25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

JK aongoza kumbukumbu ya mashujaa

Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete

Na Patricia Kimelemeta

RAIS Jakaya Kikwete, jana aliongoza mamia ya wananchi na wageni mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi katika maadhimisho ya siku ya mashujaa nchini, ambapo kitaifa yalifanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam.

Maadhimisho hayo yaliyoanza saa tatu kamili asubuhi na kumalizika saa tano, yalipambwa na gwaride rasmi la maombolezo ya mashujaa hao kutoka kwa majeshi ya ulinzi na usalama.

Wakizungumza wakati wa kuomba dua ya maadhimisho hayo, viongozi wa dini waliwaasa Watanzania kudumisha amani na mshikamano hasa katika kipindi hiki ambacho Serikali iko kwenye mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.

Mwakilishi kutoka Baraza la Maaskofu Tanzania, Padri Liberatus Kadio, alisema wananchi wanapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu ili kuepusha vurugu na migongano ambayo inaweza kujitokeza katika kipindi hiki.

“Tuepushe vurugu ambazo zinaweza kuhatarisha amani hasa katika kipindi hiki ambacho nchi ipo kwenye mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya,” alisema Padri Kadio.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanapaswa kuwa na nidhamu, upendo na mshikamano ili kuhakikisha kuwa mchakato huo unamalizika salama.

Alisema wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa kuwa na moyo wa uvumilivu wakati wa kujadili suala hilo ikiwa ni pamoja na kujadili utu wa mtu ili kuhakikisha kuwa suala hilo linafanikiwa.

“Ikiwa tutaanza kujengeana matabaka ya walionacho na wasionacho, tunaweza kusababisha migongano itakayoleta vurugu zisizo na lazima, hivyo basi tuache ubinafsi na kila mmoja kujadili utu wa mtu,” alisema.

Naye Mwakilishi kutoka Baraza la Kikristo Tanzania (CCT), Mchungaji Stephen Maligala, alisema kuwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanapaswa kujadili suala hilo katika hali ya utulivu na amani.

Alisema bila ya kufanya hivyo, mchakato huo hautafanikiwa, hivyo wanapaswa kuheshimiana na kujengeana nidhamu ya hali ya juu.

“Tuondoe itikadi za siasa na kuangalia masilahi ya wananchi kwanza ili tuweze kufanikiwa katika mchakato huu, bila ya kufanya hivyo hatutaweza kupata Katiba Mpya,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles