31.8 C
Dar es Salaam
Thursday, December 12, 2024

Contact us: [email protected]

Ishara ya mpenzi atakaye kusaliti ndani ya ndoa

Na CHRISTIAN BWAYA

WATU wengi wamejikuta kwenye matatizo makubwa ya ndoa kwa sababu tu hawakuweza kubaini ishara mbaya mapema.

Kama tulivyosema kwenye makala iliyopita, binadamu ni mtu mtata kumwelewa. Huwezi kumwelewa kwa kutazama tabia anazozionesha kwa nyakati fulani au anapokuwa na kundi fulani tu la watu.

Ukweli ni kwamba tabia halisi ya mtu huwa haibadiliki hata kama kwa juu juu unaweza kufikiri amebadilika. Mtu mgomvi, anabaki kuwa mgomvi hata kama kuna mazingira yanayomfanya aonekane ni mpole. Upole unaweza kuwa upepo unaopita lakini ndani yake akabaki kuwa mgomvi. Mtu mwenye kisasi, halika dhalika, anabaki kuwa na kisasi hata kama kuna mazingira yanamfanya aonekane kama mtu anayejua kusamehe.

Unapotaka kumwelewa binadamu vizuri, kisaikolojia tunasema zingatia tabia yake hasa anavyowatendea watu asiowahitaji. Tulisema, kwa mfano, bosi mpole kwa mhudumu wake wa ofisi ana nafasi kubwa zaidi ya kuwa na hulka hiyo ya upole kuliko mhudumu wa ofisi anayeonesha nidhamu kwa bosi wake. Vile unavyomtendea mtu wa chini yako ndivyo ulivyo.

Katika makala ya leo ningependa tutazame suala la uaminifu wa mtu. Tunafahamu kuwa ndoa imara hujengwa na watu wawili wanaoaminiana. Kuaminiana maana yake ni kutokuwa na wasiwasi usio na sababu na mwenzako; kutokuwa na hofu kuwa mwenzako anaweza kuwa kinyume na wewe na hivyo kukusaliti; pia kuaminiana maana yake ni kutokuwa na sababu ya kumfuatilia wala kumdhibiti mwenzako kupita kiasi kwa sababu ya wivu. Matatizo mengi kati ya wanandoa huanza pale mmoja wao anapokosa imani na mwenzake.

Ingawa ni vigumu kumwamini mwenzako kwa asilimia 100, bado tunafahamu umuhimu wa kuwa na kiwango cha kutosha cha imani na mwenzako. Utaficha fedha, kwa sababu huna imani na mwenzako. Utakuwa na wivu uliopindukia kwa sababu huna imani na mwenzako. Utamdhibiti mno mwenzako kwa sababu humwamini. Hakuna mtu anayeweza kuwa kwenye uhusiano wa namna hii na akajisikia amani labda kama amejikatia tamaa.

Swali ni je, ni namna gani unaweza kumfahamu mpenzi anayeweza kugeuka kuwa mtu asiyekuamini kabisa hata kama kwa sasa anaonesha kukuamini? Je, utajuaje kuwa mpenzi wako anakuamini? Siku zote imani kwa mwingine inaanza na imani uliyonayo kwako mwenyewe. Ili mpenzi wako akuamini, lazima kwanza yeye mwenyewe ajiamini. Je, mpenzi wako uliyenaye anajiamini? Je, anapokuona na watu wa jinsia nyingine hajisikii vibaya?

Naelewa mapenzi yana tabia ya kumiliki. Tunapenda kuwamiliki wale tunaowapenda. Lakini hali hii inapovuka mipaka inakuwa tatizo. Fikiria mtu anayekuzuia kuongea na watu wengine. Mtu asiyetaka ufanyekazi kwa sababu ofisini utakutana na watu wengine. Fikiria mtu anayekagua mawasiliano yako kujua umezungumza na nani. Hizi si dalili njema na zinaweza kuwa ishara kwamba uko kwenye uhusiano na mtu atakayekunyang’anya uhuru wako kama binadamu timamu.

Tusisahau kukumbusha na hapa kwamba wakati mwingine tabia zako mwenyewe zinaweza kuwa chanzo cha mwenzako kushindwa kukuamini. Unapoona mwenzako ana wivu kupindukia, kwa mfano, wakati mwingine wewe mwenyewe umeweka mazingira hayo ya kutokuaminika. Mwenzako hakuachi upumue kwa sababu anakufahamu ulivyo. Anajua ukiachiwa upenyo hufanyi makosa. Katika mazingira kama haya, ni vyema kujikagua na kuchukua hatua za kubadilika.

Uchumba ni wakati mzuri wa kufahamiana na mwenzako. Maisha unayoishi na mwenzako kabla hamjaoana, ni kielelezo cha aina ya maisha mtakayoishi mkishaoana. Rudia kusoma sentensi hiyo. Mkikosa nidhamu na mipaka kama marafiki, ndoa haitaleta miujiza. Mtakuwa vile vile, mkiishi maisha yasiyo na utaratibu mkiwa wapenzi mnakaribisha maisha ya ndoa ya kutokuaminiana, tafiti zinaonesha hivyo.

Kutokuaminiana hakuanzii kwenye ndoa. Mnaanza kujenga tabia ya kutokuaminiana kwa tabia mlizonazo kabla hamjaoana. Mnaweza kushirikiana kufanya mambo mnayojua si sahihi kwa mwamvuli wa mapenzi lakini hayo hayo yakawa chanzo cha kujenga msingi mbovu wa huko mnakokwenda.

Nikitumia mifano ya wazi zaidi, ikiwa mnaweza kuitana na mkalala pamoja mkiwa wachumba, maana yake mnafahamishana kwamba hiyo ndiyo tabia yenu. Kwamba yuko tayari kulala na wewe na anajua kwamba hamjaoana, maana yake anaweza kulala na yeyote hata baada ya ndoa. Usishangae kwanini baadae atakapokuoa atakuwa na michepuko.

Ikiwa unataka kuwa na mume au mke mtakayeaminiana, anza kuishi maisha yanayojenga misingi ya kuaminiana baadae. Kataa mazingira yatakayomfanya ajue huaminiki. Sema hapana kwa ngono kabla ya ndoa. Mchumba anayekuacha kwa sababu umemkatalia ngono kabla ya ndoa anakusaidia kuepuka majuto ya kuishi na mtu asiyeweza kujizuia hata akiwa na ndoa.

Christian Bwaya ni Mhadhiri wa Saikolojia, Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Kwa unasihi wasiliana naye kwa 0754 870 815.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles