26.7 C
Dar es Salaam
Monday, March 4, 2024

Contact us: [email protected]

Bunge la Katiba mvurugano

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

Na Waandishi wetu, Dar es Salaam

JUKWAA la Katiba nchini (JUKATA) limeitaka Serikali kusitisha mchakato wa katiba mpya sambamba na kuahirishwa kwa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, kwa kile walichodai kutoelewana miongoni mwa wajumbe wa Bunge hilo.

Wakati JUKATA ikitoa tamko hilo, Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta, ameshindwa kuonana na wanahabari kama alivyoahidi ili kutoa tathmini ya kikao cha Kamati ya Mashauriano ya Bunge kilichofanyika juzi.

Kikao hicho kilikuwa kinajadili matatizo mbalimbali yaliyojitokeza katika mkutano wa Bunge Maalumu kipindi cha awamu ya kwanza na kusababisha baadhi ya wajumbe kutoka nje ya Bunge na kuapa kususia kushiriki vikao hivyo pamoja na kutathmini namna ya kupatikana maelewano miongoni mwa makundi ya wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.

Azimio la JUKATA

Katika azimio walilotoa jana kwa waandishi wa habari, JUKATA limetaka mchakato huo uahirishwe hadi Novemba na Desemba 2016, mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu.

JUKATA pia imetaka kuahirishwa kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu, badala yake ufanyike Oktoba mwakani ukiunganishwa na uchaguzi mkuu.

Makamu Mwenyekiti wa JUKATA, Hebron Mwakagenda, aliwaambia waandishi wa habari kuwa wameunda jopo la wanasheria wao kwenda Dodoma wakati vikao vya Bunge Maalumu vitakapoanza kwa lengo la kupeleka azimio lao na kutaka vikao hivyo viahirishwe.

Jopo hilo la wanasheria litaongozwa na Wakili wa JUKATA, Armando Swenye.

Kwa mujibu wa Mwakagenda, azimio lao linataka vikao hivyo vinavyotarajiwa kuanza Agosti 5, mwaka huu vifanyike kwa wiki mbili tu hadi Agosti 16 na kuahirishwa.

Mwakagenda alisema azimio lao limependekeza katika muda huo wa wiki mbili wajumbe wafanye kazi moja ya kujadili, kuridhia na kupendekeza ratiba mpya ya mchakato wa katiba mpya itakayoitwa rasimu ya ratiba.

Alisema JUKATA imetoa tamko hilo baada ya kutathmini kwa kina mwenendo wa mchakato wa Katiba Mpya, huku wajumbe wa UKAWA wakiendelea na msimamo wa kutorudi bungeni kujadili rasimu ya katiba.

“Tunapendekeza kuahirishwa kwa mchakato huu kutokana na kupanda kwa joto la uchaguzi kwa sababu wanasiasa wameamua kuitumia nafasi hiyo kujipima kisiasa wakati tukielekea katika uchaguzi huo.

“Hadi hivi sasa wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) wamegoma kurudi bungeni, lakini bado kuna michakato sita ambayo nayo inatakiwa kufanyika katika kipindi cha miezi 15 na hii inahitaji umakini pamoja na rasilimali fedha,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwakagenda, mambo muhimu yanayohitaji kuangaliwa kwa makini katika kipindi cha miezi 15 kabla ya uchaguzi mkuu 2015 ni pamoja na uandikishaji vitambulisho vya taifa ambao haujakamilika hadi sasa.

Mambo mengine ni uchaguzi wa Serikali za mitaa, uandikishaji upya wa wapiga kura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki, upigaji kura ya maoni kuamua hatima ya katiba mpya, uhakiki wa daftari la kudumu la wapiga kura pamoja na uchaguzi mkuu wenyewe.

“Kwa maana hiyo, tunapendekeza Bunge la Jamhuri ya Muungano Novemba mwaka huu likutane kwa ajili ya kupokea hoja ya kuahirishwa kwa Bunge Maalumu la Katiba pamoja na kupokea muswada wa marekebisho ya sheria ya Mabadiliko ya Katiba Mpya, ikiwamo kuingiza ratiba (road map) mpya katika sheria,” alisema Mwakagenda.

Alisema ni muhimu kukirejesha kifungu cha 37 cha sheria ya Mabadiliko ya Katiba 2011/2012 kwa kuibakiza Tume katika wajibu wa kuwapo kikatiba, kulitambua Bunge Maalumu kama Sekretarieti na mshauri mkuu juu ya maudhui ya Rasimu hiyo pamoja na kufuta vifungu vyenye utata katika sheria ya kura ya maoni kuhusu kamati za kura ya maoni.

Katika azimio lao, JUKATA imependekeza Juni hadi Julai 2016 ufanyike uchaguzi mwingine wa wajumbe wapya wa Bunge la Katiba hilo na kuchaguliwa wajumbe wawili wa kike na kiume kutoka katika kila wilaya ya kiserikali chini ya usimamizi wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Alisema Novemba hadi Desemba 2016, Bunge Maalumu litatakiwa kukutana kwa ajili ya kujadili Rasimu ya Katiba ambayo iliandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

“Januari hadi Juni 2017, Bunge litatakiwa kuipitisha rasimu hiyo na Julai hadi Novemba mwaka huo wananchi watatakiwa kupiga kura ya maoni na hatimaye Januari mosi 2018 itangazwe kwa kutiwa saini na kuzinduliwa,” alifafanua.

Naye Mwenyekiti wa JUKATA, Deus Kibamba, alisema kutokana na hoja ya kusogeza uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili ufanyike wakati mmoja na uchaguzi mkuu pamoja na hoja ya kuahirishwa kwa mchakato wa Katiba Mpya, ipo haja ya kufanyika mabadiliko kwenye masharti mbalimbali yanayohusiana na uchaguzi katika Katiba ya Tanzania, Katiba ya Zanzibar pamoja na sheria za uchaguzi.

“Inabidi kufanyike mabadiliko katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 na sheria kadhaa za uchaguzi na zile zinazohusu usimamizi na ulinzi,” alisema.

Alisema kutokana na umuhimu wa haja ya mabadiliko ya kikatiba na kisheria kuhusu maeneo yenye athari kwa uchaguzi, JUKATA imeteua jopo la wanasheria na wataalamu ili kuandaa pendekezo la masharti yote ya Katiba na Sheria yatakayoathiriwa na mabadiliko hayo na kupendekeza jinsi yatakavyofanana katika sura zake mpya baada ya mabadiliko.

Sitta akwepa wanahabari

Awali Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta, ilikuwa akutane na waandishi wa habari katika ukumbi wa ofisi ndogo za Bunge saa tatu asubuhi, lakini wanahabari walipofika eneo hilo waliambiwa mkutano huo utafanyika katika ukumbi wa Karimjee.

Waandishi wa habari walilazimika kuelekea katika ukumbi wa Karimjee, huku taarifa zikidai kuwa mkutano huo umesogezwa mbele mpaka saa tano asubuhi kwa kuwa Mwenyekiti amekwenda kuhudhuria sherehe za Kumbukumbu ya Mashujaa, zilizokuwa zinafanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Hata hivyo, baadaye zikatokea taarifa za kutatanisha kwamba mkutano huo umesogezwa mbele hadi saa saba mchana, kwa kile kilichodaiwa ratiba kuingiliana.

Ilipofika saa 7:30 mchana, huku waandishi wa habari wakiendelea kumsubiri Samwel Sitta, taarifa nyingine zikatolewa na Katibu wa Bunge la Katiba, Yahaya Hamisi Hamad, iliyowataka waondoke katika ukumbi huo na kwenda Ofisi za Bunge kwa kuwa muda walioomba kufanyia mkutano katika Ukumbi wa Karimjee ulikuwa umekwisha.

Waandishi walitoka Karimjee na kwenda ukumbi wa ofisi ndogo za Bunge na kulazimika kusubiri nje kwa muda usipungua dakika kumi na baada ya muda waandishi waliingia ndani ya ukumbi wa Bunge na kusubiri tena kwa  dakika zisizopungua 20, ndipo Katibu wa Bunge Maalumu, Hamad aliwasili akiwa ameshikilia karatasi mkononi.

“Ilikuwa Mwenyekiti (Sitta) aongee na nyinyi tangu asubuhi, lakini ratiba zimeingiliana, lakini ameniagiza niletea tamko nitawapa, lakini mimi siyo msemaji, siruhusu maswali,” alisema Hamad.

Tamko la Mwenyekiti

Tamko  hilo ambalo lilisainiwa na Mwenyekiti Sitta, lilisisitiza azma  ya kuendelea kwa awamu ya pili na Bunge hilo Agosti 5 mjini Dodoma kama ilivyopangwa.

Sitta alisema katika awamu hiyo ya pili, Bunge hilo litazingatia upya baadhi ya kanuni za Bunge hilo ambazo ni kikwazo katika kuhakikisha kazi ya kujadili na hatimaye kupitisha Katiba inayopendekezwa inakamilika ndani ya siku 60 zilizosalia kisheria na siku tatu za nyongeza zilizokuwa pungufu ya zile siku 70 za awali.

Msimamo wa Ukawa

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeendelea kusisitiza kuwa msimamo wao wa kutorudi kwenye kikao kijacho cha Bunge kinachotarajiwa kuanza Agosti 5, mwaka huu uko pale pale.

Akizungumza na MTANZANIA, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, alisema hawawezi kurudi kwenye Bunge hilo mpaka wajumbe wenzao, wakiwamo wa CCM wakubali kujadili rasimu ya Katiba kama ilivyoainishwa na Tume ya Jaji Joseph Warioba.

- Advertisement -

Related Articles

4 COMMENTS

 1. Ukawa hongereni, msikubali hadi CCM itakapotmka wazi kwea umma, kwamba wapo tayari kujadili rasimu ya warioba. WanaCCM wamezoea kuburuza Watanzania kila wakati. Mungu awabariki na kuwatia nguvu ya kumshinda pepo huyu. Viongozi wa dini msidanganye wananchi, achweni woga wa kuikemea CCM. Vongozi wa dini ikemeeni CCM iache kiburi na kuvuruga mchakato wa katiba. Mungu aibariki Tanzania. Muda wa kuogopana umekwisha, sasa ni kupeana ukweli basi.

 2. Naungana na JUKATA kwa mawazo yao kuwa BMK lifungwe kwani hakuna chochote kitakachoendelea huko na kuwaaminisha wananchi kuwa wanachojadili ni maoni ya watanzania.

  CCM lazima wajitambue na waache kujifanya wajinga, wehu au kama hawaoni na hawajui kuwa wanafanya makosa ya kuu
  puuza akili na mawazo ya watanzania.

  Napenda kuwashauri viongozi wa CCM kuwa makini kwani watafuta nafaso (opportunist) anatumia nafasi zao kuwadanganya na kiukweli kila kukicha wanapoteza mvuto kwa wananchi.

  Wawe makini na wawakilishi wao hasa wale wanaohojiwa na vyombo vya habari hasa TVs. Hawako makini na hanatoa kauli ambazo kwa waelewa ni matusi kwa wavuja jasho wa nchi hii.

  Mfano hai ni juzi tarehe 24 mmoja wa viongozi wake alipohojiwa na kituo kimoja cha TV alisema kuwa “Tanzania ni CCM na CCM ni Tanzania na chochote wanachotaka kitafanyika na hasa BMK.

  Amkeni na mfumbuliwe macho!

 3. Watu wengi sana,wasomi, wanaharakati, watu binafsi na hata viongozi wa dini wameishauri CCM kuachana na uchakachuaji lakini haisikii. KIla mtu sasa anajua UKAWA wapo sahihi kasoro wana CCM wachache wenye hofu ya kuondoka madarakani, kwamba HOja ni HII kwamba, Je CCM pamoja na viongozi wao wapo tayari kujadili rasimu ya Maoni ya wananchi? Kama wapo tayari wautamkie umma wa Watanzania na kusaini kwa maandishi ili wasipotimiza wao wasiondoe maana watakuwa wamekiuka mkataba akama wanavyoendelea kukiuka bila aibu. Jambo hilo ni dogo sana, mbona CCM hawataki kulielewa. Kila kiongozi wa CCM au serikali sasa wimbo niule ule” Ukawa rejeeni, je ninyi wenyewe mmejitahimini mna makosa gani na je makosa hayo mnayakubali? Namna nyingine kila Mtanzania mwenye akili timamu, mpenda ukweli na jasiri lazima ataunga mkono UKAWA tena wazi wazi.Huu si muda wa kuogopana, ni muda wa kuambiana ukweli FULL STOP!

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
584,000SubscribersSubscribe

Latest Articles