Na CHRISTIAN BWAYA
FARIDA amekuwa akisifika kuwa ni mtoto mwenye nidhamu kwa wazazi wake. Mara zote ana usikivu, utii na heshima kwa watu. Hadi anamaliza darasa la saba, hakuwahi kupishana kwa vyovyote na wazazi wake.
Mambo yalianza kubadilika alipofika kidato cha pili. Siku moja wakati muda wa kwenda kanisani umefika, hakuonekana kuwa na haraka tofauti na kawaida yake.
“Unafanya nini muda wote mbona kama huna haraka?” aliuliza mama yake kwa hasira.
“Najiandaa mama,” alijibu huku akiendelea kutengeneza nyusi zake.
“Muda umeisha mwanangu tunachelewa,” baba aliamua kuingilia kati.
Ukweli ni kwamba Farida hakuwa na nia ya kwenda kanisani akiambatana na wazazi wake. Alichokosa ni ujasiri wa kulisema hili wazi wazi kwa wazazi wake.
Baada ya dakika 10 za kusubiri, baba alikumbushia kwa hasira: “Farida tunakusubiri.”
“Basi tangulieni baba. Nitakuja mwenyewe!” Hicho ndicho alichokuwa anakitaka. Hakupenda kuambatana na wazazi wake.
Katika umri wake wa miaka 14, Farida ameanza kujenga umbali na familia yake. Wazazi wake wanapozungumza naye, haonekani kufuatilia wanachokisema. Zamani, kwa mfano, alikuwa mchangamfu katika mazungumzo. Siku hizi ameanza kuwa mkimya hasa anapokuwa nyumbani.
Hata hivyo, anapokuwa shuleni akiwa na marafiki zake, Farida ni mwongeaji mzuri. Kwanini basi Farida anakuwa mkimya anapokuwa nyumbani?
Ukweli ni kwamba, Farida ana mambo mengi moyoni mwake kwa kuwa ni kijana chipukizi. Matamanio ya kujihakikishia hadhi sawa na mtu mzima yanamfanya ahisi wazazi wake hawamwelewi. Wanaposisitiza kwenda naye kanisani, hiyo kwake ni sawa na kumchukulia kama mtoto asiyeweza kujisimamia.
Ingawa anahitaji uhuru zaidi, wazazi wake wana wasiwasi. Wanajua hatari ya uhuru huo na wanaamini bado ni mtoto anayehitaji uangalizi wa karibu. Wakifanya hivyo, Farida anahisi ‘kufuatwa fuatwa.’
Katika mazingira kama haya, wazazi wanahitaji kuangalia namna ya kumfanya Farida ajisikie kuwa na uhuru kiasi hata kama bado watakuwa wanamfuatilia bila yeye kujua. Uhuru wa wastani utamfanya aamini wazazi wake wanatambua hadhi mpya aliyonayo.
Katika umri alionao, Farida anatamani kutumia muda mrefu akiwa na marafiki zake zaidi kuliko familia yake. Mtandao mpya wa marafiki mbali na familia yake unamsaidia kutengeneza haiba yake akiwa mtu mzima. Hali hii, hata hivyo, inawatia hofu wazazi.
Wazazi, kwa kutambua hatari ya uhuru, wanatamani kumdhibiti zaidi. Kadiri wanavyojaribu kumdhibiti, wanashangaa tatizo jingine linajitokeza. Umbali na tofauti za mara kwa mara zinaendelea kuongezeka. Badala ya kumdhibiti, hali inayoweza kumfanya ajihisi bado mtoto, inashauriwa kujenga ukaribu wa mawasiliano yanayotambua uhuru wake.
Mitazamo mipya inayo hitalifiana na wazazi, ni hali inayotarajiwa kwa kijana chipukizi kama Farida. Hali hii mara nyingi hutengeneza mashindano yasiyo ya wazi kati ya mzazi na kijana wake. Kinachoshindaniwa, mara nyingi ni mamlaka. Mzazi anahisi mamlaka yake yanadharauliwa na mtoto anayejifanya mjuaji, na mtoto naye anajihisi bado anaonekana mtoto asiye na sauti.
Mashindano haya ya kichini chini yanaweza kupanda ngazi na kugeuka kuwa ukosefu wa nidhamu. Mtoto anamwona mzazi wake kama mkoloni aliyepitwa na wakati na mzazi naye anamwona kijana chipukizi kama mtoto asiyejua maisha ni kitu gani.
Katika mazingira kama haya, kupambana naye inaweza isiwe njia mwafaka. Kadiri unavyopambana naye, ndivyo unavyojenga ukuta wa mawasiliano baina yenu.
Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.