30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

JINSI YA KUMWEPUSHA MTOTO NA UDUMAVU

Na MWANDISHI WETU


mama-akinyonyeshaTANZANIA ni miongoni mwa nchi 10 zinazokabiliwa na changamoto ya kuwa na watoto wenye udumavu, ugojwa ambao unachangiwa kwa kiwango kikubwa na lishe duni wanazozipata watoto chini ya umri wa miaka mitano.

Mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya nchi yamekuwa yakihangaika kuhakikisha kuwa changamoto hii inapungua kama si kutoweka kabisa hapa nchini.

Kwa nyakati tofauti, jitihada zimekuwa zikichukuliwa katika kuhakikisha kuwa afya inaimarishwa kwa kila mtu, ambapo zimekuwa zikiungwa mkono na taasisi mbalimbali za dini.

Lakini bado hali ni tete kwa watoto ambao ndio wanaokumbana na tatizo hili la udumavu na ukondefu unaosababishwa na kukosa lishe bora.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaonyesha kuwa kila siku zaidi ya watoto 270 walio chini ya umri wa miaka mitano nchini Tanzania hupoteza maisha kwa lishe duni, huku zaidi ya watoto 2,700,000 wakikabiliwa na udumavu unaotokana na utapiamlo.

Takwimu zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 40 ya vifo hivyo hutokea katika mwezi wa kwanza wa maisha ya watoto hao.

Huku takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa kwa shabaha ya kuwasaidia watoto duniani UNICEF, zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 42 ya watoto wote wa Tanzania waliochini ya umri wa miaka mitano wamedumaa kutokana na kukosa lishe bora.

Chanzo cha ugonjwa huu wa udumavu kinaelezwa kuwa ni utapiamlo unaosabibishwa na lishe duni kwa mtoto ambapo huchangia mtoto kuwa na kimo au urefu mfupi usioendana na umri wake.

Japo kumekuwapo na dalili za kupungua kwa kiwango cha udumavu nchini kwa asilimia 30, kati ya mwaka 1994 hadi 2014 japo idadi ya watoto waliodumaa ikiwa imeongezeka kutoka milioni 2.4 hadi 2.7 katika kipindi hicho.

Sababu nyingine ya udumavu ni kutokana na kuugua mara kwa mara katika miaka mitatu ya mwanzo ya makuzi yake.

 

Sababu nyingine ni afya na lishe duni kwa wanawake kabla ya ujauzito, wakati wa ujauzito na baada ya kujifungua.

Pia kutopangilia uzazi yaani kuzaa karibu karibu na tatizo la wasichana kubeba mimba wakiwa katika umri mdogo.

Taratibu duni za ulishaji watoto, ikiwamo kutonyonyeshwa maziwa ya mama pekee katika kipindi cha miezi sita ya mwanzo baada ya kuzaliwa na kupewa chakula cha nyongeza kisichokidhi mahitaji yao ya lishe pale wanapotimiza umri wa miezi sita.

Watoto kupewa kiasi kidogo cha chakula au kisichokuwa na ubora au mchanganyiko wa makundi mbalimbali ya chakula pia ni sababu nyingine zinazodumaza watoto.

 

Athari

Mtoto kuwa na udumavu huchangia kupata athari zisizoweza kurekebishika katika maisha yake hata kama kwa hapo baadaye atapewa lishe bora, mwili wake tayari utakuwa umedumaa na hivyo kushindwa kupokea marekebisho.

Kushuka kwa maendeleo ya akili ya mtoto pia ni moja ya athari za udumavu, hatua hii humfanya mtoto kushindwa kufanya vizuri hata kwenye masomo yake.

Kuwa na uzito mkubwa, kiriba tumbo na kukumbwa na magonjwa yasiyoambukiza kama moyo, kiharusi, shinikizo la damu na hata kisukari.

 

Namna ya kukabiliana na ugonjwa huu

Ni wazi kuwa mpango wa WHO kwa Tanzania ni ifikapo mwaka 2025 walau idadi ya watoto wenye umri chini ya miaka mitano waliodumaa iwe imepungua kwa walau asilimia 40.

Hata hivyo, malengo haya yatafanikiwa tu iwapo Watanzania watazingatia lishe bora kwa watoto na mjamzito  kulinda afya yake katika kipindi chote cha ujauzito na kuzingatia unyonyeshaji pindi anapojifungua.

Ni muhimu kwa akina mama kunyonyesha watoto wao maziwa hadi watakapofikia miaka miwili, hapa wanawake wajitahidi kutowaachisha watoto wao nyonyo mapema.

Inashauri kwa mama kumnyonyesha mtoto wake ziwa lake kwa kipindi cha miaka miwili.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles