleman Mzee kutoka Kwimba kwenda Kilolo, Esterina Kilasi kutoka Wanging’ombe kwenda Muheza, Subira Mgalu kutoka Muheza kwenda Karagwe na Jacqueline Liana kutoka Magu kwenda Nzega.

WAKUU WA WILAYA WALIOBAKI
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, wakuu wa wilaya wanaobaki katika vituo vyao ni Jowika Kasunga (Monduli), Raymond Mushi (Ilala), Sophia Mjema (Temeke), Amani Mwenegoha (Bukombe), Ibrahimu Marwa (Nywang’wale), Rodrick Mpogolo (Chato) Manzie Mangochie (Geita), Darry Rwegasira (Karagwe), Luteni Kanali Benedict Kitenga (Kyerwa) na Constatine Kanyasu (Ngara).
Wengine ni Paza Mwamulima (Mpanda), Peter Kiroya (Kakonko), Hadija Nyembo (Uvinza), Dk. Charles Mlingwa (Siha), Shaibu Ndemanga (Mwanga), Herman Kapufi (Same), Ephraimu Mbaga (Liwale), Abdallah Ulega (Kilwa), Joshua Mirumbe (Bunda), Deodatus Kinawiro (Chunya), Rosemary Senyamule (Ileje) na Galamhusein Shaban (Mbarali).
Pia wapo Christopher Mgala (Newala), Baraka Konisaga (Nyamagana), Sara Dumba (Njombe), Hanifa Karamagi (Gairo), Halima Kihemba (Kibaha), Nurdin Babu (Rufiji), Methew Sedoyeka (Sumbawanga), Idd Kimanta (Nkasi), Chande Nalicho (Tunduru), Senyi Ngaga (Mbinga), Wilson Nkambaku (Kishapu) na Benson Mpesya (Kahama).
Wengine ni Paul Mzindakaya (Busega), Georgina Bundala (Itilima), Fatma Toufiq (Manyoni), Luten Edward Ole Lenga (Mkalama), Hanifa Selengu (Sikonge), Seleman Kumchaya (Tabora), Mboni Mgaza (Mkinga) na Seleman Liwowa (Kilindi).

WALIOFARIKI DUNIA
Waziri Mkuu aliwataja waliofariki dunia kuwa ni Kapteni James Yamungu aliyekuwa Serengeti, Anna Magoha, Urambo na Moshi Chang’a aliyekuwa Kalambo.

MA-DC WALIOPANDA
Pinda aliwataja wakuu wa wilaya waliopandishwa vyeo kuwa wakuu wa mikoa ni John Mongela aliyekuwa Wilaya ya Arusha, akawa mkuu wa Mkoa wa Kagera, Amina Masenza kutoka Wilaya ya Ilemela kwenda Mkoa wa Iringa, Dk. Ibrahimu Msengi kutoka Wilaya ya Moshi kwenda Mkoa wa Katavi, Halima Dendego kutoka Wilaya ya Tanga kwenda Mkoa wa Mtwara na Daudi Ntibenda kutoka Wilaya ya Karatu kwenda Mkoa wa Arusha.

MAJUKUMU MENGINE
Wakuu wa wilaya waliopangiwa majukumu mengine ni Brigedia Cosmas Kayombo aliyekuwa Simanjiro, Kanali Ngemela Lubinga (Mlele), Juma Madaha (Ludewa), Mercy Silla (Mkuranga), Ahmed Kipozi (Bagamoyo), Mrisho Gambo (Korogwe) na Elinas Plangyo (Rombo).

WALIOTENGULIWA UTEUZI
“Wakuu wa wilaya 12 uteuzi wao umetenguliwa kutokana na sababu za umri, kiafya na uboreshaji wa utendaji wa kazi.
“Waliotenguliwa ni James Ole Millya (Longido), Elias Wawa Lali (Ngorongoro), Alfred Msovela (Kongwa), Dany Makanga (Kasulu), Fatma Kimario (Kisarawe), Elibariki Kingu (Igunga) na Dk. Leticia Warioba (Iringa),” alisema Pinda.
Wengine ni Evarista Kalalu (Mufindi), Abihudi Siadeya (Momba), Martha Umbulla (Kiteto), Khalid Mandia (Babati) na Elias Goroi Boe Goroi (Rorya).
Pinda alisema mabadiliko hayo yameanza mara moja kuanzia jana na kuwataka kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi.
“Kwa wale wakuu wa wilaya wapya, kutakuwa na semina elekezi ambayo itafanyika hivi karibuni itakayoandaliwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles