31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Wasomali wawili mbaroni Tanga

chagonjaNA WAANDISHI WETU, TANGA
JESHI la Polisi nchini kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), limewatia mbaroni watuhumiwa wawili wanaodaiwa kuwa na asili ya Somalia katika msako unaoendelea dhidi ya kundi la wahalifu wa silaha mkoani Tanga.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Jeshi la Polisi mjini hapa, kiliiambia MTANZANIA kuwa watu hao walikamatwa jana saa 5 asubuhi katika eneo la Kijiji cha Amboni Mafuriko, baada ya kuonekana katika eneo hilo wakiwa wanashangaa na hawajui wanakokwenda.
Baada ya kuonekana kwa watu hao, wananchi wa kijiji hicho kilicho jirani na Kijiji cha Mleni ambako kundi la wahalifu wa silaha lilijificha, walitoa taarifa kwa polisi ambao walifika na kuwatia mbaroni.
“Ni kweli leo (jana) saa tano asubuhi huku eneo la Kijiji cha Amboni Mafuriko kuna watu wawili wenye asili ya Somalia walikamatwa baada ya wananchi kuwaona na kuwatilia shaka, na hivyo kufanikisha kukamatwa,” kilisema chanzo hicho.
Wakati huohuo, jeshi hilo linawashikilia watu wawili ambao ni wafanyabiashara na waumini wa dini ya Kiislamu wa Jumuiya ya Answar Suni mkoani hapa kwa tuhuma za kuhusishwa na tukio la kufadhili vikundi vya uporaji wa silaha dhidi ya polisi.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, ndugu wa watuhumiwa hao walidai ndugu zao wamekamatwa na polisi siku tatu zilizopita.
“Kuna ndugu zetu wawili wameshikiliwa kwa mahojiano kwa zaidi ya siku tatu na hatujawahi kuwaona kila tukiwapelekea chakula na dhamana imekataliwa, hivyo hali hiyo inatupa wasiwasi mkubwa,” alisema mmoja wa ndugu wa watuhumiwa hao ambaye hakutaka jina lake litajwe gazetini.
Mbali na matukio ya kukamatwa watu hao, hali ya ulinzi katika Hospitali ya Rufaa ya Bombo imeimarishwa, hasa katika wodi ambayo askari waliojeruhiwa kwenye tukio la Amboni wamelazwa wakiendelea na matibabu.
MTANZANIA ilimpotafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Fraser Kashai pamoja na Kamishna Mkuu wa Operesheni na Mafunzo nchini, Paul Chagonja, wote walisema wapo katika kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama.

Ma-RC wakutana
Katika hatua nyingine, wakuu wa mikoa minne ya Tanga, Manyara, Kilimanjaro, Arusha na Mtwara wamekuta mkoani hapa kwa ajili ya kujadili masuala ya ulinzi na usalama ikiwamo matishio dhidi ya ugaidi kwenye Ukanda wa Bahari ya Hindi.
Kikao hicho kimehusisha pia wawakilishi wa Wizara ya Uchukuzi, mameneja wa bandari za Tanga, Dar es Salaam na Mtwara pamoja na makamanda wa polisi wa mikoa hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari, Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Shaban Mwinjaka, alisema lengo la kikao hicho ni kuimarisha masuala ya ulinzi katika eneo la Bahari ya Hindi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles