Na Anna Potinus, Dar es Salaam
Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es salaam imetoa tahadhari kwa wananchi kuwa waangalifu katika kipindi cha Sikukuu ya Pasaka kwa kujiepusha na vitendo vya kihalifu kwa kutoa taarifa ili kuhakikisha hatua zinachukuliwa haraka kabla madhara hayajajitokeza.
Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema hayo leo Ijumaa Machi 30, jijini Dar es Salaam ambapo pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kuonyesha ushirikiano kwani jukumu la kuzuia uhalifu ni la kila mmoja.
“Jeshi la polisi linawaomba wakazi wa Dar es salaam kuonyesha ushirikiano kwani jukumu la kuzuia uhalifu ni la kila mmoja wetu, hivyo washiriki kutoa taarifa za kihalifu ili kuhakikisha hatua zinachukuliwa haraka kabla madhara hayajajitokeza.
“Lengo la kuimarisha ulinzi ni kuhakikisha wakazi wa Dar es salaam wanasheherekea sikukuu ya pasaka kwa amani na utulivu,” amesema.
Katika hatua nyingine, Mambosasa amewaasa watu watakaokuwapo maeneo ya fukwe za bahari kuwa waangalifu na kuchukua tahadhari kwa kutoruhusu watoto kuogelea peke yao badala yake wawe chini ya uangalizi wa watu wazima na kuwasihi wanaokunywa pombe kunywa kwa kiasi.
“Katika maeneo ya starehe wananchi wanatakiwa kuwa waangalifu kwa kutokunywa vileo kupita kiasi na madereva wafuate sheria za usalama barabarani na kuepuka kuendesha vyombo vya moto wakiwa wamelewa,” amesema Kamanda Mambosasa.
Hata hivyo, Kamanda Mambosasa amesema jeshi lake limeimarisha doria na misako watatumia magari, pikipiki, farasi na nyinginezo kuhakikisha tuko karibu na wananchi kuhakikisha jiji letu linakuwa salama kipindi hiki cha sikukuu.