28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, December 1, 2024

Contact us: [email protected]

Jeuri ya Ukawa

MTZ Alhamisi new july.indd*Waainisha watakapopata fedha za kutoa elimu bure, kuziba pengo la bajeti watakapopunguza kodi ya mshahara kutoka asilimia 18 hadi tisa.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BAADA ya ahadi ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ya kutoa elimu bure kwenye ngazi zote na kupunguza kodi ya mishahara kutoka asilimia 18 hadi tisa, kubezwa kwamba haitekelezeki, umoja huo umeeleza ilipopata jeuri ya ahadi hiyo baada ya kuainisha vyanzo vya mapato watakavyotumia.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam juzi, Mwenyekiti Mwenza wa Ukawa, James Mbatia, amesema wamefanya utafiti wa kina na kubaini ahadi hizo zinatekelezeka tofauti na ambavyo wapinzani wanawakejeli.

Alisema utafiti uliofanyika umebaini kuwa iwapo watadhibiti mapato yanayopotea katika ulipaji kodi, kupunguza misamaha ya kodi hadi asilimia 1, kuboresha ufanisi katika Bandari ya Dar es Salaam, sekta ya utalii na uvuvi, mapato ya Serikali yataongezeka maradufu kuliko ya sasa.

“Wameanza kutukebehi kwamba ilani yetu haitatekelezeka, eti hizo fedha za kutoa elimu bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu itatoka wapi,” alisema.

Alisema takwimu za Serikali sasa hivi zinaonyesha mapato ya ndani yatokanayo na kodi na yasiyotokana na kodi ni Sh trilioni 13.47 ambayo ni asilimia 14.3.

“Hivyo kutokana na takwimu hizo, asilimia 100 ya pato la taifa ni zaidi ya Sh trilioni 90,” alisema.

Mbatia alitaja mambo yatakoyoweza kusaidia kwenye ukusanyaji kodi ni kuwekwa mazingira mazuri kwa mlipakodi na wigo wa kodi kutanuliwa, kuwapo viwango vya kodi vinavyotabirika na tegemezi na  Mamlaka ya Mapato (TRA) kupambana na ukwepaji wa kodi.

Alitaja njia nyingine kuwa ni kupunguza misamaha ya kodi hadi kufikia asilimia moja ya pato la taifa, kuongeza ufanisi Bandari ya Dar es Salaam, kuweka mazingira mazuri na endelevu kwenye sekta ya utalii na kukusanya kwa ufanisi mapato kwenye sekta ya uvuvi.

“Kwenye sekta ya uvuvi pekee tunaweza kupata zaidi ya Sh trilioni moja kwa mwaka. Lakini pia kwa sasa mapato yanayotokana na kodi ya nyumba kubwa kubwa ni asilimia tatu tu ya makusanyo yote,” alisema.

 

ZITAKAKOTOKA FEDHA ZA ELIMU

Mbatia alisema wakati Serikali ina uwezo wa kukusanya asilimia 25 pekee ya pato la taifa kwa sasa, wao wataweza kukusanya na ongezeko la zaidi ya Sh trilioni 10.

“Chukua asilimia 25 ya pato la taifa leo ambalo kwa takwimu za Wizara ya Fedha ni zaidi ya trilioni 23.55 wakati wao wanakusanya Sh trilioni 14.3, niwahakikishie Watanzania tuna uwezo wa kuleta ufanisi tukifanya uamuzi, na Lowassa anaweza kufanya uamuzi mgumu,” alisema Mbatia.

Alisema wanafunzi wanaosoma katika vyuo vikuu ni 300,000 na ada yao ni inafikia sh trilioni 1.55, hivyo hata kama wataongezeka mara mbili bado Serikali ya Ukawa itaweza kumudu gharama hizo kutokana na makusanyo ya kodi.

 

KODI YA MSHAHARA

Mbatia alisema kwa sasa kodi ya wafanyakazi wa Tanzania ni kubwa ikilinganishwa na nchi nyingine za Afrika Mashariki.

Alisema licha ya kwamba Serikali inasema kodi ni asilimia 11, ukweli ni kuwa kiasi hicho kinakatwa kwa watu wenye mshahara wa kima cha chini, huku wale wa juu wakikatwa hadi asilimia 18.

“Wafanyakazi wa Tanzania ndio wanalipa kodi kubwa ya mshahara ambayo ni takribani asilimia 18, na hizo ni takwimu za Benki ya Dunia tukifuatiwa na Uganda wanaolipa asilimia 11, Burundi asilimia 10, Kenya asilimia 6.8 na Rwanda asilimia 5.6.

“Tunavyosema tutapunguza kodi kutoka asilimia 18 mpaka tisa ambayo ni punguzo la Sh bilioni 704, hilo punguzo tutalipata kwenye sekta ya utalii, uvuvi, ndiyo maana tunasema tutaipunguza kodi kwa mfanyakazi, tunawaambia Watanzania watuamini, haya tutayafanya na yanawezekana kabisa,” alisema Mbatia.

 

SAFARI ZA VIONGOZI

Mbatia alisema mbali na kuangalia mambo makubwa, safari za viongozi ni eneo jingine watakaloweza kulitumia kupata fedha zitakazoweza kufidia pengo litakalosababishwa na kupunguza kodi ya mishahara na kutoa elimu bure.

“Viongozi walioko madarakani, hususani rais, ameshasafiri nje ya Tanzania takribani mara 409 na wastani wa kila safari ya siku tatu mpaka tano ni dola milioni 3 na milioni 5, hivyo mpaka sasa tayari wametumia takribani sh trilioni 4 katika safari hizo,” alisema.

Alisema fedha hizo zingeweza kujenga vyuo vya kisasa vya veta zaidi ya 200 nchi nzima ambapo kila kimoja kingegharimu Sh bilioni 20, pia zingeweza kujenga hospitali zaidi ya 100, kila moja ikigharimu Sh bilioni 30 na kujenga vyuo vikuu zaidi ya 80, kila kimoja kikigharimu Sh bilioni 50.

Mbatia alisema si kwamba Serikali ya Ukawa itaishi kama kisiwa bila kushirikiana na wengine bali watapunguza safari zote zisizo za lazima.

“Kwa mfano rais anataka kutunukiwa shahada ya heshima, hakuna sababu ya yeye kwenda nje ya nchi na kutumia mabilioni ya fedha za walipakodi, kwanini hao wanaotaka kumtunuku wasije pale Ikulu? Lakini hata mikutano mingine siyo lazima aende, anaweza kushiriki kwa kutumia teknolojia (teleconference),” alisema.

 

VITISHO

Mbatia alisema Watanzania sasa wanataka mabadiliko, hawataki kurudishwa nyuma pamoja na vitisho vinavyojitokeza kutoka kwa Chama Cha Mapinduzi na mgombea wake Dk. John Magufuli.

Alisema katika mikutano yake ya kampeni, Dk. Magufuli amekuwa akitoa lugha za vitisho kuwa iwapo wananchi watachagua upinzani, yaani Lowassa na wabunge na madiwani, nchi itaingia katika machafuko makubwa kama ya Libya.

Mbatia alisema kauli hiyo ya Magufuli si ya kweli bali inalenga katika kuwaogopesha wananchi walioamua kufanya mabadiliko.

“Nataka niwaambie Watanzania mfumo uliokuwa Libya ulikuwa umekatisha tamaa wananchi wa nchi hiyo. Pamoja na kuwa walipata huduma nzuri za kijamii, lakini walikosa haki, walinyimwa haki zote za kimsingi ndugu zetu wa Libya, hivyo wakaamua kuandamana,” alisema.

Aliwataka Watanzania kutokuwa na wasiwasi kwani Katiba ya Tanzania ibara ya tisa inaeleza namna Mtanzania anavyotakiwa kushiriki katika haki ya kuishi na haki ya kuzaliwa.

Alisema lakini sasa viongozi wa chama tawala na Serikali yake wameanza kuwa sehemu ya vurugu ambazo zimesababisha damu kumwagika katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Mbatia alisema Ukawa imekuwa kimya pamoja na kupoteza watu wake wilayani Tarime na maeneo mbalimbali.

Alisema Ukawa wanaheshimu amani iliyoletwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na mama Tanzania pamoja na kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakitukanwa, kuteswa na kudhalilishwa na viongozi walioko madarakani.

“Ukawa bado tuko kimya, tumeitwa majina mengi oil chafu, tumeitwa makapi, tumeitwa wapumbavu na malofa, bado tuko kimya kwa ajili ya mama yetu Tanzania,” alisema Mbatia.

Aliwataka wananchi wadharau vitisho vinavyotolewa na CCM kwani ni tabia ya vyama tawala duniani kote pindi inapotokea wanataka kuondolewa kwa kutumia sanduku la kura, huishia kutoa visingizio mbalimbali ambavyo havina msingi.

Alisema baada ya kuona kimebanwa mbavu chama hicho kimeanza kutoa maneno ya kumkatisha tamaa Lowassa kwa kumtaja kuwa ni mmiliki wa Kampuni ya Richmond ilihali Serikali inajua ukweli kuhusu suala hilo.

Mbatia alisema kushindwa kumtaja mmiliki wa kampuni hiyo inatokana na kuwa na chama legelege kuzaa Serikali ambayo kila siku imekuwa ikilalamika kuliko kuchukua hatua.

Alisema chama hicho kimekuwa kikizalisha mambo ambayo si kweli kuwa Lowassa alikwenda kanisani kuomba kura wakati alikwenda na familia yake kwa ajili ya kuombewa.

“Lowassa alikwenda kanisani kushiriki katika ibada kuomba viongozi wa dini wamwombee, hakwenda kwa waganga wala makaburini, bali kama wanavyofanya wengine alikwenda kanisani kuomba aombewe, lazima tuangalie kila tunachozungumza kisije kuleta athari,” alisema Mbatia na kuongeza.

“Tunatambua uwepo wa Mwenyezi Mungu ndiyo maana tunasema kuwa Mungu ibariki Tanzania Mungu ibariki Afrika, Lowassa hakwenda kanisani kuomba kura, Watanzania tumwombee ili atufikishe tunakohitaji kufika,” alisema.

Aliwataka Watanzania kuimarisha amani iliyopo kwani ni matokeo ya kazi kubwa iliyofanywa na Mwalimu Nyerere ambapo leo hii Tanzania imekuwa kimbilio la wakimbizi wengi kutoka nchi mbalimbali za Afrika.

Alisema iwapo amani hiyo itapotea, hakuna sehemu ya kukimbilia kwani maeneo yaote karibia nchi zote zimejaa vurugu.

Mbatia alisema Lowassa na Sumaye wanachukiwa na CCM kwa kuwa walihama katika chama hicho na kuingia upinzani, walifanya hivyo kwa ajili ya kutaka kuleta mabadiliko ndani ya nchi hii kwakuwa ndani ya CCM haiwezekani.

“Hivi jamani unaweza kusukuma gari ukiwa ndani ya gari iwapo litakuwa limepata tatizo? Jibu huwezi, itabidi ushuke na kulisukuma ukiwa nje, ndivyo walivyofanya Sumaye na Lowassa, huwezi kufanya mabadiliko ndani ya CCM ukiwa humo,” alisema Mbatia.

Alisema CCM wanasema wapinzani hawana uzoefu, sasa wamechukua watu wenye uzoefu kama Sumaye ambaye amekuwa Waziri Mkuu kwa miaka kumi ndani ya Serikali ya CCM, ataliongoza vema jahazi la Ukawa

Aliwataka CCM kuingia katika mdahalo kujadili kwa hoja Watanzania wapime nani wenye hoja nzuri zitakazoweza kuivusha nchi hii hapa ilipo na kuifikisha katika nchi ya ahadi.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
592,000SubscribersSubscribe

Latest Articles