Na WAANDISHI WETU-DAR/IRINGA
TUNAKUFA. Ndilo neno la mwisho lililotolewa na Consolata ambaye ni pacha na Maria Mwakikuti waliofariki dunia usiku wa kumkia jana mkoani Iringa.
Mapacha hao ambao walipigania uhai wao kwa siku 153 katika hospitali mbalimbali,walifariki juzi, baada ya kuwa na tatizo kubwa la kupumua.
Wakiwa na ndoto ya kuwa walimu watakaofundisha wanafunzi wenye mahitaji maalumu, mapacha hao walifariki dunia saa 2 usiku wa kuamkia jana, huku wakipishana kwa dakika 10.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Dk. Museleta Nyakaloto, alisema vifo vyao vilitokana na tatizo la upumuaji, huku Consolata akitamka neno ‘tunakufa’, baada ya mwezake kufariki dunia.
“Walikuwa wakipatiwa matibabu katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), walipishana kwa dakika 10, alianza Maria na baadaye akafuatia Consolata.
“Aliyekuwa na tatizo zaidi alikuwa Maria,tangu alipofika alikuwa akipumua kwa kutumia mashine ya oksijeni. Consolata alikuwa akitumia oksijeni mara mojamoja na kabla ya kifo chao, Consolata alisema tunakufa,” alisema Dk. Nyakaloto.
Alisema waliwapokea mapacha hao, Mei 17 mwaka huu, saa 1:30 usiku wakitokea Hospitali ya Taifa Muhimbili walikokuwa wakipatiwa matibabu.
Alisema tangu walipokuwepo hospitalini hapo (Iringa) zaidi ya wiki mbili hawakuonyesha mafanikio ya afya zao kuimarika hadi usiku wa kuamkia jana walipofariki dunia.
“Walikuwa wameruhusiwa kwenda nyumbani kuendelea na matibabu na sisi tulitakiwa kuendelea kuwafuatilia wakiwa nyumbani.
“Lakini kutokana na hali waliyokuwa nayo na safari ndefu, waliokuwa wameongozana nao waliona ni busara kuwapitisha hospitalini (Iringa) kwa ajili ya uchunguzi wa afya zao, badala ya kuwapeleka moja kwa moja nyumbani,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, alisema wakati mapacha hao wakifariki baadhi ya masista wa Shirika la Masista la Maria Consolata walikuwepo hospitalini hapo.
Kasesela alisema wanatarajia kuaga miili ya mapacha hao leo ili mazishi yafanyike kati ya kesho au kesho kutwa katika makaburi ya Tosamaganga ambayo hutumika kwa ajili ya maparoko na masista.
“Tumesikitika sana kwa vifo vya mapacha hawa na mimi niliwahi kwenda kuwaona pale Muhimbili. Tunamsubiri sista Jane (Mkuu wa Shirika la Masista la Maria Consolata) ili kuweza kupanga pamoja taratibu za mazishi yao.
“Tunawaomba wana Makete pamoja na ndugu zake kujitokeza kushiriki mazishi, watoto hawa walikuwa watu wa furaha wakati wote na walikuwa wameanza biashara ya kuuza vitenge wakati wakisoma chuo kikuu,” alisema Kasesela.
Kwa mujibu wa Kasesela, pacha hao walizaliwa wilayani Makete na mama yao alifariki mara baada ya kujifungua. Baba yao alifuata baadaye na walikuwa wakilelewa na masista hao.
Mkuu wa Wilaya ya Kilolo ambako mapacha hao walipata elimu ya sekondari, Asia Abdalah, alisema kifo hicho ni pigo kubwa kwa wana Kilolo na kwamba wataendelea kuwaenzi.
Kwa habari zaidi pata nakala yako ya gazeti la mtanzania hapo juu